Tafuta

Vatican News
Rais Sergio Mattarella wa Italia kwa niaba ya familia ya Mungu nchini Italia amemtumia Baba Mtakatifu Francisko salam za matashi mema kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya Daraja na Miaka 83 ya kuzaliwa. Rais Sergio Mattarella wa Italia kwa niaba ya familia ya Mungu nchini Italia amemtumia Baba Mtakatifu Francisko salam za matashi mema kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya Daraja na Miaka 83 ya kuzaliwa.  (AFP or licensors)

Papa Francisko: Jubilei Miaka 50 ya Daraja na Miaka 83 ya kuzaliwa!

Rais Sergio Mattarella kwa niaba ya familia ya Mungu nchini Italia, amemtumia Baba Mtakatifu salam na matashi mema, akiunganisha tukio hili na Jubilei ya Miaka 50 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre, kielelezo cha huduma kwa Mungu na watu wake; mambo yanayomwilishwa katika utekelezaji wake wa shughuli mbali mbali za kichungaji kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni ameadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre hapo tarehe 13 Desemba 1969. Baba Mtakatifu alizaliwa tarehe 17 Desemba 1936 huko Flores, Buenos Aires, nchini Argentina. Mwaka 2019 ametimiza miaka 83 tangu alipozaliwa. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 13 Desemba 1969 akapewa Daraja Takatifu  ya Upadre. Kunako mwaka 1992 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu na hatimaye, kuwekwa wakfu kuwa Askofu hapo tarehe 27 Juni 1992. Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Kardinali tarehe 21 Februari 2001.Tarehe 13 Machi 2013 akaanza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Vipaumbele katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro ni: Maskini, Mazingira na Amani Duniani; fadhila zinazopata chimbuko lake kutoka kwa Mtakatifu Francisko wa Assisi.

Katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 83 tangu Baba Mtakatifu Francisko alipozaliwa, amepokea salam na matashi mema kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kwa namna ya pekee, Rais Sergio Mattarella wa Italia kwa niaba ya familia ya Mungu nchini Italia, amemtumia Baba Mtakatifu salam na matashi mema, akiunganisha tukio hili na Jubilei ya Miaka 50 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre, kielelezo makini cha huduma kwa Mungu na watu wake; mambo yanayomwilishwa katika utekelezaji wake wa shughuli mbali mbali za kichungaji kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Rais Mattarella anampongeza Baba Mtakatifu kwa kuendelea kuwahamasisha watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia kuvunjilia mbali: vita, kinzani na mifumo mbali mbali ya kibaguzi, ili kuanza mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kujenga madaraja yanayowakutanisha watu, ili kudumisha udugu wa kibinadamu pamoja na kuimarisha haki na amani duniani.

Rais Mattarella anasema, utamaduni wa watu kukutana unawasaidia kuweza kufahamiana vyema zaidi na hatimaye, kuanza mchakato wa kuheshimiana na kuthaminiana, changamoto inayopaswa kutekelezwa kila kukicha, kwa kuwa na malengo ya muda mrefu na mfupi katika utekelezaji wake, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wote wa Mungu. Hija za kichungaji zinazotekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko nchini Italia, ni ushuhuda wa uwepo wa karibu wa Baba Mtakatifu kwa watu wa Mungu nchini Italia; hali inayoonesha pia uhusiano mzuri wa kidiplomasia kati ya Serikali ya Italia na Vatican, kama unavyofafanuliwa katika Mkataba wa Lateran. Mwishoni mwa salam na matashi mema kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya Daraja Takatifu pamoja na Miaka 83 tangu alipozaliwa, Rais Mattarella wa Italia anasema, wakati huu, waamini na watu wenye mapenzi mema wanapoendelea kujiandaa kwa ajili ya maadhimisho ya Sherehe ya Noeli kwa Mwaka 2019, bado kuna watu wanaoteseka kutokana na maafa na majanga mbali mbali. Kumbe, Kipindi cha Noeli, kiamshe tena matumaini, udugu wa kibinadamu na mshikamano wa dhati kati ya watu wa Mataifa.

Itakumbukwa kwamba, tarehe 11 Februari, 2019 imetimia miaka 90 tangu Kanisa Katoliki lilipotiliana saini Mkataba na Serikali ya Italia “Patti Lateranensi.” Mkataba wa Lateran uliifanya Vatican kutambuliwa rasmi kama nchi huru yenye uwezo wa kujiamria mambo yake yenyewe katika medani za kimataifa bila kuingiliwa na Serikali ya Italia. Papa Pio XI alilitaka Kanisa kuendelea kushiriki kikamilifu katika ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu nchini Italia: kiroho na kimwili; kwa kutumia amana na utajiri wake wa kihistoria, kitamaduni na kisanaa; mambo yanayofumbatwa katika tunu msingi za maisha ya Kikristo. Kwa upande wake, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuihakikishia Italia uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala, ili kweli nchi ya Italia,  iendelee kuwa aminifu kwa Mapokeo pamoja kupyaisha udugu wa mshikamano ambao umeipambanua Italia kwa miaka mingi.

Papa: Miaka 83
18 December 2019, 10:58