Tafuta

Jumuiya ya Kimataifa kila Mwaka ifikapo tarehe 8 Juni inaadhimisha Siku ya Bahari Duniani. Kwa mwaka 2020, Jumuiya ya Kimataifa imejielekeza zaidi katika tafakari ya tatizo na changamoto za plastiki. Jumuiya ya Kimataifa kila Mwaka ifikapo tarehe 8 Juni inaadhimisha Siku ya Bahari Duniani. Kwa mwaka 2020, Jumuiya ya Kimataifa imejielekeza zaidi katika tafakari ya tatizo na changamoto za plastiki. 

Maadhimisho ya Siku ya Bahari Kimataifa 2020: Taka za Plastiki

Maadhimisho ya Mwaka 2020 ni tafakari kwa Jumuiya ya Kimataifa kuangalia athari za taka za plastiki zinazotupwa baharini. Kila mwaka inakadiriwa kwamba, kuna tani milioni nane za taka za plastiki zinazotupwa baharini. Siku ya Bahari kwa Mwaka 2020 ni sehemu ya mpango mkakati wa Jumuiya ya Kimataifa kukuza utamaduni wa kuhifadhi taka za plastiki, ili kutunza mazingira bora.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu kufikia mwaka 2030 ni mchakato wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inajizatiti katika kutokomeza umaskini, baa la njaa na magonjwa duniani. Watu wanapaswa kupatiwa elimu bora, kwa kuhakikisha usawa wa kijinsia pamoja na uwezeshaji wa wanawake na wasichana wote. Jumuiya ya Kimataifa inataka kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na upatikanaji wa maji safi na salama; nishati mbadala kwa gharama nafuu pamoja na uwepo wa mipango bora ya miji na makazi ya watu, ili kudumisha usalama na upatikanaji wa maendeleo fungamani ya binadamu. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujifunga kibwebwe kulinda mazingira pamoja na kudumisha amani duniani! Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu anasema, Umoja wa Mataifa una wajibu wa kuwasaidia wananchi sehemu mbali mbali za dunia kudumisha ekolojia, kwa kujikita katika wongofu wa kiekolojia, ili kuleta mabadiliko yanayokusudiwa kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”.

Huu ni wajibu fungamani kwani madhara yake yanawaathiri watu wote bila ubaguzi. Uchafuzi mkubwa wa mazingira unaendelea kuhatarisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi duniani. Malengo ya Maendeleo Endelevu yanapaswa kuvaliwa njuga kwa kusikiliza kilio cha Dunia Mama pamoja na kujibu kilio cha maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kila mwaka, ifikapo tarehe 8 Juni, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Bahari Duniani, kama sehemu ya kumbukumbu endelevu ya Mkutano wa Kimataifa Kuhusu Mazingira na Maendeleo Fungamani ya Binadamu, uliofanyika mwaka 1992 huko mjini Rio de Janeiro, nchini Brazil. Maadhimisho ya Mwaka 2020 ni tafakari kwa Jumuiya ya Kimataifa kuangalia athari za taka za plastiki zinazotupwa baharini kila kukicha. Kila mwaka inakadiriwa kwamba, kuna tani milioni nane za taka za plastiki zinazotupwa baharini.

Maadhimisho ya Siku ya Bahari kwa Mwaka 2020 ni sehemu ya mpango mkakati wa Jumuiya ya Kimataifa kukuza utamaduni wa kuhifadhi taka za plastiki, ili kuiwezesha dunia kuwa bora zaidi baada ya maambukizi makubwa homa ya mapafu inayosababishwa naVirusi vya Corona, COVID-19, kupita au kupunguza makali yake. Lengo ni kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kuboresha utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, changamoto inayovaliwa juba na Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya sera na mikakati yake ya shughuli za kichungaji. Mabadiliko ya tabianchi yanaendelea kusababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao kutokana na mafuriko makubwa, ukame wa kutisha; kuongeza kwa dhoruba na vimbunga; mambo ambayo yanaendelea kusababisha madhara makubwa katika sekta ya uchumi, nishati na miundo mbinu ya usafirishaji; afya na maendeleo fungamani ya binadamu katika ujumla wake.

Takwimu zinaonesha kwamba, kumekuwepo na ongezeko kubwa la joto duniani, hali ambayo imesababisha ongezeko la kina cha bahari. Uzalishaji wa hewa ya ukaa nao umeongezeka maradufu ikilinganishwa na miaka ya 1990. Kwa upande wake, Baraza la Maaskofu Katoliki Malta katika maadhimisho haya linabainisha kwamba, Bahari ni rasilimali kubwa, ikitumika barabara inaweza kusaidia kusukuma mbele mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Huu ni wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, kadiri ya Waraka wa Kitume wa Papa Francisko, “Laudato si” pamoja na maelekezo yanayotolewa na Jumuiya ya Kimataifa. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuhakikisha kwamba, inashikamana kwa dhati ili kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kutekeleza kwa vitendo makubaliano ya Mkutano wa 21 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, Cop21 uliofanyika mjini Paris, nchini Ufaransa, kuanzia tarehe 30 Novemba hadi 12 Desemba 2015. Jumuiya ya Kimataifa ilipitisha mkataba mpya wa Paris ambao umeweka historia mpya kwa nchi 195 kukubali kushirikiana katika kushughulikia athari na changamoto za mabadiliko ya tabianchi kwa kupitisha mkataba mpya wa kisheria unaozijumuisha nchi zote katika kupunguza gesi joto duniani.

Makubaliano haya yanatoa taswira, mwelekeo, na malengo ambayo nchi zote duniani zitashiriki katika kupunguza gesi joto ili kufikia lengo la dunia la kutokuongezeka kwa wastani wa joto la dunia kwa zaidi ya nyuzi 20C au 1.50C. Hatua hii ni muhimu katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo zimeendelea kuathiri nchi changa duniani hasa katika sekta muhimu zinazochangia ukuaji wa uchumi, ustawi na maendeleo ya wengi kama vile: kilimo, mifugo, uvuvi na utalii. Baraza la Maaskofu Katoliki Malta linabainisha kwamba, matatizo na changamoto zilizojitokeza kwa Jumuiya ya Kimataifa katika kukabiliana na janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, iwe ni fundisho kwa Jumuiya ya Kimataifa kushikamana na kushirikiana kwa dhati katika kukabiliana na changamoto mamboleo. Hii inatokana na ukweli kwamba, watu wote wanategemeana na kukamilishana na wala hakuna mtu au taifa lolote lile linaloweza kujimwambafai kwamba, linajitegemea na kujitosheleza lenyewe! Utunzaji bora wa bahari na mazingira yake ni sehemu ya utekelezaji wa haki jamii.

Siku ya Bahari 2020

 

 

12 June 2020, 07:09