Tafuta

Vatican News
2020.06.17 Siku ya Wakimbizi duniani 2020.Raul Marques,ni mtunzi na mwandishi wa kitabu cha watoto juu ya wahamiaji. 2020.06.17 Siku ya Wakimbizi duniani 2020.Raul Marques,ni mtunzi na mwandishi wa kitabu cha watoto juu ya wahamiaji. 

Ni wakati sasa wa kuelezea mshikamano kwa wakimbizi ulimwenguni!

Katika Siku ya Wakimbizi Ulimwenguni,Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi(UNHCR)linasherehekea nguvu,ujasiri na uvumilivu wa mamilioni ya wakimbizi.Sasa ni wakati wa kuelezea mshikamano wao kwa njia thabiti kupitia ishara rahisi.

Na Sr. Angela Rwezaula- Vatican

Katika ulimwengu ambamo vita na vurugu hulazimisha maelfu ya familia kukimbia makazi yao kila siku, Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR, linaamini kuwa huu ni wakati wa kuonyesha viongozi wa ulimwengu kuwa umma wa ulimwengu ni upande wa wakimbizi. Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia ujumbe wake wa Siku hii  ya wakimbizi duniani tarehe 20 Juni ameeleza ahadi ya Umoja wa Mataifa ya kukomesha migogoro na mateso yanayosababisha mamilioni ya watu kuwa wakimbizi. Bwana Guterres amesema kuwa Umoja wa Mataifa unaahidi kufanya kila lililo katika uwezo wake kukomesha migogoro na mateso ambayo imesababisha takribani watu milioni 80 wanawake, watoto na wanaume kote duniani kuyakimbia makazi yao na kujikuta ukimbizini.

Utambuzi wa ukarimu na ubinadamu wa jamii wenyeji

Akifafanua ukubwa wa tatizo hilo, Katimbu Mkuu Bwana Guterres amesema cha kutisha zaidi ni kuwa watu milioni 10 kati ya hawa, waliyakimbia makazi yao katika mwaka mmoja uliopita tu. Katika ujumbe wake aidha wamezishukuru nchi na jamii ambazo zinawapokea wakimbizi licha ya kuwa nazo zina mahitaji. “Leo, pia tunatambua ukarimu na ubinadamu wa jamii wenyeji na nchi ambazo mara nyingi zinakabiliwa na wasiwasi wa kiuchumi na kiusalama. Tunastahili kuzipatia nchi hizi shukrani, usaidizi wetu na uwekezaji.”

Mchango wa wakimbizi,baadhi ni kama nesi,daktari,wanasayansi

Akizungumzia namna ugonjwa wa COVID-19 unavyoongeza tishio kwa wakimbizi, Bwana Guterres amekumbushia taarifa ya sera aliyoieleza hivi karibuni kuhusu COVID-19 kwamba alitoa wito kwa serikali duniani kote kuwahusisha katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo watu walioko katika hatua za kuhama au ukimbizini. Vile vile Katibu ameutambua pia mchango wa wakimbizi na walifukuzwa makwao kwamba baadhi yao pamoja na kuwa wakimbizi lakini wamekuwa wakifanya kazi kama nesi, daktari, wanasayansi, walimu na pia kurejesha fadhila kwa jamii zinazowapokea. “Katika siku hii ya wakimbizi duniani, tunawashukuru wakimbizi kwa urasilimali wao na uamuzi wa kujenga upya maisha yao na kuboresha Maisha ya wale wanaowazunguka. Leo na kila siku tunasimama kwa umoja na mshikamano na wakimbizi na kutambua jukumu letu la msingi la kuwalinda wanaokimbia vita na mateso.”

20 June 2020, 14:56