Ni matumaini makubwa ya Mkutano wa kimataifa uliofanyika jijini Berlin nchini Ujerumani kuleta muwafaka wa amani nchini Libya, licha ya vikwazo ambavyo bado vipo Ni matumaini makubwa ya Mkutano wa kimataifa uliofanyika jijini Berlin nchini Ujerumani kuleta muwafaka wa amani nchini Libya, licha ya vikwazo ambavyo bado vipo 

Libya:matarajio ya amani baada ya mkutano wa Berlin!

Mkutano wa kimataifa kwa ajili ya Libya uliofanyika mjini Berlin Ujerumani tarehe 19 Januari 2020 unaonesha hatua ya kwanza kuelekea amani ya nchi,japokuwa bado inakosa sahihi ya mwisho ya waziri Mkuu wa Libya Sarraj na Jenali Haftar.Viongozi wa kimataifa wametia sahihi kwa ajili ya kuzuiwa kwa silaha na hivyo Umoja wa Mataifa una zoezi la kuthibiti kuwaka moto.Papa Francisko baada ya sala ya Malaika ametoa wito ili wapate suluhisho.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres tarehe 19 Januari 2020 ameuambia mkutano wa kimataifa kwa ajili ya Libya uliofanyika mjini Berlin Ujerumani kwamba hali halisi inayoendelea nchini Libya haitokubaliwa kuendelea na kwamba suluhisho la kipekee ni kwa njia ya amani na majadiliano na si mtutu wa bunduki.  Guterres amesema, lengo lao la kuwa hapo ni kwa ajili ya  dharura na sababu ambayo ni ya msingi, kuizuia Libya kutumbukia katika janga kubwa zaidi.  Mkutano huo ambao umewaleta pamoja wakuu mbalimbali wa nchi na serikali, mwenyekiti wa tume ya Muungano wa Afrika, Katibu Mkuu wa jumuiya ya nchi za Kiarabu, marais wa Jumuiya ya Muungano wa Ulaya na tume ya Muungano wa Ulaya na wadau muhimu wa Libya ni wa kusaidia juhudi za kukomesha vita nchini Libya. Na Katibu Mkuu amewashukuru kwa kuunga mkono dhamira ya kutafuta suluhisho la mgogoro huo kwa njia ya amani.

Mapigano mjini Tripoli na viunga vyake yamekatili maisha na kujeruhi maelfu ya watu wakiwemo raia

Akiendelea na hotuba yake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema mwaka mmoja uliopita Walibya kwa msaada wa Jumuiya ya kimataifa walikuwa wakichukua hatua za matumaini ili kuisongesha nchi hiyo mbele katika suluhu ya kisiasa, “lakini matumaini hayo yalitoweka mwezi Aprili mwaka jana. Na tangu hapo mapigano mjini Tripoli na viunga vyake yamekatili maisha na kujeruhi maelfu ya watu wakiwemo raia. Sheria za kimataifa za kibinadamu zimekuwa zikikiukwa tena na tena. Zaidi ya watu 170,000 wamelazimika kuzikimbia nyumba zao, shule zaidi ya 220 mjini Tripoli zimefungwa na hivyo kuwanyika hali yao ya msingi ya kupata elimu watoto 116,00.” Kana kwamba hiyo haitoshi Katibu Mkuu amesema wahamiaji na wakimbizi wamekwama vizuizini karibu na mapigano na pia wameathirika na kuendelea kukabiliwa na madhila ya hali mbaya kwenye vituo wanakoshikiliwa. Kwa kusisitiza amesema, “hali hii mbaya haiwezi kuruhusiwa kuendelea. Libya imeingizwa katika vita vibaya sana kukiwa na ongezeko la ushiriki wa watu kutoka nje. Tunakabiliwa na hatari ya machafuko ya kikanda.

Wakati ni sasa wa hatua za haraka na za pamoja ili kuzuia vita kamili ya wenyewe kwa wenyewe nchini Libya.

Na ninaamini kwamba hakuna suluhisho lolote la kijeshi kwa vita vya Libya. Wakati ni sasa wa hatua za haraka na za pamoja kuzuia vita kamili ya wenyewe kwa wenyewe nchini Libya.” Katibu Mkuu ameonya kwamba “mgogoro huo unaweza kusababisha janga kubwa la kibinadamu na kuiacha nchi hiyo katika mgawanyiko wa daima. Kwa nchi jirani zake Kusini mwa Mediterrania na hususan ukanda wa Sahel athari zitakuwa mbaya sana, ugaidi zaidi, usafirishaji haramu wa binadamu zaidi, ongezeko la usafirishaji haramu wa dawa za kulevya, silaha na binadamu. ” Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameuambia mkutano wa Berlin akionya kwamba kwamba, “Tunashindwa katika vita dhidi ya ugaidi barani Afrika , hebu angalia Sahel na bonde la ziwa Chad, ninaamini kwamba hatotoweza kufanikiwa bila kuwepo kwa amani na utulivu Libya. Leo hii tumekuja pamoja ili kutimiza wajibu wetu wa kuhakikisha kwamba suluhu ya amani inapatikana kwa mgogoro wa Libya ambayo watu wa Libya na dunia kwa ujumla inaitaka kwa udi na uvumba.”

Ukiukwaji wa vikwazo vya silaha uliowekwa na Baraza la Usalama dhidi ya taifa hilo lazima ukomeshwe

Kufuatia na hayo yote amerudia  kutoa wito kwa wote wanaohusika moja kwa moja au kwa njia moja au nyingine katika mzozo wa Libya kufanya kila wawezalo ili kusaidia usitishaji wa uhasama na kukomesha mtutu wa bunduki. Pia amesema ukiukwaji wa vikwazo vya silaha uliowekwa na Baraza la Usalama dhidi ya taifa hilo lazima ukome. Katibu Mkuu amekaribisha usitishaji mapigano wa hivi karibuni na kuahidi kufanya kazi na pande zote ili kuendeleza hatua hizo na kuimarisha makubaliano ya usitishaji mapigano.Amezitaka pande zote nchini Libya kushiriki kwa nia njema mazungumzo ya kisiasa, kiuchumi na masuala ya kijeshi katika mchakato unaoongozwa na kumiliwa na Walibya wenyewe. Amewaahidi kwamba Umoja wa Mataifa umejizatiti na unaendelea kuunga mkono mchakato huo wa kusaka amani ya kudumu.

Walikuwapo katika mkutano huo ili kuweka mazingira ya kimataifa yatakayowezesha Walibya kuwa pamoja katika kutafuta suluhisho  la vita vinavyowakabili

Akiendelea na hotuba hiyo Bwana Guterres ameukumbusha mkutano huo kwamba, “wako hapo siku hiyo ili  kuweka mazingira ya kimataifa yatakayowezesha Walibya kuwa pamoja il kutafuta suluhu ya vita vinavyowakabili kwa pamoja.” Amesema azimio la Berlin linasisitiza misingi ambayo ni muhimu katikakulinda amani na usalama wa kimataifa , kamauhuru na kutoingiliwa na pia kuheshimu sheria za kimataifa ikiwemo maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Pia linajumuisha mbinu za kufuatilia na kuhakikisha mchakato unaendelea, “tunapaswa kuondokana na maneno na kuingiakatikahatua. Umuhimu wetu kama jumuiya ya kimataifa umejaribiwa. Kwa upande wangu naahidi kwamba Umoja wa Mataifa utaunga mkono juhudi zote za kubadili maneno kuwa hatua madhubuti zinazodhihirika mashinani.” Pia amesisitiza kwamba, “umoja wa Mataifa utasimamana watu wa Libya wakiwa katikamchakato huu wa kutatua tofauti zao kupitia majadiliano na maridhiano kwa nia njema na kuhakikisha njia inafunguliwa na kuwa na mustakabali wa amani zaidi. Na kwa hilo ninatarajia uungwaji mkono wenu.”

Papa Francisko baada ya Sala ya Malaika wa Bwana ametoa wito

Mara baada ya tafakari ya neno la Mungu katika Jumapili ya Pili ya Mwaka A, tarehe 19 Januari 2020 kwa waamini na mahujaji wote waliokusanyika katika kiwanja cha Mtakatifu Petro, Vatican, Papa Francisko amekumbusha kuwa: “ jijini Berlin wanafanya mjadala kwa mara nyingine tena kuhusiana na kipeo cha Libya”. Kwa maana hiyo ni matumani hai kwamba mkutano huo muhimu, unaweza kuanzisha mchakato mwema katika kuelekea kusitisha vurugu za mapigano nchini Libya na kupata suluhisho la mchakato wa amani ambayo inatamaniwa kuwa na msimamo wa nchi hiyo.

20 January 2020, 12:00