Tafuta

Vatican News
Tarehe 14 Novemba ni siku ya kimataifa ya kisukari.Katika fursa hiyo Shirika la Afya duniani limetangaza mpango mpya wa unaowezesha kampuni za kutengeneza dawa duniani itengeneze insulini ya bei nafuu Tarehe 14 Novemba ni siku ya kimataifa ya kisukari.Katika fursa hiyo Shirika la Afya duniani limetangaza mpango mpya wa unaowezesha kampuni za kutengeneza dawa duniani itengeneze insulini ya bei nafuu  (AFP or licensors)

Mpango wa Umoja wa Mataifa kuhusu kushuka bei ya Insulini

Katika harakati za kudhimisha siku ya kimataifa ya kisukari tarehe 14 Novemba,Shirika la Afya Duniani(WHO limechukua hatua ya kutangaza mpango mpya wa unaowezesha kampuni za kutengeneza dawa duniani zitengeneze Insulini ambayo wagonjwa wengi zaidi wa kisukari wataweza kumudu gharama yake. Kuna wagonjwa wagonjwa wengi wa kisukari wanakufa bila msaada.

Na Sr. Angella Rwezaura, - Vatican.

Kwa kawaida gharama ya Insulini ni kubwa mno kiasi kwamba zaidi ya nusu ya wagonjwa wa kisukari wanashindwa kupata huduma hiyo. Ni  uthibitisho wa kauli la Shirika la afya ulimwenguni, (WHO) ambapo tarehe 13 Novemba 2019 wakati wa kuelekea siku ya kimataifa ya kisukari ifikapo kila tarehe 14 Novemba.  Hata hivyo  akizungumzia ugonjwa huu wa kisukari kuelekea maadhimisho ya siku hiyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amegusia janga lililopo sasa la mzigo wa gharama wanazobeba wagonjwa wa kisukari. “Kisukari kinaharibu afya na kinadumaza matarajio ya kielimu na kikazi ya watu wengi,kinaathiri jamii na kulazimisha familia kuishi kwenye maisha dunia hususan katika nchi za kipato cha chini na cha kati.

Kutangaza mpango mpya wa kampuni za kutengeneza dawa duniani

Ni katika  kutambua hilo, Shirika la Afya Duniani (WHO)limechukua hatua kutangaza mpango mpya unaowezesha kampuni za kutengeneza dawa duniani zitengeneze Insulini ya ambayo wagonjwa wengi zaidi ya kisukari wataweza kumudu gharama yake. Imetangaza mpango huo tarehe 13 Novemba 2019 mjini Geneva, Uswisi, ambapo WHO imesema tayari imeshatoa tangazo la awali kwa kampuni zenye nia ya kuzalisha dutu hiyo  na itakuwa salama kwa matumizi ya binadamu. Hata hivyo naye Bwana Emer Cooke, Mkurugenzi wa udhibiti wa dawa na teknolojia nyingine za afya, wa WHO amesema: “Jambo la wazi ni kwamba ugonjwa wa kisukari unazidi kuongezeka na kiwango kilichopo cha Insulini hakitoshelezi, bei ni za juu, kwa hiyo ni lazima tuchukue hatua”.

Ukaguzi wa Insulini kuhakikisha ubora na salama

Ni kwa mantiki hiyo basi, mradi huo wa majaribio kwa miaka miwili wa WHO uliozinduliwa tarehe 13 Novemba 2019  kuelekea maadhimisho ya siku ya kisukari duniani tarehe 14 Novemba  unahusisha ukaguzi wa Insulini inayozalishwa ili kuhakikisha inau bora, salama, inatibu na gharama yake ni nafuu. Kwa kuamini kuwa kampuni nyingi za dawa zinapenda kuzalisha Insulin zaidi ili dutu hiyo ipatikane kwa urahisi zaidi kwa wagonjwa, mradi huo unaweza kupanuliwa zaidi.  “Tutaangalia idadi ya kampuni ambazo zitawasilisha maombi, tutaangalia itachukua muda gani na tutaangalia matokeo yake na iwapo mradi huu unaleta maana na kweli unawezesha Insulini kupatikana zaidi,” amesema Bi. Cooke.

WHO imeshatuma mfumo huu katika chanjo za wanaoishi na VVU,TB

Mfumo wa sasa wa kutangaza na kampuni kuwasilisha maombi unalenga kuhakikisha kuwa vifaa vya uchunguzi, dawa, chanjo na vifaa vya kitabibu vinavyotumika kwenye magonjwa yenye mzigo mkubwa zaidi vinakidhi viwango vya kimataifa, ubora, usalama ili kuweza kuboresha matumizi ya rasilimali za afya. WHO imeshatumia mfumo huu katika chanjo zisizo na majina makubwa ikiwemo zile za kutibu au kuzuia Kifua Kikuu au TB, Malaria na Virusi Vya Ukimwi, VVU. Vile vile  Bi. Cooke amesema mpango huu umekuwa na manufaa makubwa kwa wagonjwa duniani kote ambapo asilimia 80 ya watu wanaoishi na VVU au HIV hivi sasa wanategemea dawa zilizotengenezwa kwa gharama nafuu. Aidha amesema kuwa tayari baadhi ya kampuni zimeahidi kupunguza bei, “wakati dawa za kupunguza makali ya VVU au HIV zilipotengenezwa kwa mara ya kwanza, gharama kwa mgonjwa mmoja kwa mwaka ilikuwa dola 1,000. Lakini baada ya kufungua mchakato wa maombi haya ya kuzalisha za bei nafuu, bei ilipungua hadi dola 300 kwa mwaka.” Kutokana na hiyo Bi. Cooke ameongeza kusema kuwa  wana uhakika  ushindani utapunguza bei na kwa mantiki hiyo serikali zitakuwa na wigo mpana wa kuchagua bidhaa ambazo ni bei nafuu zaidi.

Tangu kugunduliwa Insulini kunako 1921 lakini hadi leo bei yake ni ya juu sana

Hii leo kampuni tatu tu duniani ndio zinadhibiti soko la insulin ambayo iligunduliwa kwa mara ya kwanza kuwa ni tiba dhidi ya kisukari mwaka 1921. Kile ambacho Insulini inafanya ni kupunguza kiwango cha sukari kwenye damu, kazi ambayo kwa kawaida hufanywa na Insulini iliyoko mwilini ambayo huzalishwa na kongosho wakati mtu anapokula chakula. Idadi ya wagonjwa wa kisukari imeongezeka kupindukia tangu mwaka 1980 na kufikia milioni 420 hii leo, idadi kubwa ikiwa ni katika nchi za kipato cha chini na kati, chanzo kikubwa kikiwa ni milo isiyo bora na ukosefu wa mazoezi. WHO inasema kuwa wagonjwa wa kisukari aina ya I ni milioni 20 na wao huhitaji sindano ya Insulini ili waweze kuishi ilhali ni nusu tu ya watu milioni 65 wenye kisukari aina ya II wanaohitaji Insulini ndio huipata.

Katika baadhi ya nchi bei ya Insulini ni mzigo kwa wagonjwa

Katika baadhi ya nchi, WHO inasema kuwa, “bei ni za juu sana kiasi kwamba wagonjwa wanalazimika kuipata kwa mgao. Hii husababisha wawe hatarini kupata kiharusi, figo kushindwa kufanya kazi, upofu na hata kukatwa miguu.” Wakati ugonjwa wa kisukari mwaka 2016 ulikuwa unashika nafasi ya 7 duniani kwa kusababisha vifo, hali inatisha kwa kuwa husababisha watu wafe mapema. Dk. Gojka Roglic, mtaalamu wa ugonjwa wa kisukari WHO amesema:“tunafahamu kuwa siku moja sote tutakufa na kwa nini si kwa kisukari? Lakini basi iwe baada ya kusherehekea miaka 90 ya kuzaliwa. Tatizo ni kwamba kisukari kinachangia asilimia kubwa ya vifo, nusu ni kwa watu ambao hawajafikisha umri wa miaka 70.” Takwimu zilizokusanywa na WHO kutoka mataifa 24 yaliyopo katika mabara 4 zinaonesha kuwa Insulini inapatikana katika asilimia 61 tu ya vituo vya afya. Takwimu hizo kutoka mwaka 2016 hadi 2019 gharama ya mwezi ya Insulini kwa mfanyakazi mjini Accra, Ghana ni sawa na moja ya tano ya msharaha wake.

14 November 2019, 16:26