Tafuta

Vatican News
Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Jumbu kumbu ya Miaka 25 tangu kufanyike Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Wanawake huko Beijing, China mwaka 1995. Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Jumbu kumbu ya Miaka 25 tangu kufanyike Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Wanawake huko Beijing, China mwaka 1995.  (REUTERS)

Jubilei ya Miaka 25 ya Mkutano wa Wanawake Beijing, China! Haki na Usawa!

Haki msingi za wanawake ni kwa ajili ya watu wote mahali popote pale walipo. Wadau mbali mbali wanapaswa kuhakikisha kwamba, wanalinda na kudumisha haki msingi za wanawake. Mafanikio yaliyofikiwa katika kipindi cha Miaka 25 iliyopita yanapaswa kuendelezwa na kuboreshwa zaidi sanjari na kuimarisha umoja na mshikamano katika kutetea haki msingi za wanawake! Beiing Miaka 25.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Gertrude Ibengwe Mongella, mwanasiasa mkongwe kutoka Tanzania, kati ya mwaka 1993-1995 alikuwa ni Katibu Mkuu wa Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Wanawake na kuhudhuria mkutano wake wa nne uliofanyika Beijing, China mwaka 1995. Huu ni mkutano ulioleta mabadiliko makubwa miongoni mwa wanawake, ili kusimama kidete, kudai na kutetea haki zao msingi. Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 25 tangu Mkutano Mkuu wa Wanawake ulipofanyika mjini Beijing huko nchini China. Bi. Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Alhamisi, tarehe 27 Februari 2020 katika hotuba yake elekezi kama sehemu ya maadhimisho ya Miaka 25 tangu kufanyike Mkutano wa Beijing, amesema kwamba ingawa mazingira yamebadilika sana tangu wakati huo, lakini kumekuwepo pia na wimbi kubwa linaloshambulia haki msingi za wanawake katika medani mbali mbali za maisha.

Bi Bachelet anakaza kusema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti zaidi katika kukuza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu mambo ambayo kamwe hayawezi kuwa ni kwa ajili ya fursa ya watu wachache ndani ya jamii. Haki msingi za wanawake zilizovaliwa njuga miaka 25 iliyopita zinaendelea kudorora; usawa wa kijinsia bado unayo safari ndefu kutokana na ubaguzi na mfumo dume unaoendelea kutawala sehemu mbali mbali za dunia. Kumbe, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti kwa dhati kwa kuonesha utashi wa kisiasa ili kukabiliana kikamilifu na changamoto mamboleo katika maisha na utume wa wanawake katika medani mbali mbali za maisha. Haki msingi za wanawake ni kwa ajili ya watu wote mahali popote pale walipo. Wadau mbali mbali wanapaswa kuhakikisha kwamba, wanalinda na kudumisha haki msingi za wanawake. Mafanikio yaliyofikiwa katika kipindi cha Miaka 25 iliyopita yanapaswa kuendelezwa na kuboreshwa zaidi sanjari na kuimarisha umoja na mshikamano katika kutetea haki msingi za wanawake, ili kujenga na kuimarisha Jamii zinazosimikwa katika: haki, usawa, ustawi na maendeleo ya wengi.

Wanawake Beijing 25 Yrs
29 February 2020, 15:45