Tafuta

Vatican News
Mahakama ya kikatiba imefutilia mbali uchaguzi wa rais wa Malawi Bwana Peter Mutharika uliofanyika mwezi Mei 2019. Mahakama ya kikatiba imefutilia mbali uchaguzi wa rais wa Malawi Bwana Peter Mutharika uliofanyika mwezi Mei 2019.   (AFP or licensors)

Malawi:Mahakama yafutilia mbali uchaguzi wa rais wa Malawi!

Kwa mujibu wa mahakama ya kikatiba nchini Malawi yenye majaji watatu imefutilia uchaguzi wa rais wa Malawi Bwana Peter Mutharika uliokuwa umefanyika Mei 2019

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Mahakama ya kikatiba imefutilia mbali uchaguzi wa rais wa Malawi Bwana Peter Mutharika uliofanyika mwezi Mei 2019. Kwa mujibu wa mahakama yenye majaji watatu imesema ya kuwa wamegundua kwamba kulikuwa na makosa mengi katika uchaguzi huo hali ya kwamba maadili ya matokeo hayo yaliingiliwa.

Mahakama ilitangaza kwamba matokeo ya uchaguzi huo yalikuwa na makosa na kwamba hayakustahili na wakati huohuo ikakubaliana na walalamishi kwamba uchaguzi huo ulikuwa na udanganyifu mkubwa. Katika uchaguzi huo wa mwezi Mei mwaka 2019 , Mutharika alitangazwa kuwa mshindi akiwa na asilimia 38 ya kura zote zilizopigwa, Lazarus Chakwera alikuwa wa pili na asilimia 35 naye aliyekuwa wakati mmoja makamu wa rais Saulos Chilima akiwa wa tatu na asilimia 20 ya kura zilizopigwa.

Chakwera na Chilima waliwasilisha kesi dhidi ya uchaguzi wa Mutharika na kuongoza maandamano ya kutaka maafisa wa tume ya uchaguzi nchini humo kujiuzulu. Hata hivyo Runinga ya taifa haikurusha matangazo ya moja kwa moja ya mambo yaliokuwa yakiendelea katika mahakama hiyo. Uchaguzi mpya utafanyika katika kipindi cha siku 150, mahakama hiyo ilisema katika uamuzi wake, ikisisitiza mwishowe kwamba inatumai uamuzi huo hautaliharibu taifa hilo.

Katika kesi yao Chakwera na Chilima walipinga matokeo ya uchaguzi huo wakisema makosa yaliofanyika yaliathiri zaidi ya kura milioni 1.4 kati ya kura milioni 5.1 zilizopigwa. Hata hivyo uamuzi huo wa siku ya Jumatatu tarehe 3 Februari 2020 unaweza kupingwa katika mahakama ya kilele. Kulingana na  Gazeti la The New York Times mawakili waliokuwa wakimwakilisha rais walikataa kujibu maswali na kuondoka kwa haraka katika eneo la mahakama hiyo. Mwanasheria mkuu , aliyekuwa akiwakilisha tume ya uchaguzi alisema kwamba watalazimika kutafuta ushauri kuhusu hatua watakazochukua.

Majaji hao wa mahakama ya kikatiba walisema kwamba matokeo hayo yalionyesha kwamba hakuna aliyechaguliwa kwa wingi wa kura kulingana na katiba ya taifa hilo, ikiangazia ufafanuzi wa wingi wa kura na anayeongoza kwa kura. Mahakama hiyo ililiagiza bunge kufanya kikao baada ya kipindi cha siku 21 ili kutoa sheria mpya itakayoongoza uchaguzi mpya.

04 February 2020, 13:33