Vatican News
Watafiti nchini Uingereza wamesifu dawa ya Steroid dexamethasone iliyowatibu wagonjwa mahututi wa COVID-19. Watafiti nchini Uingereza wamesifu dawa ya Steroid dexamethasone iliyowatibu wagonjwa mahututi wa COVID-19.  (REUTERS)

DUNIA#coronavirus:Watafiti wamesifu dawa ya Steroid-dexamethason kutibu wagonjwa wa covid-19!

Watafiti wamesifu dawa ya Steroid dexamethasone iliyowatibu wagonjwa mahututi wa COVID-19.Maambukizi ya virusi vya Corona yaendelea kwa kasi huko Beijing,Afrika na Brazil.Jumla ya wanajeshi 20 wa India wameuawa wakati wa makabiliano mpakani na vikosi vya China.Korea Kaskazini imetishia kupeleka jeshi katika eneo lisilo la kijeshi kati yake na Korea Kusini.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Ni zaidi ya maambukizi ya watu milioni 8 kwa kiwango cha kimataifa, ambapo janga kubwa kwa sasa ni nchini Brazil wakiwa wamefika vifo karibia 1,300 katika masaa 24 yaliyopita. Wakati huo huo Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limetoa ufafanuzi kuwa ni “mafanikio ya kisayansi”, kutoka na  dawa ya steroid iliyotengenezwa na watafiti wa Uingereza. Watafiti katika chuo kikuu cha Oxford nchini Uingereza wamesifia kile walichokitaja kuwa ni  ‘hatua kubwa’ katika kuwatibu wagonjwa wa virusi vya corona au  COVID-19. Hii ni baada ya dawa aina ya steroidi dexamethasone kuthibitishwa kuwa na uwezo wa kuepusha hatari ya kifo miongoni mwa wagonjwa mahututi. Utafiti uliofanywa kwa zaidi ya wagonjwa 2,000, umeonyesha kuwa dawa hiyo ilipunguza hatari ya mgonjwa kufa kutoka asilimia 40 hadi asilimia 28, hasa hasa wagonjwa ambao hawangeweza kupumua bila usaidizi wa mashine. Matokeo ya awali pia yameonyesha kuwa dawa hiyo iliweza kupunguza hatari ya vifo kutokea miongoni mwa wagonjwa waliowekewa oksijeni bila ya mashine kutoka asilimia 25 hadi 20. Mtafiti kwa jina Peter Horby katika chuo cha Oxford amesema hiyo ndiyo dawa pekee ambayo hadi sasa imethibitishwa kuweza kupunguza hatari ya kifo kwa wagonjwa mahututi wa COVID-19.

Virusi vya corona nchini China

Katika mapambano dhidi ya Virusi vya corona inayoendelea  ulimwenguni kote, kwa mara nyingine tena Soko kuu la jumla kwenye jiji la Beijing nchini China limefungwa baada ya visa vya maambukizi ya virusi vya Corona kuhusishwa na soko hilo. Kesi mpya jijini Beijing zimerekodia kwani Mamlaka zimewaweka karantini karibia watu 140 waliokutana kwa karibu na visa hivyo vilivyothibitishwa na kutengwa mitaa 28, Shule za msingi na za chekechea na vyuo vikuu na mahali popote pa mikusanyiko vimefungwa. Viwanda na ofisi vimeachwa wazi na pia wamefuta safari za ndege kwa asilimia 70%.

Maambukizi ya virusi vya Corona yaendelea hata barani Afrika

Ofisi ya Shirika la Afya Duniani WHO barani Afrika tarehe 11 Juni ilitoa habari kuwa, tangu kuripotiwa kwa mtu wa kwanza aliyeambukizwa virusi vya Corona barani Afrika katikati ya mwezi Februari, hivi sasa idadi ya watu waliothibitishwa kuambukizwa virusi hivyo imezidi laki 2, na watu zaidi 5,600 wamekufa kutokana na virusi vya Corona, na maambukizi ya virusi hivyo bado yanazidi kuenea. Takwimu kutoka idara hiyo zinaonesha kuwa miongoni mwa nchi 54 za Afrika, maambukizi katika nchi 10 yanachukua asilimia 80 ya jumla. Afrika Kusini imeathiriwa zaidi, na inachukua asilimia 25 ya kesi za maambukizi ya virusi hivyo barani Afrika.

Mivutano nchini India na China

Ongezeko la mivutano linazidi huko Himalaya ambapo kwa wiki sasa wanakabiliana katika ya India na China katika Kanda ya Ladakh. Jeshi la India limesema jumla ya wanajeshi 20 wa India wameuawa wakati wa makabiliano ya mpakani, kati yao na vikosi vya China. Jeshi la India limesema hayo tarehe 16 Juni 2020, baada ya wiki kadhaa za machafuko kati yao. Kwenye taarifa jeshi la India limesema makabiliano yalizuka usiku wa kuamkia tarehe 16 Juni, katika bonde la Galwan wakati wa kutuliza machafuko. Hii ni mara ya kwanza katika miongo mingi kwa mataifa hayo mawili makubwa barani Asia kukabiliana. Hata hivyo Wizara ya Mambo ya nchi za nje ya China imethibitisha makabiliano hayo, lakini bila ya kutoa maelezo kuhusu vifo.

Korea Kaskazini imetishia kupeleka jeshi katika eneo lisilo la kijeshi kati yake na Korea Kusini

Jeshi la Korea Kaskazini, limetishia kuingia tena, katika eneo lililoko kati yao na Korea Kusini, ambalo kwa mujibu wa makubaliano waliyosaini, halipaswi kuwa na shughuli za kijeshi. Kwenye taarifa ambayo imeripotiwa na shirika la habari la nchi hiyo (KCNA), na pia kunukuliwa na shirika la habari la Korea Kusini Yonhap, mkuu wa jeshi la Korea Kaskazini amesema wanafuatilia kwa karibu hali ya sasa, ambapo uhusiano kati ya nchi hizo mbili, unazorota, na wanajiandaa kijeshi kwa hatua yoyote itakayoamuliwa na serikali.

17 June 2020, 11:25