Vatican News
Mafuriko nchini Sudan Kusini yamesababisha baa la njaa.Inasadikika milioni 5.5 ya watu ni waathirika wa njaa kwa mwaka 2020 Mafuriko nchini Sudan Kusini yamesababisha baa la njaa.Inasadikika milioni 5.5 ya watu ni waathirika wa njaa kwa mwaka 2020  (AFP or licensors)

Sudan Kusini:Milioni 5.5 ni waathirika wa njaa kwa 2020!

Dharura nchini Sudan Kusini kutokana na ukame,mafuriko na kipeo cha kisiasa.Inasadikika kuwa milioni 5.5 ni waathirika wa njaa kwa 2020,kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la WFP.Na Shirika la chakula na kilimo (FAO) limesema suluhisho la asili ya mabadiliko ya tabia nchi ni muhimu na lazima zichagizwe katika mifumo ya chakula.Udhibiti endelevu wa maliasili na kulinda bayoanuai ni ili lazima kufikia mifumo endelevu ya chakula.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa WFP limesema linakimbizana na muda ili kukusanya fedha zinazo hitajika kuwalisha mamilioni ya watu nchini Sudan Kusini wakati huu wa njaa inayozidi kushika kasi na watu wanahitaji haraka msaada wa kibinadamu. Hata hivyo Shirika hilo limelaumu ukame, sintofahamu ya mustakbali wa kisiasa na mafuriko makubwa yaliyotokea katika miezi ya karibuni na kwamba vyote hivyo vimelipelekea taifa  na watu wake katika hali mbaya wakati mwaka unakaribia ukongoni mwake.

Takribani watu milioni 5.5 wanakabiliana na njaa

Kwa mujibu wa taarifa zaidi la Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) linasema kuwa takriban watu milioni 5.5 wanatarajiwa kukabiliwa na njaa mapema mwaka 2020 huku idadi ya watu watakaohitaji msaada wa kibinadamu inatarajiwa kuongezeka  kwa sababu ya uharibifu mkubwa uliosababishwa na mafuriko tangu mwezi Oktoba  mwaka huu baada ya ukame ambao uliathiri sehemu kubwa ya nchi na kuharibu mazao. Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa (WFP) Bwana  David Beasley amesema:  “Kwa majanga yote tunayo yashuhudia duniani kitu cha mwisho tunachokihitaji ni kutotokea kwa janga jingine, tunayajua matatizo ambayo tumekuwa nayo  nchini Sudan Kusini, lakini mvua na mafuriko vimesababisha janga la kitaifa kubwa na baya kuliko kila mtu alivyotarajia. Na endapo tusipopata fedha za ufadhili katika wiki au miezi michache ijayo tutakuwa tunazungumzia baa la njaa, na hivyo tunahitaji msaada na tunauhitaji sasa.”

Mafuriko yameathiri watu milioni moja

Takribani watu milioni moja wameathiriwa moja kwa moja na mafuriko ambayo yamesambaratisha tani 73,000 za uwezekano wa mavuno na kuangamiza maelfu ya ng’ombe na mbuzi ambao wanategemewa na watu wengi kwa ajili ya kuishi. Msaada wa kibinadamu unaokoa maisha katika maeneo mengi Sudan Kusini. Mwaka 2019 WFP ilijitahidi kuwafikia watu milioni 4.6 na msaada wa kuokoa maisha lakini sasa inahitaji dola milioni 270 kwa ajili ya nusu ya kwanza ya mwaka 2020 na kwa mwezi Januari mwaka kesho (WFP) inahitaji dola milioni 100 kwa ajili ya kununua chakula kabla ya msimu wa mvua kuanza Mei 2020. Mwezi Oktoba mwaka huu serikali ya Sudan Kusini ilikwisha tangaza hali ya dharura katika majimbo ya Bahr El Ghazal, Greater Upper Nile na Greater Equatoria kwa sababu ya mafuriko na kuomba kuongezwa kwa msaada wa kimataifa. Mwaka 2017 baa la njaa nchini Sudan Kusini iliweza kukabiliwa vyema baada ya miezi minne kwa njia ya kutoa jibu la msaada wa kibinadamu. Na wataalam wanakubaliana wakisema kuwa matatizo ya usalama wa vyakula haijawahi kuwa hasi kwa maana hiyo ni matarajio ya kupata msaada huo ili kuthibiti haja ya baa hili la njaa.

FAO yataka suluhisho la asili za mabadiliko ya tabianchi katika mifumo ya chakula

Na  Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limesema suluhisho la asili ya mabadiliko ya tabia nchi ni muhimu sana na lazima zichagizwe katika mifumo ya chakula. Amezungumza hayo Mkurugenzi Mkuu wa FAO Bwana Qu Dongyu kandoni mwa mkutano wa 25 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabia nchi COP25 mjini Madrid Hispania tarehe 12 Desemba 2019. Mkutano huo ulikuwa unazungumzia kuhusu jukumu kubwa la kilimo katika kutoa suluhisho la asili za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi walilopatia jina la tukio maalum la “kuchagiza hatua za suluhiso la asili kwa pamoja 2020”.

Ubunifu na teknolojia ni kitovu cha maendeleo endelevu

Bwana Qu Dongyu amesema ubunifu ikiwemo kujumuisha teknolojia kwa sasa ni kitovu cha maendeleo endelevu ya sekta ya kilimo. Na amezitaja suluhisho  hizo kuwa zinajumuisha hatua katika masuala ya misitu na mifumo mingine kama udongo, maji, mifugo, bahari na mifumo ya chakula pamoja na mazingira ya chakula na watumiaji. Mkuu huyo wa FAO aidha amesema “tunajiandaa kubadili mfumo wa chakula, na lazima tuufanyie mbadadiliko kama  mnyororo wa uzalishaji chakula, thamani na wa usambazaji, lakini suluhisho pekee ni ubunifu”. Bwana Qu Dongyu amesisitizia pia ushirikiano na wadau wote katika kufanikisha hilo. Katika taarifa yake pia amesisitiza udhibiti endelevu wa maliasili na kulinda bayoanuai kwa ajili ya kufikia mifumo endelevu ya chakula ambayo itasaidia sana kuboresha kilimo na uzalishaji wa chakula. Ametoa mfano wa mradi uliotangazwa tarehe 12 Desemba 2019 kati ya FAO, Ujerumani na shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP wa kuzisaidia nchi zinazoendelea kushughulikia mabadiliko ya tabianchi katika sekta zao za kilimo.

FAO kuendelea na ushirikiano wa karibu na wadau wote

Amesisitiza kwamba FAO itaendelea kushirikiana na kwa karibu na wadau wote katika mfumo wa Umoja wa Mataifa, nchi, asasi za kiraia, sekta binafsi, na mashirika yote muhimu ili kuongeza ufanisi wa suluhisho zilizopo na kuhakikisha kwamba suluhisho la asili zibakia kuwa kitovu kwa hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kulinda bayoanuai.

13 December 2019, 14:54