Tafuta

Vatican News
Coronavirus:mstari wa watu katika kituo cha chakula Coronavirus:mstari wa watu katika kituo cha chakula   (ANSA)

UN#coronavirus:Umoja wa Mataifa waomba dola bilioni 6.7 kusaidia watu dhidi ya janga!

Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuratibu Misaada ya Kibinadamu OCHA amesema hivi sasa COVID-19 imefika katika kila nchi,kukiwa na karibu wagonjwa milioni 3,596,000 waliothibitishwa na vifo zaidi ya 247,650 duniani kote hivyo ni lazima kuchukua hatua madhubuti ili kuepuka athari kubwa za mlipuko wa virusi hivi vya corona na kwa njia hiyo ombi la bilioni 6.7 zinahitajika kulinda watu dhidi ya janga la corona.

Bwana Lowcock Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA tarehe 7 Mei 2020 ametoa wito wa kuchukua hatua Madhubuti ili kuepuka athari kubwa za mlipuko wa janga la corona au COVID-19 wakati akitoa ombi la dola bilioni 6.7 amelezea mipango ya kimataifa ya kupambana na virusi vya corona katika nchi zisizojiweza.  Bwana Lowcock amesema kilele cha ugonjwa huo katika nchi masikini kabisa bado hakijafika na kinatarajiwa zaidi ya miezi mitatu hadi sita ijayo. Hata hivyo amesema tayari kuna ushahidi  wa kipato kuporomoka na ajira kutoweka, minyororo ya usafirishaji wa chakula nayo imeathirika na bei kupanda na pia watoto wakikosa likizo na vyakula.

Kadhalika mkuu huyo amesisitiza kwamba hivi sasa mfumo wa masuala ya kibinadamu unachukua hatua ili kuepuka kuongezeka kwa vita, njaa, umasikini na magonjwa kutokana na janga hili na mdororo wa kiuchumi unaoikumba dunia hivi sasa. Mpango mpya wa kimataifa wa masuala ya kibinadamu uliotangazwa tarehe 7 Mei 2020 umepanua wigo wa msaada wake na sasa kujumuisha nchi nyingine zisizojiweza na kuwa katika hali hatarishi zikiwemo Benini, Djibout, Liberia, Msumbiji, Pakistan, Ufilipino, Sierra Leone, Togo na Zimbabwe ambapo mipango pia inahusisha hatua za kukabiliana na ongezeko la kutokuwa na uhakika wa chakula.

Ombi lilotolewa la fedha na pia mipango mipya ya msaada wa kibinadamu limezinduliwa kwenye mkutano uliofanyika kwa njia ya mtandao mwenyeji akiwa mkuu wa OCHA Bwana Mark Lowcock  akishirikiana na mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula WFP  Bwana David Brasley, mkurugenzi wa shirika la afya duniani WHO wa kitengo chadharura za kiafya Bwana Mike Ryan, Rais wa Oxifarm Marekani Bwana Abby Maxima  na Kamishina mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR Bwana Filippo Grandi. Mpango huo ulizinduliwa mara ya kwanza mwezi Machi na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Akizungumzia umuhimu wa ombi la leo mkuu wa OCHA Bwana Lowcock amesema “Janga la COVID-19 linatuumiza sote lakini athari kubwa na mbaya zitakuwa katika nchi masikini kabisa duniani. Katika nchi masikini tayari tunashuhudia uchumi ukisinyaa kutokana na kushuka kwa mapato ya kusafirisha nje bidhaa, kupungua kwa kiwango cha fedha zinazotumwa toka nje na kutoweka kwa utalii. Tusipochukua hatua sasa lazima tujiandae kwa ongezeko kubwa la migogoro, njaa na umasikini. Hali ya baa la njaa inanyemelea.” Aidha emesisitiza kwamba endapo hatutawasaidia masikini hususan wanawake na wasichana na makundi mengine yaliyo katika hatari wakati huu yakipambana na janga la corona na athari za mdororo wa kimataifa wa uchumi , basi tutakabiliwa na athari mbaya za kuzishughulikia kwa miaka mingi ijayo ambazo zitadhihirika kuwa za mauamivu makali zaidi na za gharama kubwa zaidi kwa kila mtu.

Mpango wa kimataifa wa kushughulikia janga la COVID-19 ni nyenzo ya jumuiya ya kimataifa ya kuchangisha fedha ili kukabiliana na athari za virusi vya corona katika nchi za kipato cha kati na cha chini na kusaidia juhudi zao za kupambana na janga hilo. Mpango huo unaleta pamoja maombi ya Shirika la Afya duniani (WHO) na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya kibinadamu. Mashirika yasiyo ya kiserikali yaani NGOs na vyama vya NGOs yamekuwa chachu kubwa katika kuunda mpango huo. Na ni wadau wakubwa katika kuhakikisha fedha zinapatikana na fedha zinaweza kufikiwa kupitia wao. Mpango huo unatoa msaada na ulinzi ambao unaweka kipaumbele kwa walio katika hatari zaidi. Hawa ni pamoja na wazee, watu wenye ulemavu na wanawake na wasichana, ukizingatia kwamba janga la COVID-19 limezidisha kiwango cha ubaguzi uliokuwepo, pengo la usawa na ukatili wa kijinsia. Pia mpango unajumuisha hatua za kukabiliana na ongezeko la kutokuwepo na uhakika wa chakula.

Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa WHO Dk. Tedros Ghebreyesus amesema “idadi ya wagonjwa katika nchi nyingi zilizojumuishwa kwenye mpango wa usaidizi wa kibinadamu inaweza kuwa ndogo lakini tunajua kwamba uwezo wa ufuatiliaji, upimaji maabara na mifumo ya afya katika nchi hizi ni dhaifu. Hivyo kuna uwezekano mkubwa kwamba kuma maambukizi yanayoendelea kwenye jamii ambayo bado hayajabainika.” Pia Dk Tedros amesema kwamba wakati huohuo hatua zingine za kuzuia watu kusalia majumbani na nyinginezo za kuepuka maambukizi zina athari kubwa katika huduma muhimu za afya. Hivyo amesema ni muhimu sana kuhakikisha huduma hizi kuanzia chanjo, hadi huduma za afya ya uzazi, huduma za usafi na huduma za afya ya akili.

Naye Bwana Filippo Grandi, kamishina mkuu wa wakimbizi akitoa  sauti yake katika ombi hilo amesema“janga hili linaacha vidonda vikubwa kote duniani , kwa watu ambao walikimbia vita na mateso athari za mlo na kipato chao cha kila siku na kwa jamii zinazowahifadhi zimekuwa kubwa sana. Kwa kushirikiana na wadau wetu NGO, Umoja wa Mataifa umedhamiria kuhakikisha tunawasaidia wakimbizi, wakimbizi wa ndani, watu wasio na utaifa na jamii zinazowahifadhi, na kuhakikisha kwamba wanajumuisha katika hatua za afya za umma na hifadhi ya jamii.” Pia amesisitiza kwamba mahitaji yao ni makubwa lakini siyo ya kiwango cha kutosaidia, na ni kwa hatua za pamoja tu ndiyo dunia itaweza kulishinda tishio hili la janga la corona na kuokoa maisha.” Hatua ambazo ni za wakati, za kujitolea na za aina mbalimbali kutoka kwa washirika wetu wote ni muhimu sana”.

Hali kadhalika kwa upande wa maoni ya mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula WFP Bwana David Brasly akisisitiza umuhimu wa shikamano katika ombi la leo amesema “Katika siku yoyote WFP inatoa msaada wa kuokoa maisha kwa karibu watu milioni 100, endapo tutashindwa kuendelea na operesheni hizo muhimu basi janga hili la kiafya muda si mrefu litageuka janga la njaa, ni muhimu kwa jumuiya ya kimataifa kutimiza hatua hizi za kibinadamu na kuweka mfumo imara wa mipango ambayo itawalinda raia walio katika hatari zaidi dhidi ya majanga ya kibinadamu.”

Hata hivyo tangu mpango huo ulipozinduliwa 25 Machi mwaka huu dola bilioni 1 zimekwisha changwa kutoka kwa wahisani. Fedha hizo zinajumuisha dola milioni 166 kutoka mfuko wa OCHA za kusaidia nchi 37, dola milioni 95 kutoka mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa CERF na dola milioni 12 kutoka mifuko ya usaidizi katika nchi 12.

08 May 2020, 12:03