Tafuta

Kutokuwa na Sera ya Walemavu kunasababisga  hata miundombinu ya  baadhi ya taasisi kutokuzingatia mahitaji  ya walemavu. Na kumbe walemavu wakiwezeshwa wanaweza kabisa zaidi hata ta watu wa kawaida Kutokuwa na Sera ya Walemavu kunasababisga hata miundombinu ya baadhi ya taasisi kutokuzingatia mahitaji ya walemavu. Na kumbe walemavu wakiwezeshwa wanaweza kabisa zaidi hata ta watu wa kawaida 

Tanzania:Fanyeni sera za walemavu wakiwezeshwa wanauwezo mkubwa!

Ulemavu si dhambi wala laana! Si kundi linalotakiwa kutengwa na jamii,badala yake"tunatakiwa kuwawezesha kwa kuangalia mahitaji yao ya msingi ikiwemo elimu na miundombinu rafiki ya kupata elimu hii".Ni kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Ujumuishaji wa Watu wenye Ulemavu katika Masuala ya Maendeleo cha CCBRT, Dar es Salaam Tanzania,Bw.Frederick Msigala akihimiza taasisi husuka kuwa na sera ya walemavu.

Na Dalphina Rubyema & Sr.Angela Rwezaula - Vatican

Katika kujenga  jamii  yenye usawa na kujali makundi  yote, taasisi na mashirika mbalimbali  nchini  Tanzaniania yakiwemo ya kidini, yameshauriwa  kutunga Sera  yenye kuwalinda  na kuwatetea watu wenye ulemavu. Maoni hayo yametolewa na Mkuu wa  Kitengo cha Ujumuishaji wa Watu wenye Ulemavu katika Masuala ya Maendeleo  cha CCBRT, Bw. Frederick Msigala,  wakati akizungumza na vyombo vya habari vinavyomilikiwa na Kuendeshwa na Kanisa Katoliki nchini Tanzania.

Katika mazungumzo  hayo hivi karibuni yaliyofanyika katika ofisi za Baraza la Maaskofu Katoliki, Dar es Salaam, Tanzania (TEC) Bw. Msigala amesema licha ya asilimia 9.3 ya Watanzania kutajwa kuwa ni watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali, bado jamii haijatoa umuhimu unaotakiwa wa kundi hili, jambo linalorudisha nyuma juhudi za serikali na wadau wengine wa maendeleo. Hata hivyo ameyataja baadhi ya mambo yanayokwamisha juhudi hizi kuwa ni pamoja na baadhi ya taasisi na mashirika mbalimbali  nchini kutokuwa na Sera ya Walemavu jambo  ambalo amesema linawanyima stahiki zao.

Bwana Msigala amesema: “Ni kutokuwa na Sera ya Walemavu ndiko kunakosababisha hata miundombinu ya  baadhi ya taasisi kutokuzingatia mahitaji  ya walemavu. Unakuta taasisi  ina kumbi nzuri za mikutano lakini ujenzi wake ni wa ghorofa na hakuna lifti kwa ajili ya watu wenye ulemevu… vivyo hivyo mazingira unakuta yana barabara zenye ngazi, lakini hakuna ngazi mbetuko maalum kwa kundi hili. Hata sehemu za kujisitiri si rafiki kwa walemavu,”.

Hata hivyo amesisitiza kuwa, Sera hiyo ilinde makundi yote ya walemavu wakiwemo wale  wa viongo, kutokuona, ngozi,  viziwi na wale wenye upoozi wa ubongo. Bw. Msigala ambaye pia ni mlemavu wa viungo amesema, kutojali kundi  la walemavu ndiko kunasababisha  kundi hili kuendelea kunyanyapaliwa huku baadhi ya watu wakiwachukulia kama  watu wanaohitaji hisani  jambo ambalo siyo sahihi na siyo kweli. “Ulemavu si dhambi wala laana! Si kundi linalotakiwa kutengwa na jamii, badala yake tunatakiwa kuwawezesha kwa kuangalia mahitaji yao ya msingi ikiwemo elimu na miundombinu rafiki ya kupata elimu hii”.

Aidha amefafanua zaidi kuwa: “Tunauwezo wa kupambanua mambo kama ilivyo kwa binadamu wengine wasiyo walemavu, tatizo ni kwamba hatupewi kipaumbele…hatupelekwi shule badala yake tunafichwa majumbani, na hili linachangia sana idadi ya watu wenye ulemavu wasiyojua kusoma na kuandika kuwa kubwa ikilinganishwa na wale watu wa kawaida” .

Katika kufafanua juu ya takwimu anesema kwamba, asilimia 45 ya Watu wenye ulemavu nchini Tanzania, hawajui kusoma na kuandika na katika watoto 10 wenye ulemavu, wanne kati yao hawaendi shule na chini ya asilimia tano ndiyo walioajiriwa katika sekta rasmi, kwa maana hiyo :“Tusichukuliwe kama watu wakupewa hisani… sisi ni binadamu kamili. Tuna akili na uwezo wa kupembua mambo hata darasani tunafanya  vizuri…mfano ni kwangu mimi ambaye wazazi wangu hawakuniona mzigo tangu awali, walinisomesha”.

Akitoa ushuhuda binafsi Bwana Msigala amethibitisha:“Sekondari nilisoma Tosamaganga  Iringa, Digrii yangu ya kwanza nilisoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Masters nimesoma Uingereza… ninauwezo ndiyo maana hata CCBRT wameniajiri na ajira yangu siyo ya upendeleo ni stahiki yangu, hivyo tusiwadharau watu wenye ulemavu bali tuwawezeshe kulingana na mahitaji  yao,” amesisitiza. Amesema kuwawezesha huku  kusiwe kule kwa  kuwajengea nyumba au kuwatengea makazi maalum, badala yake wapewe elimu, wawezeshwe  kupata taarifa kila kundi kulingana na mahitaji yake ikiwa ni pamoja na kuwekewa wataalam wa alama, maandishi kuwa katika mfumo wa nukta nundu  na mahitaji mengineyo.

Katika maoni yake pia amesema:“Kutujengea nyumba au kututafutia makazi maalum ni zaidi ya kututenga sisi watu wenye ulemavu … ni sawa na kutuambia tujitenge na jamii tuishi peke yetu …inasahau  kwamba tunayo haki ya kuishi na ndugu,jamaa na familia zetu kwa ujumla…hili nalo liangaliwe kwa  mapana linatuumiza,” amesisitiza Bw.Msigala. Kwa kufanya  hayo yote amesema yataondolewa endapo serikali, wadau na jamii kwa ujumla watatengeneza mazingira rafiki ya kuwawezesha watu hawa wenye ulemavu.

19 February 2020, 16:30