Tafuta

Vatican News
Mahakama ya Katiba Nchini Burundi imeonesha ya kutaka kumtangaza hivi karibuni Rais mteule Jenerali Evariste Ndayishimiye! Mahakama ya Katiba Nchini Burundi imeonesha ya kutaka kumtangaza hivi karibuni Rais mteule Jenerali Evariste Ndayishimiye!  (AFP or licensors)

Mahakama ya Katiba Burundi: Rais mteule kuapishwa hivi karibuni!

Rais Magufuli amemhakikishia Rais mteule wa Burundi kwamba, Tanzania itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake wa karibu na Burundi kwa kuwa nchi hizi mbili ni majirani, marafiki na ndugu wa kihistoria. Rais Magufuli pamoja na watanzania wote wanaungana na wananchi wa Burundi katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.. Ametoa pole kwa wananchi wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania, tarehe 13 Juni 2020 amezungumza kwa njia ya simu na Rais mteule wa Jamhuri ya Watu wa Burundi Jenerali Evariste Ndayishimiye na kumpongeza kwa uamuzi wa Mahakama ya Katiba nchini Burundi iliyoagiza Rais mteule aapishwe haraka. Katika mazungumzo baina ya viongozi hawa wawili kadiri ya taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, imeonesha kwamba, Rais Magufuli amemtakia heri Rais mteule Evariste Ndayishimiye kuelekea kuapishwa kwake kuwa Rais wa Jamhuri ya Burundi kunakotarajiwa kufanyika hivi karibuni.

Rais Magufuli amemhakikishia Rais mteule wa Burundi kwamba, Tanzania itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake wa karibu na Burundi kwa kuwa nchi hizi mbili ni majirani, marafiki na ndugu wa kihistoria. Rais Magufuli amerudia kumpa pole kwa msiba wa kuondokewa na Rais Pierre Nkurunziza aliyefariki dunia hivi karibuni. Rais Magufuli pamoja na watanzania wote wanaungana na wananchi wa Burundi katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo. Amemwomba, kufikisha salam zake za rambirambi kwa wananchi wote wa Burundi na kuwasihi waendelee kuwa watulivu na wastahimilifu.

Wakati huo huo, Serikali ya Tanzania imetangaza siku tatu za maombolezo kuanzia Jumamosi tarehe 13 Juni 2020 hadi Jumatatu tarehe 15 Juni 2020. Kipindi hiki chote, bendera zitapeperushwa nusu mlingoti. Hii ni heshima kubwa kwa Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi, nchi ambayo ina uhusiano wa karibu sana na Tanzania kutokana na urafiki na historia yake. Itakumbukwa kwamba, Burundi pia ni nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Ni kiongozi aliyeipenda Jumuiya hii na Tanzania katika ujumla wake. Rais Magufuli amerudia kutoa pole kwa Mama Denise Bucumi Nkurunziza, mjane wa Rais Nkurunziza, familia, serikali na wananchi wote wa Burundi kwa kuondokewa na mpendwa wao. Anamwombea kwa Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, aweze kuipumzisha roho yake mahali pema peponi, Amina.

13 June 2020, 14:53