Tafuta

Jukwaa la Wakimbizi Duniani UNHCR GLOBAL REFUGEE FORUM limefunguliwa tarehe 16-18 Desemba 2019: Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani! Jukwaa la Wakimbizi Duniani UNHCR GLOBAL REFUGEE FORUM limefunguliwa tarehe 16-18 Desemba 2019: Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani! 

UNHCR: Jukwaa la Wakimbizi Duniani: 16-18 Desemba 2019

Lengo la jukwaa hili ni kutafsiri kwa vitendo Mkataba wa “Global Compact 2018” unaojikita hasa katika mchakato wa uwajibikaji pamoja na kushirikishana uchangiaji wa gharama kwa ajili ya kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za duniani. UNHCR inasema, katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, idadi ya wakimbizi na wahamiaji duniani imeongezeka maradufu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres, anasema wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani linagusa na kutikisa misingi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu. Chanzo kikuu cha wakimbizi na wahamiaji ni vita, kinzani, nyanyaso, dhuluma pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi. Kumekuwepo pia na ongezeko kubwa la idadi ya watu duniani sanjari na kukua na kupanuka kwa miji na majiji. Changamoto zote hizi zinachangia ongezeko la wimbi kubwa la wakimbizi  na wahamiaji duniani. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, kuna watu zaidi ya milioni 70 wasiokuwa na makazi maalum, kati yao kuna wakimbizi milioni 25 waliotawanyika sehemu mbali mbali za dunia na hawana tena fursa ya kuweza kurejea katika nchi zao asilia. Kuanzia tarehe 16-18 Desemba 2019, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (United Nations High Commission for Refugees, UNHCR), huko Geneva, Uswiss, linaendesha Jukwaa la Wakimbizi Duniani (GRF) linalowashirikisha wadau mbali mbali ili kutoa maoni yatakayoisaidia Jumuiya ya Kimataifa kupambana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani kwa sasa na kwa siku za usoni.

Lengo la jukwaa hili ni kutafsiri kwa vitendo Mkataba wa “Global Compact 2018” unaojikita hasa katika mchakato wa uwajibikaji pamoja na kushirikishana uchangiaji wa gharama kwa ajili ya kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za duniani. Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, Filippo Grandi katika hotuba yake elekezi amesema, katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, idadi ya wakimbizi na wahamiaji duniani imeongezeka maradufu. Huu ni wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kuibua mbinu mkakati utakaosaidia kuwahudumia wakimbizi pamoja na kuzijengea uwezo nchi zile zinazotoa hifadhi kwa wakimbizi na wahamiaji kama sehemu ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030, bila kumwacha mtu awaye yote nyumba ya utekelezaji wa Malengo haya. Mkutano umesikiliza jinsi ambavyo nchi, mashirika ya kitaifa na kimataifa, makampuni na watu binafsi pamoja na wakimbizi na wahamiaji wenyewe wanavyoweza kuchangia katika utekelezaji wa dhana ya uwajibikaji kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji duniani.

Mchango unaohitajika kwa sasa ni : rasilimali fedha, msaada wa kiufundi, kisheria, sera na mikakati itakayosaidia utekelezaji wa mchakato wa ujenzi wa jamii shirikishi zaidi; ujenzi wa makazi ya wakimbizi na wahamiaji na pale ambapo amani na utulivu vimerejea, wakimbizi na wahamiaji wawe na fursa ya kuweza kurejea tena katika nchi zao asilia, ili kushiriki katika ujenzi wa nchi zao. Kwa kuwasaidia na kuwajengea uwezo wakimbizi na wahamiaji wataweza pia kushiriki katika mchakato mzima wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Katika mkutano huu, mambo makuu sita yamepewa kipaumbele cha kwanza: mchakato wa kuratibu uchangiaji wa gharama za huduma kwa wakimbizi na wahamiaji, elimu, fursa za ajira, maboresho ya hali ya maisha, nishati, miundombinu, suluhu, ulinzi na usalama.

Kimsingi “Global Compact 2018” yaani “Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji 2018” unapania pamoja na mambo mengine kukomesha ubaguzi na maamuzi mbele; kuongeza fursa za ushirikishwaji wa wahamiaji katika maisha ya nchi wahisani; kupunguza gharama za kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji ambazo kwa sasa umekuwa ni mzigo mkubwa sehemu mbali mbali za dunia. Lengo la jukwaa hili ni kupambana pia na biashara ya binadamu na viungo vyake; sababu zinazopelekea watu kuthubutu kuhatarisha maisha yao kwa kufunga safari zisizo na uhakika pamoja na kutafuta suluhu ya vita na migogoro mbali mbali duniani. Ushirikiano na mshikamano wa kimataifa ni jibu makini katika kukabiliana na changamoto za wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji. Kuna haja pia kushirikishana nyajibu na majukumu.

Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, Filippo Grandi anasema kuna haja kwa wananchi wa Sudan ya Kusini kuhakikisha kwamba, pande zote zinazohusika na mgogoro wa kisiasa ambao umepelekea vita ya wenyewe kwa wenyewe katika kipindi cha miaka sita, wanaanza mara moja kujielekeza katika utekelezaji wa muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa kama suluhu ya amani ya kudumu na uhakika wa usalama wa misaada inayopelekwa kwa waathirika wa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan ya Kusini. Takwimu zinaonesha kwamba, Sudan ya Kusini ina idadi kubwa ya wakimbizi na wahamiaji Barani Afrika, hali ambayo pia inachangiwa na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Jukwaa la Wakimbizi

 

 

18 December 2019, 11:49