Tafuta

Vatican News
Raia wa Sudan wameanza kumsubiri Baba Mtakatifu Francisko japokuwa hali halisi ya hewa ni mbaya na watu zaidi ya milioni 8.5 wakiwemo wakimbizi wa ndani milioni 1.9 wanahitaji msaada wa kibinadamu Raia wa Sudan wameanza kumsubiri Baba Mtakatifu Francisko japokuwa hali halisi ya hewa ni mbaya na watu zaidi ya milioni 8.5 wakiwemo wakimbizi wa ndani milioni 1.9 wanahitaji msaada wa kibinadamu   (AFP or licensors)

Jumuiya ya wakristo Sudan wanamsubiri Papa licha ya mahitaji mengi!

Mara baada ya tamko la Baba Mtakatifu la ziara nchini Sudan Kusini 2020,Askofu Edwardo Hiiboro Kussala,wa Jimbo la Tombura Yambo,anasema ziara yake na viongozi wengine kama Askofu Mkuu wa Canterbury na askofu Mkuu wa Kanisa la Presbiteriana wa Scotland itakuwa ni fursa maalum yakuunganisha jumuiya zote za kikristo nchini.Hata hivyo mahitaji ya nchi hiyo ni makubwa sana kwa mujibu wa OCHA.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Askofu Edwardo Hiiboro Kussala,wa Jimbo la Tombura Yambo, mara baada ya tangazo la Baba Mtakatifu Francisko kuhusiana na shauku yake ya kutaka kwenda nchini Sudan Kusini mwaka 2020 amethibitisha kuwa ni matumaini ziara hiyo  itaweza kuwa na utume wa pamoja na ziara ya Askofu Mkuu wa Canterbury Justin Welby na askofu Mkuu wa Kanisa la Presbiterian wa  Scotland. Akizungumza na waandishi wa habari za kimisionari Fides, Askofu Hiiboro, ambaye  hadi mwisho wa mwezi Oktoba alikuwa ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki wa Sudan na viongozi wengine amebainisha kwamba hii itakuwa ni fursa maalum kwa sababu wataunganisha jumuiya zote za kikristo katika nchi yao. Hata hivyo amesema kwamba ikumbukwe mwezi April mwaka huu Baba Mtakatifu Francisko na Askofu wa Canterbury na kiongozi wa Kanisa la Kipresbiterian wa Scotland walikutana na viongozi wa Kisiasa mjini Vatican na kutoa ahadi ya kuwasindikiza watu, hadi Taifa litakapokuwa na amani ya kudumu. Baba Mtakatifu Francisko amekuwa alieleza juu ya  shauku yake ya kutaka kwenda katika nchi yao anasisitiza Askofu  na hii ndiyo sasa maana ya kweli ambayo alitaka.

Kanisa la Sudan linahitaji muungano wa Makanisa ya AMECEA

Na katika kuipokea hiyo shauku ya Baba Mtakatifu Francisko, kama Kanisa mahalia na kama nchi, Askofu  Hiiboro amebainisha kwamba wanahitaji Kanisa lote la muungano wa Kanda zote za AMECEA (zinazounganisha nchi za Afrika ya Mashariki). Kwa niba ya Kanisa Katoliki la Sudan Kusini, Askofu Mkuu anamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuweza kuwa kama  Baba, mchungaji, kiongozi na mfuasi wa Kristo, hata kwa namna ya kuwa hivyo na ukaribu wa watu wa Sudan Kusini. “Watu wetu wametawanyika kutokana na migogoro, katika dunia ya vita, katika maono na umasikini. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kututafuta na ninamshukuru pia kwa hilo.” Ameongeza kusema  Askofu Hiiboro.

Licha ya matarajio ya Baba Mtakatifu,bado mahitaji ya kibinadamu Sudan ni makubwa kwa mujibu wa OCHA

Mahitaji ya kibinadamu nchini Sudan ni makubwa na yanachangiwa na sababu mbalimbali amesema hayo mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA. Bwana Mark Lowcock ambaye yuko katika ziara yake ya kwanza nchini Sudan tangu kuanzishwa serikali ya mpito mwezi Agosti mwaka huu amesema miongoni mwa sababu hizo ni mabadiliko ya tabianchi, milipuko ya magonjwa na mgogoro wa kiuchumi. Bwana Lowcock pia amesema kuwa watu zaidi ya milioni 8.5 wakiwemo wakimbizi wa ndani milioni 1.9 wanahitaji msaada wa kibinadamu na mahitaji yao yanatarajiwa kuongezeka. Hivi sasa kinachotoa hofu kubwa ni milipuko ya magonjwa inayoendelea  na imechochewa na mafuriko ya hivi karibuni ambayo ni mabaya zaidi tangu mwaka 2013, kwani maji yaliyotuama yamekuwa chachu kubwa ya magonjwa yatokanayo na maji na pia mazalia ya mbu.

Mlipuko wa homa ya bonde la ufa:visa 319 vimeripotiwa

Hata hivyo Wizara ya afya nchini Sudan wiki hii imetangaza mlipuko wa homa ya bonde la ufa ambapo hadi sasa kumeripotiwa visa 319 vinavyoshukiwa ikiwemo vifo 11. Kwa mujibu wa OCHA vikosi kazi maalum vimeanmzishwa katika maeneo yaliyoathirika zaidi kwenye majimbo ya Bahari ya Sham na Mto Nile. Pia shughuli za kudhibiti kusambaa kwa wadudu zinaendelea kwa ukaguzi majumbani na kupuliza dawa za kutokomeza mbu. Mkuu wa OCHA amesema moja ya kipengele cha mgogoro wa kiuchumi kinachowaathiri watu wasiojiweza moja kwa moja ni bei ya chakula ambayo bado ni ya juu sana au karibu inavunja rekodi licha ya kuwa na mwaka mzuri wa mavuno mwaka jana na kuwa na matumaini ya msimu mzuri mwaka huu. Akitoa mfano amesema mwezi Oktoba mwaka huu bei ya mtama kwenye masoko mjini Khartoum ilikuwa mara tano zaidi ya mwezi Oktoba mwaka 2017. Hata hivyo Bwana Lowcock amesema ili kuisaidia hatua za kitaifa kukabiliana na hali hiyo makundi ya misaada kote nchini yanachukua hatua kusaidia chini ya mwamvuli wa mpango wa usaidizi wa Umoja wa Mataifa na mpango huo unahitaji dola bilioni 1.1 za ufadhili na hadi sasa umefadhiliwa asilimia 51 tu.

23 November 2019, 12:35