Tafuta

Vatican News
Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 25 Mei inaadhimisha Siku ya Umoja wa Afrika inayopania kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa nchi za Kiafrika katika medani mbali mbali za maisha. Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 25 Mei inaadhimisha Siku ya Umoja wa Afrika inayopania kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa nchi za Kiafrika katika medani mbali mbali za maisha. 

Siku ya Umoja wa Afrika: 25 Mei 2020: Vita Dhidi ya COVID-19

Umoja wa Afrika: Kumbukizi la Miaka 57 tangu Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika ulipoanzishwa yanasherehekewa wakati bado kuna janga kubwa la maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Licha ya changamoto zote hizi, Serikali ya Italia itaendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na nchi za Kiafrika katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Barani Afrika. Viva Afrika!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 25 Mei, inaadhimisha Siku ya Umoja wa Afrika, kumbu kumbu endelevu ya kuanzishwa kwa Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika, OAU kunako tarehe 25 Mei 1963 huko mjini Addis Ababa, nchini Ethiopia. Kunako tarehe 11 Julai 2001, Mkutano mkuu wa OAU uliamua kuunda Umoja wa Afrika kama sehemu ya mbinu mkakati wa kukuza na kudumisha Umoja na mshikamano miongoni mwa nchi za Kiafrika na tarehe 9 Julai 2002, Umoja wa Afrika ukazaliwa rasmi! Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika ulikuwa na jukumu la kupambana na ukoloni, mifumo ya ubaguzi wa rangi, vita, njaa na umaskini, uliokuwa unadhalilisha utu, heshima na haki msingi za watu wa familia ya Mungu Barani Afrika. Umoja wa Afrika unataka kukuza na kudumisha umoja na mshikamano katika medani mbali mbali za maisha ya watu Barani Afrika: kiuchumi, kijamii, kisiasa na kitamaduni ili kuondokana na ukoloni mamboleo pamoja na ukoloni wa kiitikadi na utamaduni wa kifo, unaofumbatwa mara nyingi kwenye masharti ya misaada kwa Bara la Afrika.

Rais Sergio Mattarella wa Italia katika maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Afrika, amewapongeza wanadiplomasia wanaoziwakilisha nchi zao kutoka Barani Afrika. Maadhimisho ya Mwaka huu 2020 ambao ni kumbukizi la Miaka 57 tangu Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika ulipoanzishwa yanasherehekewa wakati bado kuna janga kubwa la maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Licha ya changamoto zote hizi, Serikali ya Italia itaendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na nchi za Kiafrika katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu Barani Afrika. Ni matumaini ya Rais Mattarella kwamba, Nchi zinazozunguka Bahari ya Mediterrania zitaendelea kuwa aminifu kwa wito wake wa kihistoria na kijiografia kama daraja linalounganisha Bara la Afrika na Ulaya. Huu ni wakati kwa Umoja wa Afrika kujizatiti zaidi katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19 vinavyosababisha maafa makubwa kwa watu, familia pamoja na kuvuruga mfumo mzima wa uzalishaji na utoaji wa huduma.

Umoja wa Afrika kwa kushirikiana na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, EU na kwa namna ya pekee, Italia, wanapaswa kushikamana kwa dhati ili kupambana na athari za Virusi vya Corona, COVID-19, ili kufufua tena uchumi kwa kuimarisha soko la bidhaa kutoka Afrika, kwa kuzingatia tunu msingi za ustawi, maendeleo na mafungamano, ili kuliwezesha Bara la Afrika na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya kushikamana kwa nguvu zaidi. Huu ni wakati wa kuangalia ya mbeleni zaidi, ili kuimarisha moyo wa ushirikiano, ili kusimama kidete kulinda, amani, utu, heshima, ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu. Kutokana na muktadha huu, Serikali ya Italia, itaendelea kujikita katika mchakato wa upatanisho wa kitaifa sanjari na kuunga mkono juhudi za Umoja wa Mataifa za kutaka kusitisha vita sehemu mbali mbali za dunia, ili kukusanya nguvu kwa ajili ya kupambana na Virusi vya Corona, COVID-19.

Ni kwa njia hii, Jumuiya ya Kimataifa itaweza kuonesha mshikamano wa kimataifa ili kukabiliana na matatizo pamoja na changamoto zinazoibuliwa kutoka katika masuala ya kiuchumi, kifedha na kwa namna ya pekee kabisa, na janga hili la Virusi vya Corona, COVID-19. Italia ambayo kwa Mwaka 2021 itakuwa ni Rais wa G20 inatarajia kutoa ushirikiano wa dhati kwa Umoja wa Afrika katika kutafuta suluhu ya matatizo na changamoto za Bara la Afrika. Italia na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya, itaendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na Bara la Afrika, ili kuimarisha historia ya pande hizi mbili!

Umoja wa Afrika
25 May 2020, 13:41