Tafuta

Vatican News
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ametunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel kwa Mwaka 2019 kutokana na jitihada zake za upatanisho, haki na amani kati ya Ethiopia na Eritrea. Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ametunukiwa Tuzo ya Amani ya Nobel kwa Mwaka 2019 kutokana na jitihada zake za upatanisho, haki na amani kati ya Ethiopia na Eritrea. 

Tuzo ya Amani ya Nobel 2019 ni heshima kwa Bara la Afrika

Bwana Abiy Ahmed alichaguliwa kuwa Waziri mkuu wa Ethiopia mwaka 2018 na hapo akajizatiti katika mchakato wa upatanisho wa mipaka kati ya Ethiopia na Eritrea. Wafungwa wa kisiasa wakaachiwa huru, wale waliokuwa wamekimbilia uhamishoni kutafuta: hifadhi na usalama wa maisha yao, wakajisikia huru kurejea tena nchini mwao, ili kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa nchi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, ameshinda Tuzo ya Amani ya Nobel Kwa Mwaka 2019 “Nobel Peace Prize” na hivyo kuwa ni mshindi wa 100 katika Tuzo ya Amani Duniani. Waziri mkuu Ahmed ametunukiwa tuzo hii kutokana na juhudi zake za zilizosaidia mchakato wa upatanisho, haki, amani na maridhiano kati ya Ethiopia na Eritrea, mgogoro ambao ulikuwa umedumu kwa takribani miaka 20, yaani kuanzia mwaka 1998 hadi mwaka 2018. Taarifa zinaonesha kwamba, katika kinyang’anyiro hiki, Waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ameshindana na washiriki wengine 301, kati yao washiriki 223 ni watu binafsi pamoja na makampuni 78. Itakumbukwa kwamba, Bwana Abiy Ahmed alichaguliwa kuwa Waziri mkuu wa Ethiopia mwaka 2018 na hapo akajizatiti katika mchakato wa upatanisho wa mipaka kati ya Ethiopia na Eritrea. Wafungwa wa kisiasa wakaachiwa huru, wale waliokuwa wamekimbilia uhamishoni kutafuta: hifadhi na usalama wa maisha yao, wakajisikia huru kurejea tena nchini mwao, ili kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa nchi.

Waziri mkuu Abiy Ahmed akajipambanua kuwa ni chombo cha amani, haki na upatanisho, kwa kuweka saini mkataba wa amani na Eritrea. Na hiki ndicho kiini cha kuteuliwa kwake kuwa ni mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel kwa Mwaka 2019 na kwamba, huu ni ushindi wa Bara la Afrika na wale wote wanaotaka kuona Bara la Afrika likijikita zaidi katika mchakato wa haki, amani na maridhiano, chachu muhimu sana ya maendeleo fungamani ya binadamu. Waziri mkuu wa Ethiopia amekuwa na ushirikiano wa karibu sana na Rais Isaias Afwerki wa Eritrea, ambao kwa pamoja wanasema hakuna sababu ya vita kati ya Ethiopia na Eritrea, kwani huu ni wakati wa ujenzi wa misingi ya amani. Hata kama bado kuna migogoro ya ndani, lakini Waziri mkuu wa Ethiopia ameanzisha mchakato wa maboresho ya maisha ya wananchi wa Ethiopia pamoja na jirani zake kwa kujikita zaidi katika mchakato wa: upatanisho, mshikamano na haki jamii.

Tuzo ya Nobel ni tuzo ya fedha kwa ajili ya mafanikio ya pekee katika fani mbalimbali. Ilianzishwa na Alfred Nobel. Tangu mwaka wa 1901 imetolewa kwa watu waliojipambanua katika fani zifuatazo yaani: Fizikia, Kemia, Tiba (au Fiziolojia), Fasihi na Amani. Tangu mwaka wa 1969, tuzo ya sita imeongezwa kwa wale wanaojipambanua katika masuala ya Uchumi. Tuzo hii imekuwa na umaarufu sana katika Jumuiya ya Kimataifa. Kwa wale wanaoteuliwa hupokea hati, medali ya dhahabu na kiasi cha fedha takribani dola milioni 1.2.

Tuzo ya Nobel 2019
12 October 2019, 13:41