Tarehe 25 Novemba ni siku ya Kimataifa ya kutokomeza aina zote za ukatili dhidi ya wanawake na wasichana Tarehe 25 Novemba ni siku ya Kimataifa ya kutokomeza aina zote za ukatili dhidi ya wanawake na wasichana 

Kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana ni wajibu wetu!

Wakati dunia ikiadhimisha siku ya Umoja wa Mataifa ya kutokomeza ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana ifikapo kila mwaka tarehe 25 Novemba Katibu Mkuu wake Bwana Antonio Guterres amesema ukatili huu ni miongoni mwa ukatili mbaya zaidi duniani,unaoendelea na ukiukwaji mkubwa kabisa wa haki za binadamu uliosambaa,na ambao ukiathiri mtu mmoja miongoni mwa kila wanawake watatu duniani.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Siku ya kimataifa ya kutokomeza ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana huadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 25 Novemba, siku ambayo pia huanza siku 16 za harakati za uchagizaji na uelimishaji kuhusu ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana. Kwa maana hiyo wakati dunia ikiadhimisha siku hii Umoja wa Mataifa umesema umedhamiria kukomesha mifumo yote ya ukatili kwa kundi hilo kwani ni wajibu na haki kufanya hivyo. Kupitia ujumbe wake maalum wa siku hii, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres amesema ukatili huu ni miongoni mwa ukatili mbaya zaidi duniani, unaoendelea na ukiukwaji mkubwa kabisa wa haki za binadamu uliosambaa, ukiathiri mtu mmoja miongoni mwa kila wanawake watatu duniani. Aidha hii inamaanisha kwamba mtu mmoja karibu nawe, jamaa wa familia, mfanyakazi mwenzako, rafiki yako au hata wewe mwenyewe unakugusa!

Ukatili wa kingono dhidi ya wanawake na wasichana umeanza karne nyingi

Katibu Mkuu Bwana Guterres amesisitiza kuwa ukatili wa kingono dhidi ya wanawake na wasichana haujaanza leo hii bali  chimbuko lake ni karne za mfumo dume, kwa maana hiyo :“hebu tusisahau kwamba pengo la usawa wa kijinsia ambalo limechochea utamaduni wa ubakaji ni suala la kutokuwepo na uwiano wa mamlaka. Unyanyapaa, dhana potofu, kutoripotiwa vya kutosha na utekelezwaji duni wa sheria kunachochea ukwepaji wa sheria na ubakaji bado unatumika kama silaha mbaya ya vita.” Hivyo amesema yote haya sasa ni lazima yabadilike na kutoa wito kwa serikali zote, sekta binafsi, asasi za kiraia na watu kila mahali kuchukua msimamo thabiti dhidi ya dhuluma za kijinsia na ujinga. Amemsihi kila mmoj kuonyesha mshikamano mkubwa na waathirika, watetezi na wapigania haki za wanawake na kwamba“Lazima tuchagize haki za wanawake na fursa sawa. Pamoja, tunaweza na lazima tumalize ubakaji na unyanyasaji wa kijinsia wa kila aina.”

Bi Phumzile Mlambo:ubakaji ni ukatili mkubwa

Naye mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake UN Women Phumzile Mlambo- Ngcuka akiunga mkono hayo ametoa wito wa kutokomeza moja ya ukatili mkubwa kabisa ambao ni ubakaji, mitindo yake na gharama zake zisizovumilika kwa wanawake na jamii, “Endapo ningekua na tamanio langu moja litakalotimizwa linaweza kuwa ni kutokomeza kabisa ubakaji na mifumo yote ya ukatili dhidi ya wanawake”. Ubakaji sio tukio tu la kipekee lina athari kubwa za kubadili maisha, mimba au magonjwa ya zinaa, kiwewe kikubwa na aibu. Wakati wote wa amani au wa vita unakuwa sababu ya maamuzi ya wanawake kuondoka katika jamii zao kwa kuhofia kushambuliwa.”

Historia fupi ya Siku ya Kimataifa ya kutokomeza ukatili wa kijinsia

Ikumbukwe kwamba  Siku ya kimataifa ya kutokomeza ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana huadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 25 Novemba iliyokuwabaliwa kunako tarehe  17 Desemba  1999 na Mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa. Tarehe hiyo ilichaguliwa kama siku ya kukumbuka shughuli za kuwasaidia wanawake ambao daima wanaendelea kuwa waathirika wa vurugu, ukatili mkubwa wa ubakaji dhuluma za kijinsia, na matukio ya kukandamizwa ndani ya kuta hata za nyumbani. Hata hivyo tarehe 25 Novemba siyo siku iliyotengwa kwa bahati mbaya bali ni siku ambayo inakumbusha mwaka 1960 ambapo waliuwawa madada watatu wa Mirabal, wanaharakati wa kisiasa kutoka Jamhuri ya Dominika.

Dada watatu wa Mirabal –Jamhuri ya Dominika

Mauaji ya kikatili ya dada hao watatu wa Mirabal yalisikika sana na maoni ya umma. Wanawake hao watatu bado wanafikiriwa kuwa wanamapinduzi kwa jitihada ambayo walijaribu kupinga serikali ya kidikteta ya Rafael Leónidas Trujillo (1930-1961), ambaye aliiweka Jamhuri ya Dominika kuwa nyuma na machafuko.  Kunako tarehe 25 Novemba 1960, wanawake hao watatu walikwenda kuwatembelea waume zao gerezani walipokuwa wamefungwa na barabarani  wakazuiwa na maafisa wa Huduma ya Habari ya kijeshi na ambao waliwapeleka mahali pa siri. Hapa waliteswa, walibakwa, walipigwa kwa mabakola na kuwanyonga kwenye gari lao.

Aliyeokoka kati ya dada hao wa Miarabal alikuwa ni wa nne aitwaye Belgica Adele na ambaye alijitoa maisha yake kwa ajili heshima ya kumbukumbu ya wanawake hao watatu. Yeye baadaye aliachapisha hata kitabu kiitwacho: "memorie:Vivas in su jardin", yaani “kumbukumbu hai katika bustani”. Dada wa Mirabal pia hujulikana kwa jina “Mariposas”, yaani sawa sawa na "vipepeo katika kutafuta uhuru". Hadithi yao pia imeweza kusimuliwa hata katika kazi ya mwandishi wa Kidominika, aitwaye Julia Alvarez, kwa kitabu kiitwacho “kipindi cha vipepeo”, kilicho chapishwa nchini Italia na Giunti. Pia kuna filamu mbili ambazo zinaelezea wasifu wao, ziitwazo kwanza: "In the Time of Butterflies” (2004) yaani “katika wakati wa Vipepeo”  na pili  “Trópico de Sangre” (2010), yaani damu ya kitropiki”.

KUTOKOMEZA UKATILI
25 November 2019, 14:35