Papa Francisko aliwambia wamama kwamba watoto wakilia wawanyonyeshe! Papa Francisko aliwambia wamama kwamba watoto wakilia wawanyonyeshe! 

Kusikiliza kilio cha mtoto ni sanaa katika malezi

Utafiti juu ya zana za mawasiliano ya watoto uliofanywa na R.G.Hopkins na J.K.Green pamoja na mwanasaikolojia John Bowlby unaonyesha kuwa mzazi anapaswa kusikiliza kilio cha mtoto wake ili kubaini mahitaji ya mtoto huyo.Kusikiliza kilio cha watoto siyo tu wajibu kwa wazazi bali pia ni sanaa ambayo wanapaswa kuwa nayo katika malezi ya watoto wao.

Na Padre  Richard Kashinje - Vatican

Ufahamu wa kusikiliza kilio cha watoto ni sanaa katika malezi na hali hii siyo tu wajibu wa mzazi/mlezi bali pia ni sanaa ambayo mzazi/mlezi kwa anapaswa kuwa nayo daima katika maisha yote. Haya yameelezwa na Profesa R.G. Barr, B. Hopkins, J.A. Green, na mwanasaikolojia John Bowlby kutoka Chuo kikuu cha Cambridge. Kwa mana hiyo utafiti juu ya zana za mawasiliano ya watoto unabainishwa kuwa mzazi anapaswa kusikiliza kilio cha mtoto wake ili kubaini mahitaji ya mtoto huyo. Wakizungumzia malezi ya watoto, wasomi hao wanashauri kuwa wazazi wanapaswa kuwa makini zaidi ili kuweza kufahamu namna ambavyo watoto wanaweza kufikisha ujumbe kwa wazazi/walezi wao kwa njia mbalimbali. Jambo la muhimu ambalo mzazi/mlezi anapaswa kulizingatia ni kusikiliza kilio. Hii inaweza kueleweka kama namna ya mawasiliano ambayo mtoto hujieleza mwenyewe.  Wasomi hawa wanasema kuwa kilio huonyesha jambo linalomkera mtoto ama pengine huonyesha kuwa kuna jambo hajapendezwa nalo.

Kulia inakuwa pia ni lugha, ishara ambayo inaonyesha mchakato wa kujishikamanisha

Kulia inakuwa pia ni lugha, ishara ambayo inaonyesha mchakato wa kujishikamanisha ndani ya familia, kama vilevile anavyoonyesha mwanasaikolojia John Bowlby katika kitabu chake cha Attachment and Loss (Basic Books, 1980). Kwa mujibu wa wasomi hawa, kilio cha mtoto, sanjari na kuonekana kama kielelezo cha maumivu, lakini pia ni dhihirisho lisiloelezeka na lisilodhibitiwa ambalo mtoto anafikisha ujumbe kwa mzazi ama mlezi wake. Kilio pia kina kazi nyingine muhimu: kujifariji. Wanaeleza kuwa kifungu cha machozi juu ya uso wa mtoto kinaweza kutoa aina ya ujumbe, msukumo, na inaonekana kuna uwezekano kuwa kinaweza kuwa kichocheo cha kutosha kwa utengenezaji wa homoni za kukabiliana na mfadhaiko.

Kilio lazima kitambuliwe na kufasiriwa

Mtoto anapoendelea kulia sana na kwa muda mrefu, mzazi wakati mwingine anaweza kujaribu kumtuliza kwa vurugu, wakati mwingine kwa nia nzuri, kumtikisa mtoto kwa bidii katika jaribio la kumtuliza au wakati mwingine - kama ilivyoelezewa katika fasihi ya kisayansi - kuchukuliwa na wasiwasi au hasira kumdhuru, na kusababisha kitu ambacho hakijulikani sana lakini cha kutisha "dalili ya mfadhaiko". Ni ushauri wa kitaalamu kwamba kulia lazima kutambuliwe na lazima kufasiriwe na kuokolewa. Hii inatumika pia katika mazingira ya matibabu ambapo maumivu ya mtoto bado hayajapatiwa uangalizi wa kutosha na kuthibitiwa ipasavyo. Maumivu ya mtoto lazima yapewe uangalifu mkubwa kutoka kwa wahusika wote na ikiwa nguvu kazi haitoshi, lazima itafutwe na ipatikane kwa sababu, mateso ya mwanzo ya mtoto huashiria mahangaiko yasiyokoma maishani mwake.

Kilio kisichosahaulika

Kuna kilio kingine ambacho hakiwezi kusahaulika: kile cha mtoto anayenyanyaswa na kudhurumiwa/kubakwa. Ni kilio kilichofichika, kwa sababu vurugu, njaa, kutengwa mara nyingi hutokea ndani ya familia husika, au katika maeneo yaliyojificha,  mbali na magazeti ya utangamano mkubwa, ambako njaa na maumivu vimetanda. Ni kilio kisicho haki, ambacho kina ladha chachu, kwa sababu ni kilio cha dhuluma. Ni kilio kinachotatanisha sana, kwa sababu wakati anakata tamaa ya kupata msaada, hata kulia hukoma kuwa na maana: machozi huisha na kutoa nafasi ya hofu kwa mtoto anayedhulumiwa na mwenye njaa.

Kilio cha mtoto mdogo kisipuuzwe

Kilio cha mtoto mdogo ni jambo kubwa sana lisilopaswa kupuuzwa hata kidogo. Mzazi/mlezi, acha kulia kwa mtoto kukufikie na usiogope aibu inayosababisha ugumu wa lugha isiyo ya maneno, na udhaifu unaodhihirika. Kilio cha wale ambao ni dhaifu huonyesha pia udhaifu wetu: kwa wengi ni fursa ya ukuaji, kutopuuzwa, hata ikiwa kwa wengine ni ugunduzi wa aibu.

Kilio cha mtoto katika mazingira mapya

Kuhusiana na kilio cha watoto, hata Papa Francisko kama kiongozi wa Kanisa kwenye sherehe za Ubatizo wa Bwana Jumapili tarehe 12 Januari 2020, aliongoza ibada ya ya  Misa Takatifu na kutoa ubatizo kwa watoto 32 katika Kikanisa cha Sistina mjini Vatican.  Jambo muhimu alilogusia kwa kutazama tabia za watoto alisema kutokana na nafasi waliyo kuwamo, hakutaka kuendelea zadi na mahubiri, bali  kuwataadharisha, kwamba, watoto hawajazoea kwenda Sistina. Ni  kwa mara yao ya kwanza! Hawajuhi kukaa mahali palipo fungwa na kidogo penye joto. Hawajazoea kuvalishwa jinsi walivyo na nguo za sikukuu nzuri kama hiyo. Kwa maana  halisi watoto hao watakosa utulivu ndani humo wakati wa misa.

Kilio cha watoto ni kwaya nzuri

Kwa kuendelea Papa  alisema katika hali hiyo akianza mmoja kulia, ni kwaya itaanza kwa wote! Lakini akianza mmoja na kufuatia mwingine, wao wasiogope sauti ya kulia kwa watoto. Na badala yake, mtoto akilia na kulalamika, labda ana joto, apunguzwe nguo mojawapo; au akiwa na njaa, basi anyonyeshwe hapo, kwani kuna amani daima”. Hili ni jambo ambalo Papa Francisko amekumbusha, alikuwa amesema hata mwaka jana na kwamba, watoto wanayo sifa kuu ya kutengeneza kwaya. Inatosha kuanza mmoja note ya ‘la’ na wote wakafuatia na kufanya kikundi cha kwaya moja. Kwa maana hiyo: “Msiogope”. Hayo ni mahubiri mazuri ya mtoto anapolia kanisani. Lakini fanyeni kwa namna ya kwamba mtoto anahisi na kujisikia vema ili kuendelea mbele na ibada”. https://www.vaticannews.va/sw/pope/news/2020-01/ubatizo-wa-bwana-msisahau-kupelekeni-roho-mtakatifu-ndani.html

KILIO CHA MTOTO
20 January 2020, 16:00