Tume Huru ya Uchaguzi Nchini Burunsi, CENI, imemtangaza Jenerali Evariste Ndayishimiye mwenye umri wa miaka 52 kutoka Chama Tawala kuwa Mshindi wa Uchaguzi Mkuu 2020, Kiti cha Urais. Tume Huru ya Uchaguzi Nchini Burunsi, CENI, imemtangaza Jenerali Evariste Ndayishimiye mwenye umri wa miaka 52 kutoka Chama Tawala kuwa Mshindi wa Uchaguzi Mkuu 2020, Kiti cha Urais. 

Jenerali Ndayishimiye Ashinda Uchaguzi Mkuu Burundi, 2020

Tume Huru ya Uchaguzi Nchini Burundi, CENI imemtangaza Jenerali Evariste Ndayishimiye aliyekuwa anapeperusha bendera ya Chama tawala cha CNDD-FDD kuwa mshindi wa uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Burundi, tarehe 13 Mei 2020 kwa kujipatia asilimia 68.72% ya kura zote halali zilizopigwa! Bwana Agathon Rwasa amejinyakulia asilimia 24.19%. Amani na utulivu ni muhimu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tume Huru ya Uchaguzi nchini Burundi, CENI imemtangaza Jenerali Evariste Ndayishimiye mwenye umri wa miaka 52, aliyekuwa anapeperusha bendera ya Chama tawala cha CNDD-FDD kuwa mshindi wa uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Burundi Jumatano tarehe 13 Mei 2020 kwa kujipatia asilimia 68.72% ya kura zote halali zilizopigwa! Bwana Agathon Rwasa amejinyakulia asilimia 24.19%. Tume Huru ya Uchaguzi nchini Burundi, CENI imesema yeyote yule ambaye hatakubaliana na matokeo anayo haki ya kutoa malalamiko yake mbele ya Mahakama ya Katiba kadiri ya sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi mkuu nchini Burundi. Katika muktadha wa matokeo ya uchaguzi mkuu yaliyotangazwa na CENI, chama tawala cha CNDD-FDD kimeshinda viti 72 katika Bunge la Seneti, Chama cha CNL kimejipatia viti 27 na Chama cha Uprona cha Makamu wa kwanza wa Rais anayemaliza muda wake Bwana Gaston Sindimwo kimeambulia kiti kimoja tu!

Historia inaonesha kwamba, Jenerali Evariste Ndayishimiye anakuwa ni rais wa tatu kuchaguliwa katika misingi ya kidemokrasia baada ya mtangulizi wake Pierre Nkurunziza (2005, 2010, 2015) na Melchior Ndadaye ( mwaka 1993). Evariste Ndayioshimiye anasubiri kuthibitishwa na Mahakama ya Katiba na hivyo kuwa rais rasmi wa taifa la Burundi.  Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi katika ujumbe wake kabla ya uchaguzi mkuu, liliwataka watu wa Mungu nchini humo, kuhakikisha kwamba uchaguzi mkuu unakuwa wa amani, huru na haki kama kielelezo cha ukomavu wa kisiasa nchini Burundi. Huu si muda wa kuendekeza kinzani za kikabila kwani madhara yake ni makubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Burundi.

Bado watu wa Mungu nchini Burundi wanakumbuka athari za vurugu na mipasuko ya kisiasa iliyojitokeza kwenye uchaguzi mkuu wa Mwaka 2015, ulioitumbukiza Burundi katika ombwe na machafuko ya kisiasa. Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi liliwataka wananchi kutumia vyema haki yao ya kupiga kura ili kurejesha tena misingi ya haki, amani na maridhiano ya kitaifa. Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi linawataka viongozi wa serikali, vyama vya kisisasa pamoja na wapambe wao kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha misingi ya amani na utulivu; upendo na mshikamano wa kitaifa. Maaskofu wanawataka watu wa Mungu nchini Burundi, kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo kwani maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Maaskofu waliwataka viongozi wa Serikali na vyama vya kisiasa kuhakikisha kwamba, wanafuata sheria, kanuni na taratibu zote za uchaguzi mkuu, ili Burundi iweze kuwapata viongozi watakaosongesha mbele gurudumu la maendeleo fungamani ya binadamu. Kwa waandishi wa habari wawe makini katika taarifa zao na kamwe wasiwe na mawakala wa: chuki, vurugu na uhasama wakati na baada ya uchaguzi mkuu. Wanasiasa wanaowania nafasi mbali mbali za uongozi wawe tayari kukubaliana na matokeo na kama kuna watu watakaopinga basi watumie taratibu zilizopo ili kudai haki yao. Uchaguzi mkuu wa Mwaka 2020 uwe ni chemchemi ya matumaini kwa watu wa Mungu nchini Burundi.

Burundi
26 May 2020, 13:13