Tafuta

Vatican News
Kila tarehe 8 Machi ni Siku ya wanawake duniani kwa lengo la kuhamasisha na kukuza maendeleo yao kisiasa, kijamii na kiuchumi.Katika harakati hizi bado kuna changamoto kubwa. Kila tarehe 8 Machi ni Siku ya wanawake duniani kwa lengo la kuhamasisha na kukuza maendeleo yao kisiasa, kijamii na kiuchumi.Katika harakati hizi bado kuna changamoto kubwa. 

Siku ya wanawake duniani:ni siku ya kutathimini maendeleo ya wanawake!

Kila tarehe 8 Machi ya kila mwaka ni siku ya wanwake duniani.Siku hii inataka kukumusha matokeo chanya ya kisiasa,kijamii, kiuchumi waliyofikia wanawake.Lakini licha ya jitihada na msimamo wao bado changamoto ni kubwa katika mantiki za usawa.Tuifahamu siku hii ilianza lini na sababu zake ni zipi kuwa na mshindo mkuu namna hii.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Kila tarehe 8 Machi ya kila mwaka ni Siku ya wanawake duniani, ambapo siku hii inataka kukumbuka na kutafakari juu ya matokeo ya kisiasa, kijamii, kiuchumi waliyofikia wanawake na msimamo wao imara katika ngazi ya kijamii kwa ujumla. Je  ni kwa nini  zaidi ya karne sasa watu duniani wamekuwa wakisherehekea siku hii? Siku ya wanawake duniani ilianza kutokana na jitihada za wanawake 15,000 mwaka 1908 walipoandamana mjini New York Marekani wakidai kupunguziwa muda wa kufanya kazi, ujira wa kuridhisha na haki ya kupiga kura. Kilikuwa ni chama cha kisoshalisti cha Amerika kilichotangaza kuwa ni siku ya kwanza ya kitaifa ya wanawake, mwaka mmoja baadaye. Wazo la kuwa siku ya kimataifa lilianzishwa na mwanamke kwa jina la Clara Zetkin. Yeye alipendekeza wazo hilo mwaka 1910 katika mkutano wa kimataifa wa wafanyakazi wanawake huko Copenhagen Denmark.

Wanawake 100 kutoka nchi 17

Kulikuwa na wanawake 100 hapo kutoka nchi 17 na wakakubaliana kwa pamoja. Kwa mara ya kwanza ilisheherekewa mwaka 1911, Austria, Denmark, Ujerumani na Switzerland. Sherehe ya miaka 100 ilifanyika kunako mwaka 2011. Suala hilo likawa rasmi mwaka 1975 baada ya Umoja wa Mataifa kuanza kusherehekea siku hiyo na baadaye kubuni kauli mbiu. Ya kwanza mwaka 1996 ilikuwa “furahia yaliyopita, panga kwa ajili ya baadaye”. Kwa hakika siku ya kimataifa ya wanawake duniani imekuwa siku ya kutathimini maendeleo ya wanawake katika jamii katika nyanja za siasa na uchumi, kulikuwa pia na migomo na maandamano yaliyoratibiwa kwa ajili ya kusisitiza masuala ya usawa.

Tarehe 8 mwezi Machi

Wazo la Clara Zetkin la Siku ya kimataifa ya wanawake duniani halikuwa na tarehe maalum na haikuwa rasmi mpaka kipindi cha vita ya mwaka 1917 wakati wanawake wa kirusi walipodai Amani na kufanyia kazi tatizo la upungufu wa chakula (Waliimba Amani na Mkate). Siku nne za mgomo, zilifanya watawala wa Urusi kuwapa wanawake haki ya kupiga kura. Tarehe ambayo mgomo ulianza ulikuwa kwenye kalenda ya Julian, ambayo ilikuwa ikitumika Urusi wakati huo, ilikuwa siku ya Jumapili tarehe 23 Mwezi Februari. Siku hii katika kalenda ya Gregoriana ilikuwa tarehe 8 mwezi Machi na ndiyo siku hii inayosherehekewa kila mwaka.

Chereko za Sherehe za siku hii,kupeana maua, maandamano ya kudai haki na usawa

Siku ya kimataifa ya wanawake ni siku ya mapumziko katika baadhi ya nchi nyingi ikiwemo Urusi, ambapo mauzo ya maua huwa mara mbili zaidi wakati wa siku tatu au nne kabla ya siku yenyewe, ambapo wanaume na wanawake huwapa maua wapendwa wao wa kike na wafanyakazi wenzao. Nchini China, wanawake wengi hufanya kazi nusu siku tarehe 8 Machi, kama ilivyoshauriwa na Baraza la nchi hiyo ingawa waajiri si mara zote wanatekeleza utamaduni huo. Nchini Italia, siku ya kimataifa ya wanawake au “La Fiesta della Donna” inasheherekewa kwa kupeana maua chanzo cha utamaduni huu hakifahamiki lakini inaaminika ilianzia Roma baada ya vita ya pili ya dunia. Nchini Marekani, Mwezi Machi ni mwezi wa historia kwa wanawake. Rais hutambua kila mwaka na kuthamini mafanikio ya wanawake wa Marekani. Lakini na zaidi sasa wanawake wengi kila mwaka  mamilioni ya waandamanaji kila nchi duniani kote ushuka barabarani huki wakipaza sauti kuhusu haki za wanawake.

Kumbuka kuwa Siku ya wanaume duniani ipo japokuwa bado haijatambuliwa na Umoja wa Mataifa

Hata hivyo tunakisikia siku ya wanawake kuvuma sana na wengi wa wanaume hawatambui  kuwa hata wao wana siku ya wanaume duniani. Siku hii inaadhimishwa kila tarehe 19 Novemba, lakini maadhimisho haya yameanza miaka ya hivi karibuni , kwani yalianza tangu miaka ya 90 na bado haijatambuliwa  rasimi na Umoja wa Mataifa. Watu huiadhimisha katika nchi zaidi ya 60. Lengo la siku hii ni kutazama afya za wanaume na wavulana, kuimarisha mahusiano ya jinsia, usawa wa jinsia na kutathimini jinsia ya kiume kama mfano watu wa kuigwa.

05 March 2020, 10:31