Tafuta

Vatican News
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amepongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuunga mkono jitihada za Jumuiya ya Kimataifa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amepongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuunga mkono jitihada za Jumuiya ya Kimataifa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.  (Vatican Media)

Hotuba ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Papa Francisko Desemba 2019

Katiba ya Umoja wa Mataifa inakazia: Utu, heshima, haki msingi za binadamu na ustawi wa wengi. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita zaidi katika utunzaji wa mazingira nyumba ya wote kwa sasa pengine hata kuliko wakati mwingine wowote ule katika historia ya mwanadamu kutokana na athari zake zinazoendelea kuwatumbukiza watu wengi katika majanga na hatimaye, umaskini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres, Ijumaa tarehe 20 Desemba 2019 amekutana kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican ili kumshukuru kwa jitihada zake kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; mapambano dhidi ya umaskini duniani unaodhalilisha utu na heshima ya binadamu pamoja na mchango wake kuhusu umuhimu wa kulinda na kudumisha haki, amani, ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu. Katibu mkuu amemshukuru Baba Mtakatifu kwa mapokezi makubwa aliyompatia wakati alipowasili mjini Vatica na kwamba, kwa hakika amekuwa ni chombo na mjenzi wa matumaini kwa watu waliokata tamaa; mtetezi wa maskini na wanyonge duniani, ili kulinda na kudumisha utu, heshima na haki zao msingi. Katibu mkuu anamshukuru Baba Mtakatifu kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele kuihamasisha Jumuiya ya Kimataifa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano katika kukabiliana na changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kwa: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji katika maisha ya jamii inayowapokea.

Waraka wake wa kitume “Laudato si”  yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” ni rejea muhimu katika mchakato wa ekolojia fungamani inayopania: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mambo yote haya ni sehemu muhimu sana zinazobainishwa kwenye Katiba ya Umoja wa Mataifa yaani: Utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita zaidi katika utunzaji wa mazingira nyumba ya wote kwa sasa pengine hata kuliko wakati mwingine wowote ule katika historia ya mwanadamu kutokana na athari zake zinazoendelea kuwatumbukiza watu wengi katika majanga na hatimaye, umaskini. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres anasema,  Mkutano wa 25 Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi COP25 uliokuwa ukifanyika mjini Madrid nchini Hispania umehitimishwa bila mafanikio yoyote. Kumbe, uwepo wake mjini Roma ni kutaka kuihimiza Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti zaidi ili kuhakikisha kwamba, inapunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa ifikapo mwaka 2050.

Nchi mbali mbali duniani, hazina budi kusikiliza na kujibu kwa umakini mkubwa ushauri wa wanasayansi ili kulinda na kutunza mazingira. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa amempongeza Baba Mtakatifu kwa kuendelea kuunga mkono jitihada mbali mbali zinazofanywa na Umoja wa Mataifa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya binadamu. Amemshukuru kwa kutembelea Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa huko New York, Marekani, kunako mwaka 2015. Kwa hakika, Baba Mtakatifu ameendelea kuihamasisha Jumuiya ya Kimataifa katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu Ifikapo mwaka 2030 kwa kusimama kidete kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi; kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana na kujadiliana katika ukweli na uwazi ili kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Huu ndio mchakato wa ujenzi wa utandawazi unaopaswa kusimikwa katika misingi ya haki, amani, umoja na mshikamano kati ya watu wa Mataifa.

Hiki ni kipindi cha shamrashamra za maadhimisho ya Sherehe ya Noeli. Huu ni muda muafaka wa kuombea amani duniani. Inasikitisha kuona kwamba, kuna baadhi ya Jumuiya za Kikristo hazitaweza kuadhimisha Sherehe ya Noeli kutokana na sababu za ulinzi na usalama. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anasikitika kusema kwamba, kumekuwepo na ongezeko kubwa la uvunjwaji wa haki ya uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini; hali inayojikita katika: vita, chuki na uhasama; misimamo mikali ya kidini na kiimani; pamoja na vitendo vya kigaidi vinavyotishia misingi ya haki, amani, umoja na mafungamano ya kijamii. Kuna waamini wanauwawa wakati wakiwa kwenye nyumba za Ibada, Makanisa na Misikiti inachomwa moto bila kusahau kufuru na unajisi unaotendwa kwenye nyumba  na maeneo ya Ibada. Kumbe, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusimama kidete ili kuhakikisha kwamba,  uhuru wa kuabudu unalindwa na kutekelezwa na wote.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema, Hati ya Udugu wa Kibinadamu kwa Ajili ya Amani na Utulivu iliyotiwa mkwaju kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari  2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu ni kielelezo makini cha jinsi ya kuwekeza katika ujenzi wa mafungamano ya kijamii, kwa kuheshimiana na kuthaminiana hata katika tofauti msingi zinazojitokeza kati ya watu. Huu ni mwaliko na changamoto kwa waamini wa dini mbali mbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu wa kibinadamu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho. Elimu makini inapaswa kusaidia mchakato wa ujenzi wa mafungamano ya kijamii, kwa kuondokana na misimamo mikali ya kidini na kiimani pamoja na mahubiri ya chuki dhidi ya waamini wa dini nyingine.

Katika kipindi hiki cha patashika nguo kuchanika kutokana na vita, kinzani na msimamo mikali ya kidini na kiimani, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kushikamana ili kulinda na kudumisha amani na utulivu kati ya watu wa Mataifa. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, amemwambia Baba Mtakatifu Francisko kwamba, mambo haya yanajionesha dhahiri katika maisha na utume wake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Amemshukuru kwa namna ya pekee Baba Mtakatifu na kumtakia heri na fanaka katika maadhimisho ya Sherehe ya Noeli, ili kweli Noeli, iweze kuwa ni chemchemi ya amani na baraka kwa mwaka mpya wa 2020.

Umoja wa Magtaifa
21 December 2019, 15:33