Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kusitisha vita, chuki na uhamasa, ili kuunganisha nguvu kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu kutokana na janga la Virusi vya Corona, COVID-19. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kusitisha vita, chuki na uhamasa, ili kuunganisha nguvu kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu kutokana na janga la Virusi vya Corona, COVID-19. 

Umoja wa Mataifa watoa wito wa kusitisha vita ili kuokoa maisha!

Wito wa kusitisha vita sehemu mbali mbali za dunia ni muhimu sana, ili kushikamana na kuunganisha nguvu kwenye mapambano dhidi ya Virusi vya Corona ili kuokoa maisha ya watu wengi. Tabia ya chuki, uhasama na hali ya kutoamianiana; ni mambo yanayopaswa kuwekwa kando, ili kutoa fursa ya misaada kupelekwa kwa waathirika pamoja na kuanza “kuwasha cheche za matumaini”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres, tarehe 23 Machi 2020 aliitaka Jumuiya ya Kimataifa kuunganisha rasilimali na nguvu yake kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Huu ni ugonjwa ambao haujali ukabila, utaifa, kikundi au imani ya mtu! Ni Virusi vinavyoshambulia bila huruma hata kidogo! Lakini, jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, bado mtutu wa bunduki unaendelea kutawala sehemu mbali mbali za dunia na waathirika wakubwa ni watu wasiojiweza, wanawake, watoto, wazee na walemavu. Hawa pia ndio waathirika wakubwa wa Virusi vya Corona, COVID-19. Nchi ambazo kwa sasa zimo vitani, zinakabiliwa pia na changamoto kubwa ya uhaba wa kada katika afya na kwamba, miundo mbinu imekuwa ni dhaifu sana kiasi cha kutoweza kuhimili kishindo cha maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19.

Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia, liko hatarini kukumbwa na maambukizi ya Virusi vya Corona. Kumbe, wito wa kusitisha vita na mapambano ya silaha sehemu mbali mbali za dunia ni muhimu sana, ili kushikamana na kuunganisha nguvu kwenye mapambano dhidi ya Virusi vya Corona ili kuokoa maisha ya watu wengi. Tabia ya chuki, uhasama na hali ya kutoamianiana; ni mambo yanayopaswa kuwekwa kando, kwa kusitisha mashambulizi ya makombora na yale ya anga, ili kutoa fursa ya misaada kupelekwa kwa waathirika pamoja na kuanza “kuwasha cheche za matumaini”.

Mazingira ya vita, uhasama na chuki yanapaswa kumalizika na hivyo kuiwezesha Jumuiya ya Kimataifa kupambana kufa na kupona na ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Familia kubwa ya binadamu inahitaji umoja, upendo na mshikamano kwa wakati huu, kuliko kuendekeza vita isiyokuwa na mashiko wala mvuto, ustawi na maendeleo ya wengi! Wachunguzi wa mambo ya kidiplomasia wanasema kwamba, wito wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres, umeanza kufanyiwa kazi na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kwamba, Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wanataka kulivalia njuga wazo hili na kuanza utekelezaji wake! Kimsingi vita ni mama wa majanga yote duniani!

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres katika salam na matashi mema kwa mwaka 2019 aliitaka pia Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda na kudumisha: haki msingi za binadamu, utu na heshima yake; daima kwa kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya kuboresha maisha ya watu wengi zaidi duniani. Mwaka 2018 umekuwa ni mwaka ambao umegubikwa kwa kiasi kikubwa na athari za mabadiliko ya tabianchi sehemu mbali mbali za dunia, kiasi cha watu kukata tamaa ya maisha. Alisema, bado mtutu wa bunduki unaendelea kurindima, kuna kinzani na migawanyiko ya watu kutokana na sababu mbali mbali hali ambayo pia imesababisha wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani; watu wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anasikitika kusema kwamba, kila kukicha kuna ongezeko kubwa la matabaka ya watu duniani, kiasi kwamba, idadi ya maskini, yaani “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” inazidi kuongezeka, wakati ambapo utajiri na rasilimali dunia, zinaendelea kumilikiwa na watu wachache duniani.

Licha ya patashika nguo kuchanika sehemu mbali mbali za dunia, lakini Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema, kuna alama za matumaini kwa baadhi ya nchi duniani yaani: Mkataba wa kusitisha vita uliotiwa sahihi huko Yemen; mkataba wa amani kati ya Eritrea na Ethiopia na kwamba, Serikali ya Sudan ya Kusini itaheshimu mkataba wa amani uliowekwa kati yake na wapinzani, ili amani na utulivu viweze kurejea tena Sudan ya Kusini ambako watu wanaendelea kuteseka kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe, magonja na baa la njaa. Dhuluma na nyanyaso za watu wa kabila la Rohingya huko nchini Myanmar ni kati ya changamoto pevu kwa Jumuiya ya Kimataifa ili kuhakikisha kwamba, utu, heshima na haki msingi za wananchi hawa zinalindwa na kudumishwa. Mlipuko wa ugonjwa wa Ebola huko DRC, umekwisha waathiri watu zaidi 560 na kati yao, 288 wamekwisha kufariki dunia.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa ameridhishwa na makubaliano yaliyofikiwa juu ya “Global Compact 2018” yaani “Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji 2018” unaopania pamoja na mambo mengine: kukomesha ubaguzi na maamuzi mbele; kuongeza fursa za ushirikishwaji wa wahamiaji katika maisha ya nchi wahisani; kupunguza gharama za kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji ambazo kwa sasa umekuwa ni mzigo mkubwa, kiasi cha kutishia umoja na mshikamano wa kimataifa katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia!

Umoja wa Mataifa

 

 

30 March 2020, 14:08