Taarifa ya UNICEF kwenye Mkutano wa COP25 inasema, waathirika wakubwa kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi ni watoto. Taarifa ya UNICEF kwenye Mkutano wa COP25 inasema, waathirika wakubwa kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi ni watoto. 

Taarifa ya UNICEF kwenye Mkutano wa COP25 kuhusu Mazingira!

UNICEF, katika taarifa yake kwenye Mkutano wa COP25 kuhusu mazingira inasema kwamba, waathirika wakuu ni watoto wanaoishi katika maeneo yanayoweza kukumbwa na mafuriko, ukame wa kutisha pamoja na mazingira machafu. Haya ni mambo ambayo kimsingi yanachangia kwa kiasi kikubwa magonjwa ya milipuko pamoja na vifo kwa watoto. WHO afya ipewe msukumo wa pekee.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Kuanzia tarehe 2-13 Desemba 2019, Umoja wa Mataifa unafanya Mkutano wa 25, COP25 chini ya uongozi wa Mrs. Carolina Schmidt, Waziri wa Mazingira kutoka Chile ambaye pia ndiye Rais wa Mkutano wa 25, COP25 kuhusu mazingira unaoendelea mjini Madrid, nchini Hispania. Mkutano huu unawajumuisha wataalam wa mazingira kutoka katika nchi 196 na unahudhuriwa na wajumbe 29, 000. Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii kuwatumia ujumbe washiriki wa mkutano huu unaopania pamoja na mambo mengine, kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inatekeleza Makubaliano ya Mkutano wa 21 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, Cop21 uliopitishwa mjini Paris kunako tarehe 12 Desemba 2015. Utekelezaji huu ni mwaliko kwa wadau wote kujizatiti ili kuhakikisha kwamba, malengo yaliyowekwa yanafikiwa ili kukabiliana na changamoto kubwa ya athari za mabadiliko ya tabianchi. Jumuiya ya Kimataifa inatambua fika athari za mabadiliko ya tabianchi kama kikwazo kikubwa kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, katika taarifa yake kwenye Mkutano wa 25 kuhusu mazingira inasema kwamba, waathirika wakuu ni watoto wanaoishi katika maeneo yanayoweza kukumbwa na mafuriko, ukame wa kutisha pamoja na mazingira machafu. Haya ni mambo ambayo kimsingi yanachangia kwa kiasi kikubwa magonjwa ya milipuko pamoja na vifo kwa watoto. Shirika la Afya Duniani, WHO linasema, mabadiliko ya tabianchi yana athari kubwa katika afya na makuzi ya watoto. Kumbe, teknolojia rafiki kwa mazingira pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa. Upandaji wa miti mijini unaendelea kuhimizwa ili kupambana na uchafuzi wa hali ya hewa unaopelekea watoto wengi kukumbwa na magonjwa.

Kiwango kikubwa cha hewa ya ukaa ni hatari sana kwa maisha, ustawi na maendeleo ya watu. Kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, watoto wengi wamejikuta wakiwa wanahifadhiwa kwenye kambi za watu wasiokuwa na makazi maalum na matokeo yake ni watoto kama hawa kuambukizwa magonjwa. Kumbe, kuna haja ya Jumuiya ya Kimataifa kuwa na mpango mkakati utakaodhibiti idadi ya watu wanaohudumiwa kwenye kambi za watu wasiokuwa na makazi maalum. Athari za mabadiliko ya tabianchi ni chanzo pia kwa sehemu kubwa ya watoto kuacha kuendelea na masomo na matokeo yake ni kutumbukizwa kwenye ndoa za watoto wadogo na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo. UNICEF inasema watoto waelimishwe kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote!

UNICEF
10 December 2019, 14:54