Tafuta

Ripoti mpya ya mashirika ya who,Unicef na Lancet wasema kuwa  watoto nchini Norway,Korea Kusini na Uholanzi wana nafasi bora zaidi ya kuishi  watoto wa Jamhuri ya Afrika ya Kati,CAR, Chad,Somalia,Niger na Mali Ripoti mpya ya mashirika ya who,Unicef na Lancet wasema kuwa watoto nchini Norway,Korea Kusini na Uholanzi wana nafasi bora zaidi ya kuishi watoto wa Jamhuri ya Afrika ya Kati,CAR, Chad,Somalia,Niger na Mali  

Tabianchi,matangazo ya biashara vinatishia afya ya watoto duniani!

Kwa mujibu wa ripoti mpya iliyochapishwa kwa ushirikiano kati mashirika ya Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto la Afya na jarida la Lancet kuwa afya na mustakabali wa kila mtoto na kijana duniani kwa sasa anakabiliwa na tishio la uharibifu wa mazingira,mabadiliko ya tabianchi, mbinu mbovu na za ushawishi za masoko ambazo zinachochea zaidi kwa watoto ulaji wa vyakula vilivyosindikwa,vinywaji vyenye sukari,vilevi na tumbaku

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Vitisho vitokanavyo na  mabadiliko ya tabianchi na biashara vinavyozidi kuongezeka kwa kasi sana  na  nchi kushindwa kuchukua hatua kuweka mazingira bora kwa afya ya mtoto ndiyo yaliyomo kwenye  ripoti mpya iliyochapishwa kwa ushirikiano kati mashirika ya Umoja wa Mataifa  la kuhudumia watoto, UNICEF na  la afya, WHO na jarida la Lancet. Ripoti  iliyopewa kauli mbiu “Mustakabali wa watoto? Ni kwamba afya na mustakabali wa kila mtoto na kijana duniani kwa sasa anakabiliwa na tishio la uharibifu wa mazingira,mabadiliko ya tabianchi, mbinu mbovu na za ushawishi za masoko ambazo zinachochea zaidi kwa watoto ulaji wa vyakula vilivyosindikwa,vinywaji vyenye sukari,vilevi na tumbaku. Ripoti  iliyoandaliwa na wataalamu zaidi ya 40 wa masuala ya afya ya watoto na vijana wadogo kutoka maeneo mbalimbali duniani na kutolewa New York, Marekani, London,  Uingereza na Geneva, Uswisi inasema “Hakuna hata nchi moja iliyo na mikakati toshelezi ya kulinda afya ya watoto, mazingira yao na mustakabali wao.

Mwenyekiti mwenzake  wa kamisheni hiyo, Bi Helen Clark amesema licha ya mafanikio katika afya ya mtoto na vijana katika miaka 20 iliyopita, maendeleo yamekwama na kuna mwelekeo wa kurudi nyuma. Amesema kwamba  inakadiriwa “watoto milioni 250 wenye umri wa chini ya miaka mitano ambao wanaishi katika nchi za vipato vya chini na kati wako hatarini kutofikia ustawi wao kutokana na kudumaa na umaskini. Lakini hofu kubwa zaidi ni kwamba kila mtoto duniani hivi sasa anakabiliwa na vitisho vya sasa vya mabadiliko ya tabianchi na mashinikizo ya biashara.” Kwa mantiki hiyo amesema nchi lazima zibadilishe kabisa mifumo yao kwa afya za watoto na na vijana wadogo ili kuhakikisha kuwa si kwamba dunia inalea watoto wao hivi sasa  bali pia inatunza dunia ambayo watairithi siku za mbele. Ripoti hiyo imetumia vipimo vipya kutoka nchi 180 duniani ambapo mataifa hayo yanalinganishwa utendaji wao katika ustawi wa mtoto ikiwemo afya, elimu  na lishe, maendeleo yao kwa kumulika utoaji wa gesi chafuzi, uwiano na pengo la kipato. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wakati nchi maskini zinapaswa kuchukua hatua zaidi kusaidi watoto wao kuishi maisha yenye afya, kiwango cha juu cha hewa ya ukaa kutoka mataifa tajiri kinatishia mustakabali wa watoto wote.

Aidha Ripoti  hiyo imesema ripoti: “Iwapo kwa mujibu wa makadirio ya sasa kiwango cha joto kitazidi nyuzi joto 4 katika kipimo cha selsiyasi ifikapo mwaka 2100, hii itasababisha madhara mabaya zaidi ya afya kwa watoto, kutokanana kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari, mawimbi joto, magonjwa kama vile malaria, denge na utapiamlo,”   Kipimo hicho kimeonesha kuwa watoto nchini  Norway, Korea Kusini na Uholanzi wana nafasi bora zaidi ya kuishi na kustawi kuliko watoto wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, Chad, Somalia, Niger na Mali ambao wanakabiliwa na machungu ya kupindukia katika makuzi yao. Akiangazia suala la matangazo ya biashara, Profesa Anthony Costello, ambaye ni mmoja wa waandishi wa ripoti hiyo amesema hoja ya viwanda kujidhibiti vyenyewe imeshindwa kwa sababu tafiti zinaonesha kuwa viwanda vimeshindwa kuzuia matangazo yasiyofaa kwa watoto. “Mfano, licha ya viwanda nchini Australia kutia saini kanuni za kujidhibiti, watoto na barubaru bado wanaona matangazo milioni 51 ya pombe kwa kipindi cha mwaka mmoja tu wakati wa matangazo ya mpira wa miguu, kriketi na raga na hali inaweza kuwa mbaya zaid,” amesema Profesa Costello.

Wataalam wanatoa mapendekezo matano ambayo yanaweza kufuatwa katika kukabiliana na tishio hilo kwamba:  mosi kuacha utoaji wa hewa chafuzi, pili watoto na vijana wadogo kuwa kitovu cha kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, tatu, sera mpya na uwekezaji katika sekta zote ili kulinda afya na haki za mtoto, nne, kujumuisha sauti za watoto kwenye maamuzi ya kisera na tano kusimamia kwa kina kanuni dhidi ya matangazo ya kibiashara kupitia itifaki mpya ya ziada ya mkataba wa kimataifa wa haki za mtoto.

19 February 2020, 16:08