Tafuta

Jumuiya ya Kimataifa tarehe 20 Juni 2020 inaadhimisha Siku ya Wakimbizi Duniani, sanjari na kumbukumbu ya Miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Siku hii hapo mwaka 2000. Jumuiya ya Kimataifa tarehe 20 Juni 2020 inaadhimisha Siku ya Wakimbizi Duniani, sanjari na kumbukumbu ya Miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Siku hii hapo mwaka 2000. 

UN: Siku ya Wakimbizi Duniani 2020: Kumbukumbu ya Miaka 20

Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi, UNHCR, zinaonesha kwamba, kuna watu takribani milioni 80 kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wamelazimika kuishi kama wakimbizi, wahamiaji, watu wasiokuwa na makazi maalum pamoja na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa. Kuna watoto milioni 13 ambao wamelazimika kuishi kama wakimbizi na wahamiaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Umoja wa Mataifa, tarehe 20 Juni 2020 unaadhimisha Kumbukumbu ya Miaka 20 tangu Siku ya Wakimbizi Duniani ilipoanzishwa kunako mwaka 2000, kama kumbukumbu ya Mkataba wa Wakimbizi Duniani uliotiwa sahihi na Jumuiya ya Kimataifa kunako mwaka 1951. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres katika maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi Duniani inayoadhimishwa na Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 20 Juni anasema, Umoja wa Mataifa hauna budi kujifunga kibwebwe ili kukomesha vita, kinzani na migogoro ya kijamii inayoendelea kusababisha mamilioni ya watu kuyakimbia makazi na nchi zao ili kutafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi.

Takwimu zilizotolewa na Bwana Filippo Grandi, Kamishna mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi, UNHCR, zinaonesha kwamba, kuna watu takribani milioni 80 kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wamelazimika kuishi kama wakimbizi, wahamiaji, watu wasiokuwa na makazi maalum pamoja na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa. Kuna watoto milioni 13 ambao wamelazimika kuishi kama wakimbizi na wahamiaji. Hii inatokana na ukweli kwamba, Jumuiya ya Kimataifa imeshindwa kudhibiti vita, kinzani na mipasuko mbali mbali ya kijamii hasa nchini Siria yenye wakimbizi na wahamiaji milioni 13.2 na inafuatiwa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo, DRC.

Idadi ya wakimbizi na wahamiaji duniani tangu mwaka 2012 imeendelea kuongezeka maradufu kutokana na vita, ghasi na kinzani za kijamii. Hadi sasa Jumuiya ya Kimataifa imeshindwa kudhibiti wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani. Kuna wasi wasi mkubwa kwamba, pengine, wimbi hili, likaongezeka maradufu ifikapo mwaka 2021, ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa itashindwa kusimama kidete kupambana na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Takwimu zinaonesha kwamba, katika kipindi cha Mwaka 2019, watu zaidi ya milioni 46 walikuwa ni watu wasiokuwa na makazi maalum ndani mwa nchi zao wenyewe. Watu zaidi ya milioni 26 walilazimika kuvuka mipaka ya nchi zao ili kutafuta hifadhi na usalama zaidi. Katika sakata hili, Venezuela nayo ni kati ya nchi zenye wakimbizi na wahamiaji wapatao milioni 3.6.

Kwa upande wa Kanisa Katoliki, Siku ya 106 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2020 itaadhimishwa Jumapili, tarehe 27 Septemba 2020 kwa kuongozwa na kauli mbiu: “Kama ilivyo kwa Kristo Yesu, alilazimishwa kwenda uhamishoni”. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutafakari tema hii na kuchukua hatua kama sehemu ya sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia. Idara ya Wahamiaji na Wakimbizi katika Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na Fungamani inasema, kauli mbiu ya Mwaka 2020 inachota uzoefu na mang’amuzi yake kutoka kwa Kristo Yesu, ambaye wazazi wake, yaani Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu, walilazimika kusalimisha maisha yake kwa kukimbilia nchini Misri.

Hii ni changamoto kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kukuza na kudumisha utamaduni wa ukarimu. Ujumbe huu, utatoa ufafanuzi wa kina kuhusu: Kujifunza ili kufahamu; kujenga ujirani mwema ili kuhudumia; kusikiliza ili kujipatanisha; kushirikishana na wengine ili kukua na kukomaa; kuwahusisha wengine, ili kuwaendeleza na hatimaye, kushirikiana ili kujenga. Kutokana na unyeti wa wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia, Idara ya Wahamiaji na Wakimbizi katika Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na Fungamani kila mwezi, itajitahidi kuhakikisha kwamba, inaendesha kampeni, kwa njia ya tafakari makini, ili kuwasaidia waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuweza kujiandaa kikamilifu katika maadhimisho haya.

Siku ya Wakimbizi Duniani 2020
20 June 2020, 14:35