Tafuta

Vatican News
CORONAVIRUS:Ni bora kuangalia dalili za ugonjwa wa corona ambao ni kikohozi kikavu, uchoka pia kuwa na homa, katika maeneo ambayo tayari yameathiriwa na virusi hivi. CORONAVIRUS:Ni bora kuangalia dalili za ugonjwa wa corona ambao ni kikohozi kikavu, uchoka pia kuwa na homa, katika maeneo ambayo tayari yameathiriwa na virusi hivi.  (ANSA)

Covid-19#Dhana potofu kuhusu kinga na tiba ya virusi vya virusi vya corona!

Zijue dhana potofu zilizoibuka duniani kote baada ya virusi vya corona,Covid-19 na ambazo zimefafanuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa pamoja na mashirika mengine.Ni katika muktadha wa kuweka taadhari ili kila mmoja awe na jukumu la kujilinda na kulinda wenzake lakini kwa kuepuka kabisa na dhana hizo potofu.

Tangu kuibuka kwa virusi vya corona, COVID-19, ulimwenguni kote  watu wamekuwa pia wakiibuka na dhana mbalimbali potofu  kuhusu namna ya kujikinga au kutibu maambukizi ya virusi hivyo. Shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO, kupitia tovuti yake pamoja na mengine,limechapisha dhana hizo potofu na kutoa  ufafanuzi zaidi.

Je, kujianika juani au kukaa katika nyuzi joto 25 kunaweza kuepusha na virusi vya corona?

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa linasisitiza kuwa dhana hiyo ni potofu kwani unaweza kupata virusi hivyo bila kujali kama umekaa juani muda mrefu au katika hali ya hewa yenye joto. Vile vile Shirika la Afya WHO bado  linasisitiza kuendelea kujilinda kwa kuosha mikono mara kwa mara, kuepuka kugusa macho, mdomo na pua. 

Je, kubana pumzi kwa sekunde 10 au zaidi kunaweza kuwa kipimo binafsi cha kujua kama umeambukizwa virusi vya corona?

Watu wengine wamekuwa wakiamini kuwa njia moja ya kujipima mwenyewe kama umeambukizwa na virusi vya corona, COVID-19 ni kujaribu kubana pumzi bila kupumua kwa sekunde 10 au zaidi na kwamba usipokohoa au kujisikia vibaya basi hauna virusi vya corona. Shirika la Afya  Ulimwenguni (WHO ) la Umoja wa Mataifa linasema hata nayo ni dhana potofu kwani njia hiyo haiwezi kukuthibitishia kuwa hauna virusi vya corona, pia haiwezi kukuweleza kuhusu magonjwa mengine ya mapafu. Kwa maana hiyo Shirila la Afya  WHO linasisitiza njia bora ni kuangalia dalili za ugonjwa huu ambazo ni  kikohozi kikavu, kuchoka pia kuwa na homa. Ni vema kuwasiliana na wahudumu wa afya pindi unapoona una dalili za namna hiyo ili uweze kupatiwa msaada pamoja na kuwaepusha wale ambao unaweza kukutana nao. 

Nikinywa pombe itanikinga na virusi vya corona, COVID-19?

Wako wanaoamini kuwa, unywaji wa pombe utawakinga na virusi vya corona, COVID-19, lakini  Shirika la afya la Umoja wa Mataifa linawaambia watu kama hao kuwa pombe si tu haiwezi kukukinga na virusi hivyo, bali pia unywaji wa pombe wa mara kwa mara na uliopita kiwango, unaweza kuwa hatari na kukuweka katika matatizo ya kiafya.

Je kuoga maji moto kunaweza kuepusha na virusi hivi vya corona?

La hasha! kwa kawaida joto la mwili wa binadamu hubakia katika nyuzi joto 36.5 hadi nyuzi joto 37 bila kujali joto la maji anayooga mtu.  Kimsingi, shirika la Afya duniani WHO wanakutahadharisha kwamba kuoga maji ya moto sana kunaweza kuwa hatari kwani unaweza kuunguza hata ngozi yako. Kwa maana hiyo inabidi kuendelea kutumia njia zinazoshauriwa kitaalamu kama vile kunawa  na sabuni na kuoga vile vile.

Je na kuhusu Mbu?

Kwani kuna wale ambao wanaamini kwamba huenda mbu anaweza kuwaambukiza virusi vya corona. Shirika la afya duniani WHO linasema, hapana. Ingawa unapaswa kuwadhibiti mbu ili wasikuambukize magonjwa mengine kama vile malaria, hadi hivi sasa hakuna ushahidi wowote unaoonesha kuwa wadudu hao wanaweza kusambaza virusi vya corona. Virusi vya corona, COVID-19 vinasambazwa pale ambapo maji maji hutoka kwa mtu aliyeathirika aznaposambaza kwa kuangukia mahali na baada ya kupiga chafya au kukohoa au maji maji mengine kutoka mdomoni na katika pua.

Kitunguu swaumu kina nafasi gani katika kinga na tiba ya corona?

Wako watu wenye imani kuwa ulaji wa vitunguu swaumu kunaweza kuwakinga na COVID-19. Shirika la Afya duniani (WHO ) linaeleza kuwa ijapokuwa vitunguu swaumu ni chakula cha afya, lakini hakuna ushahidi wowote kuwa kinaweza kukusaidia kuzuia kuambukizwa virusi vya corona. Nawa mikono mara kwa mara kwa kutumia sabuni na maji yanayotiririka.

01 April 2020, 12:02