Shirika la Afya Duniani limeutangaza Mwaka 2020 kuwa ni Mwaka wa Kimataifa wa Wauguzi na Wakunga Shirika la Afya Duniani limeutangaza Mwaka 2020 kuwa ni Mwaka wa Kimataifa wa Wauguzi na Wakunga 

Yanayojiri: Mwaka wa Kimataifa wa Wauguzi na Wakunga 12 Mei 2020

Jumuiya ya Kimataifa imeutangaza Mwaka 2020 kuwa ni Mwaka Kimataifa wa Wauguzi na Wakunga. Jumuiya ya Kimataifa inatambua mchango mkubwa uliotolewa na Florence Nightingale katika huduma ya uuguzi na ukunga katika ulimwengu mamboleo. Jumuiya ya Kimataifa inafanya kumbukizi ya Miaka 200 tangu alipozaliwa Florence Nightingale. Kundi hili ni uti wa mgongo wa afya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Afya maana yake ni hali ya ukamilifu kimwili, kiakili, kijamii na kutokuwepo kwa maradhi. Afya bora ni nguzo na raslimali muhimu katika kuchangia ustawi, mafao na maendeleo ya mtu binafsi, familia na nchi hususan katika kuleta maisha bora na kupunguza umaskini. Kwa mantiki hii, afya inalenga kuwa na ustawi fungamani kwa jamii, kwa kuzingatia mchango wa mtu binafsi kulingana na nafasi, uwezo na fursa zilizopo katika kuleta maisha bora. Upatikanaji wa afya bora unahitaji uwezeshaji wa jamii iwe na uwezo wa kushiriki, kuamua, kupanga na kutekeleza mikakati yao ya kuwaletea maendeleo fungamani katika ngazi mbalimbali. Dr. Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Afya Duniani, WHO, anasema, Jumuiya ya Kimataifa imeutangaza Mwaka 2020 kuwa ni Mwaka Kimataifa wa Wauguzi na Wakunga. Jumuiya ya Kimataifa inatambua mchango mkubwa uliotolewa na Florence Nightingale katika huduma ya uuguzi na ukunga katika ulimwengu mamboleo. Jumuiya ya Kimataifa inafanya kumbukizi ya Miaka 200 tangu alipozaliwa Florence Nightingale.

Kimsingi, uuguzi na ukunga ni muhimu katika kupunguza maumivu kwa wagonjwa, kuboresha huduma za mama na mtoto na makundi mengine ya jamii. Huduma za uuguzi na ukunga zimezoeleka kwamba zinatolewa katika mazingira ya zahanati, vituo vya afya na hospitali tu za umma na binafsi. Hali halisi ni kuwa huduma hizo sasa zinatolewa pia nje ya vituo hivyo katika kaya na jamii. Hali hii imetokana na kuwepo kwa ongezeko la magonjwa sugu yanayohitaji tiba na matunzo ya muda mrefu, mahitaji ya huduma za utengemao na umuhimu wa ushirikishwaji wa jamii katika upangaji na utoaji wa huduma za afya. Hivyo, wigo na ubora wa huduma za uuguzi na ukunga unahitaji kuinuliwa ili kukidhi matarajio ya wananchi, uwiano, viwango na usalama. Ili kuweza kufikia matarajio haya, kuna haja ya serikali mbali mbali duniani kuunda mazingira bora zaidi ya kazi kwa wauguzi na wakunga; kwa kuhakikisha kwamba, wanalipwa vizuri stahiki zao za kazi.

Ili kuendana na mabadiliko makubwa katika sayansi ya tiba ya mwanadamu, wauguzi na wakunga wanapaswa kupewa mafunzo zaidi; kupatiwa vifaa vya kinga na tiba dhidi ya magonjwa ya milipuko na yale ya kuambukiza kama ilivyo kwa wakati huu, ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona-COVID-19. Wauguzi na wakunga wamekuwa mstari wa mbele kwa ajili ya kutoa huduma bora ya afya. Wamejisadaka bila ya kujibakiza kuokoa maisha ya watu wengi, kiasi kwamba, wengi wao wamehatarisha maisha na wengine kwa hakika wamepoteza maisha, wakati wakiwahudumia wagonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19 sehemu mbali mbali za dunia. Lakini nchini Italia, idadi ya madaktari, wauguzi na wakunga waliopoteza maisha ni kubwa zaidi, ikilinganishwa na sehemu nyingine za dunia!

Baraza la Wauguzi na Wakunga Kimataifa, “The International Council of Nurses, ICN” lililoanzishwa kunako mwaka 1899 linaloviunganisha vyama vya wauguzi na wakunga kitaifa vipatavo 130, vyenye wanachama milioni 20 linawapongeza wanachama wake wote kwa maadhimisho haya. Linasema, changamoto zote hizi zisaidie kukuza na kuimarisha vyama vya wauguzi na wakunga kitaifa na kimataifa. Kwa njia hii wauguzi na wakunga wataendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kulinda: utu, heshima na maisha ya wagonjwa wanaowahudumia. Ni jambo la muhimu sana kwa wauguzi na wakunga kuhakikisha kwamba, wanatumia kikamilifu taaluma, weledi, sheria, kanuni na taratibu za kazi ili kukuza na nidhamu, maadili na uwajibikaji kazini, kwani Jumuiya ya Kimataifa inatambua kwamba, wauguzi na wakunga ni uti wa mgongo wa huduma ya afya. Shirika la Afya Duniani, WHO linakadiria kwamba, ifikapo mwaka 2030, kutakuwepo na upungufu wa wauguzi na wakunga wapatao milioni 9! Kumbe, kuna haja kwa Serikali na wadau mbali mbali kuhakikisha kwamba, wanawezeka katika mchakato wa kuwaandaa wauguzi na wakunga kwa siku za usoni. Kundi hili ni muhimu sana katika mchakato wa maboresho ya sekta ya afya duniani!

Mwaka: Wauguzi na Wakunga
12 May 2020, 12:58