Tafuta

Bado ghasia dhidi ya wanawake na wasichana zimezidi na cha ajabu zinakubalika kwa maana hiyo elimu kwa wasichana haina maana iwapo jamii ina mtazamo hasi dhidi yao. Bado ghasia dhidi ya wanawake na wasichana zimezidi na cha ajabu zinakubalika kwa maana hiyo elimu kwa wasichana haina maana iwapo jamii ina mtazamo hasi dhidi yao. 

Mkutano wa 64 wa Kamisheni ya wanawake duniani,umeahirishwa sababu ya COVID-19

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto,UNICEF, la masuala ya wanawake,UN-Women na shirika la Plan International,kabla ya kuahirisha kikao kutokana na virusi vya Corona yalikuwa yameandaa Ripoti kwa kuonesha kuwa miongo 2 na nusu tangu baada ya mkutano wa wanawake mjini Beijing,China bado ghasia dhidi ya wanawake na wasichana zinaendelea na elimu kwa wasichana haina maana iwapo jamii ina mtazamo hasi dhidi yao.

Virusi vya Corona (COVID-19) vimeendelea kuathiri shughuli a kiuchumi, kijamii na kisiasa duniani na athari hasi za hivi karibuni zaidi ni kuahirishwa kwa mkutano wa 64 wa Kamisheni ya hali ya wanawake duniani, CSW uliokuwa ufanyike kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani kuanzia tarehe 9 hadi 20 Machi 2020. Kabla ya kuharishwa kilele cha fursa ya mkutano, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, lile la masuala ya wanawake, UN-Women na shirika la Plan International, limeandaa Ripoti yao kwa kuonesha kuwa miongo miwili na nusu tangu mkutano wa kihistoria wa wanawake mjini Beijing, China bado ghasia dhidi ya wanawake na wasichana zimeshamiri na cha ajabu zinakubalika na kwamba elimu kwa wasichana haina maana iwapo jamii ina mtazamo hasi dhidi yao.

Mafanikio ya kuandikishwa namba kubwa ya wasichana shuleni bado haionekani katika jamii

Katika Ripoti yao inaonesha kuwa ingawa idadi ya wasichana wanaoandikishwa shule na kumaliza masomo ni kubwa kuliko wakati wowote, mafanikio hayo hayajaweza kuunda jamii yenye usawa na yenye mazingira yasiyo na katili kwa wasichana. “Idadi ya wasichana watoro shuleni tangu mwaka 1995 imepungua kwa wasichana milioni 79, yaani wasichana wana fursa zaidi ya kuingia shule ya sekondari kuliko wavulana.” Ripoti inabainisha. Hata hivyo ukatili dhidi ya wanawake na wasichana umeshamiri. Aidha inasema “Mathalani mwaka 2016, asilimia 70 ya watu waliosafirishwa kiharamu duniani walikuwa ni wanawake na wasichana, wengi wao wakisafirishwa kwa ajili  ya kulazimishwa vitendo vya ngono. Cha kustaajabisha zaidi, msichana mmoja kati ya wasichana 20 wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 19, sawa na wasichana milioni 13 wamebakwa kwenye familia zao, moja ya ukatili mbaya zaidi wa kingono ambao wanawake na wasichana wanakabiliwa nao.”

Ahadi zilizotolewa kwa miaka 25 iliyopita bado kutimizwa na serikali

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF, Bi Henrietta Fore akizungumzia juu ya ripoti hiyo amesema kuwa,  “miaka 25 iliyopita, serikali duniani zilitoa ahadi kwa ajili ya wanawake na wasichana, lakini zimetekeleza ahadi kidogo tu. Wakati dunia ilizingatia utashi wa kisiasa wa kupeleka wasichana wengi zaidi shuleni, bado ni aibu kuwa imeshindwa kuwapatia stadi na msaada wanaohitaji ili kuunda siyo tu mustakabali wao bali pia kuishi maisha salama na yenye utu.” Bi. Fore ameongeza kusema kuwa “kupata elimu pekee haitoshi bali lazima kubadili tabia na mitazamo  ya watu kwa wasichana. “Usawa wa ukweli utakuwepo pindi wasichana watakuwa salama dhidi ya ukatili na waweze kufurahia haki zao na fursa sawa maishani,”.

Ripoti inataka  maeneo matatu yashughulikiwe

Ni kwa kuzingatia changamoto hizo wanazokabili wasichana hivi sasa, ripoti hiyo inataka hatua zaidi kwenye maeneo  matatu ambapo mosi, kufurahia na kupanua fursa za wasichana wa makabila, vipato na hadhi tofauti kwenye jamii ili wawe waleta mabadiliko na wabunifu wa suluhu za changamoto kwenye jamii zao. Halikadhalika kujumuisha sauti zao, maoni na mawazo kwenye mijadala, majukwaa kuhakikisha kuna michakato ambayo inazingatia jamii, elimu na mustakabali wao. Pili ni kuongeza uwekezaji kwenye sera na mipango na kuchagiza miundo ambamo kwayo maendeleo yanasongeshwa na wasichana barubaru kwa ajili yao wenyewe ikiwemo kusongesha stadi zao na kutokomeza ghasia kama vile ndoa za umri mdogo na ukeketeji. Eneo la tatu ni kuongeza uwekezaji kwenye utafutaji, uchambuzi na matumizi ya takwimu zilizonyambuliwa kutokana na tafiti kwenye maeneo ambayo hivi sasa hayana taarifa za kutosha. Maeneo hayo ni kama vile ukatili wa kijinsia, stadi zihitajikazo karne hii ya 21 na lishe na afya ya akili kwa barubaru.

Karne ya 21 iwe ya usawa wa wanawake

Karne ya 21 inatakiwa kuwa karne ya usawa wa wanawake, ndiyo  kauli iliyotolewa alhamis tarehe 4 Machi 2020 na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres alipokuwa akitoa wito wa kuibadilisha dunia katika kuhakikisha ushiriki sawa kwa wote. Akiwahutubia wanakitivo na wanafunzi katika Chuo Kikuu cha New School jijini New York Marekani, Katibu Mkuu Guterres amejitangaza mwenyewe kuwa ni mwanaharakati wa haki za wanawake anayejivunia na akatoa wito kwa wanaume kila mahali kuunga mkono haki za wanawake. “Kama ilivyo utumwa na ukoloni ulivyokuwa doa katika karne zilizopita, wote tunatakiwa kuona aibu kutokana na ukosefu wa usawa wa wanawake katika karne ya 21. Kwa sababu siyo tu haukubaliki, bali pia ni ujinga.” Amesisitiza Bwana Guterres.

Ukosefu wa usawa kijinsia na ubaguzi ni dhuluma

Kwa mujibu wa  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, anasema ukosefu wa usawa wa kijinsia na ubaguzi dhidi ya wanawake na wasichana vinasalia kuwa dhuluma kubwa ulimwenguni, “kutokuwepo kwa usawa na ubaguzi ni desturi ambazo bado ziko kila mahali. Maendeleo yamezorota kwa kiasi cha kukwama na katika mazingira mengine yamerudi nyuma. Kuna msukumo wa nguvu wa kurudisha nyuma haki za wanawake. Ukatili dhidi ya wanawake, ikiwemo mauaji dhidi ya wanawake yako katika viwango vya janga. Na zaidi ya mwanamke mmoja kati ya watatu atakumbana na ukatili wa namna fulani katika maisha yake.” Aidha Bwana Guterres ametoa ushauri kuwa hivi sasa ni wakati wa kuacha kujaribu kuwabadilisha wanawake na badala yake kuanza kuibadili mifumo ambayo inawazuia wanawake kuweza kuuufikia uwezo wao. Na kwa msingi huo karne ya 21 inapaswa kuwa karne ya usawa wa wanawake. Vilevile Bwana Guterres amesisitiza mwelekeo wa taasisi anayoiongoza akisema, “wakati Umoja wa Mataifa ukitimiza miaka 75, unachukua hatua kubwa kuunga mkono haki za wanawake.”

05 March 2020, 11:14