Mpango mkakati wa Serikali ya Tanzania kupambana na homa ya mapafu unaosababisha na Virusi vya Corona ni kuzuia kuenea kwa Virusi vya Corona! Mpango mkakati wa Serikali ya Tanzania kupambana na homa ya mapafu unaosababisha na Virusi vya Corona ni kuzuia kuenea kwa Virusi vya Corona! 

Virusi vya Corona: Mpango mkakati wa Serikali ya Tanzania ni kuzuia!

Katika kipindi cha saa 24 jumla ya watu 292,142 duniani walibainika kuwa na virusi vya Corona kati yao watu 12,784 walifariki. Bara la Afrika watu 736 walibainika kuwa na Virusi vya Corona na kati yake watu 20 walifariki katika kipindi cha saa 24. Tanzania, Waziri Ummy alisema jumla ya watu 12 walibainika kuwa na Virusi vya Corona tangu mgonjwa wa kwanza alivyogundulika nchini Tanzania.

Na Ofisi ya Waziri Mkuu, - Dodoma.

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema Serikali inaendelea kufanya tathmini ili kuhakikisha inazuia ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona, COVID-19) isiweze kusambaa kwa kiasi kikubwa nchini. Pia, Waziri Mkuu amevishukuru vyombo vya habari nchini kwa ushirikiano wanaoutoa kwa Serikali katika kuelimisha umma namna ya kujikinga na Virusi vya Corona. Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo Jumatatu, Machi 23, 2020 wakati akizungumza na Mawaziri na Makatibu Wakuu katika Kikao Kazi kilichofanyika kwenye ukumbi wa Hazina, jijini Dodoma. Imeelezwa kuwa kinga dhidi ya virusi vya corona liwe ni jambo la kimkakati zaidi kuliko kusubiri kutibu, hivyo kwa sasa Serikali imeweka mkazo kwenye kuwahamasisha wananchi kujikinga na virusi hivyo. “…Mawaziri hakikisheni katika kipindi hiki ziara za kwenda kukagua miradi zielekezwe kwa Wakurugenzi ikibidi kwa Makatibu Wakuu, Mawaziri mnatakiwa mjikite katika kukinga Taifa na Corona.”

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema Serikali imeunda kamati tatu kwa ajili ya kukabiliana na homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi ya Corona (COVID-19). Kamati hizo ni ya Kitaifa ambayo itaongozwa na Waziri Mkuu na itahusisha baadhi ya Mawaziri, Makatibu Wakuu na Msemaji Mkuu wa Serikali. Kamati ya pili ni ya Makatibu Wakuu kutoka sekta husika na itaongozwa na Katibu Mkuu Kiongozi na kamati ya tatu ni ya Kikosi Kazi cha Taifa ambacho kitaongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto huku wajumbe wake wakiwa ni wataalamu akiwemo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Awali, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema katika kipindi cha saa 24 jumla ya watu 292,142 duniani walibainika kuwa na virusi vya Corona kati yao watu 12,784 walifariki. Pia, katika Bara la Afrika watu 736 walibainika kuwa na virusi vya corona na kati yake watu 20 walifariki katika kipindi cha saa 24. Akizungumzia kwa upande wa Tanzania, Waziri Ummy alisema jumla ya watu 12 walibainika kuwa na Virusi vya Corona tangu mgonjwa wa kwanza alivyogundulika nchini na kwamba wagonjwa wote hali zao ni nzuri na mmoja amepimwa zaidi ya mara mbili na kubainika kuwa hana virusi.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameonya juu ya upotoshwaji na utoaji holela wa taarifa kuhusu ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababisha na Virusi vya Corona, COVID-19 unaofanywa na watu mbalimbali nchini Tanzania. Amesema kuanzia sasa taarifa hizo zitatolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na ikilazimika zitatolewa na Waziri Mkuu na ikilazimika sana zitatolewa na viongozi wakuu wa nchi ili kuepusha mikanganyiko. Waziri Mkuu ametoa onyo hilo Jumamosi, Machi 21, 2020 wakati akizungumza na Wakuu wa Mikoa yote nchini Tanzania: Makatibu Tawala wa Mikoa na Waganga Wakuu wa Mikoa kwa njia video kutokea ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma. Kufuatia hali hiyo, Waziri Mkuu ameiagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ifuatile watu wote wanaofanya upotoshaji kwa kupitia mitandao ya kijamii ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao. “Watu wote wanaopotosha umma na kuleta taharuki kuhusu ugonjwa wa corona badala ya kuelimisha namna ya kujikinga, wafuatiliwe na kuchukuliwa hatua,” amesisitiza.

Waziri Mkuu amesema licha ya hali ya maambukizi ya Corona nchini kutia matumaini, viongozi hao hawana budi kupeana taratibu za namna ya kukabiliana na tatizo hilo. “Wakuu wa mikoa kila mmoja ahakikishe eneo lake linakuwa salama na endapo kutakuwa na mgonjwa tumieni zahanati ambazo bado hazijaanza kutumika kwa ajili ya kutolea huduma kwa wagonjwa wa Corona,” amesema. Amewataka wakuu hao wa mikoa waimarishe utoaji wa elimu kwa umma na ikiwezekana watumie magari ya matangazo ili wananchi waelewe athari za ugonjwa huo na namna ya kujikinga pamoja na kuwaondolea hofu ili waweze kuendelea na shughuli zao za kimaendeleo. Pia amewataka watumie radio za kijamii katika maeneo yao kutoa elimu kwa umma juu ya kujikinga na ugonjwa huo na wasimamie maeneo ya utoaji huduma kama vituo vya mabasi na kuhakikisha kila abiria anakaa kwenye kiti. “Nendeni kwenye maeneo ya mikusanyiko, vituo vya mabasi kutoa elimu kwa umma na kuwaondoa hofu. Upande wa maofisini, viwandani na kwenye mgodi kuwe na utaratibu wa kutoa elimu kwa wafanyakazi kila siku asubuhi watumie hata robo saa kabla ya kuanza kazi waelekezwe namna ya kujikinga.”

Waziri Mkuu amesema kwa wanaoishi katika maeneo ya makambi, viongozi wao waelekezwe namna ya kutoa elimu ya kujikinga na corona na pia wadhibiti utorokaji na Serikali kwa upande wake inaendelea kuimarisha udhibiti mipakani, uwezo wa kupima sampuli na upatikanaji wa vifaa. Amewataka wakuu hao wa mikoa, wawashirikishe wakuu wa wilaya kwenye mikoa yao ili wasimamie utekelezaji wa maagizo hayo. Habari zaidi zinasema, Waziri Mkuu amewaagiza wakuu hao wa mikoa wahakikishe wanawafuatilia na kuwachukulia hatua wafanyabiashara wote watakaobainika kuongeza bei kwa bidhaa ambazo zinatumika katika udhibiti wa maambukizi ya ugonjwa wa Corona. Kuhusu viongozi wa dini, Waziri Mkuu amewaomba waendelee kushirikiana na Serikali katika kuwaelimisha waamini wao wote kuzingatia tahadhari za ugonjwa huu. Pia awaendelee kuliombea Taifa kwa kufunga na kusali!

23 March 2020, 15:35