Tafuta

Viongozi wakuu wanne wa Umoja wa Mataifa wamezitaka Serikali duniani kuchukua hatua za ualimu kama chaguo la kwanza kwa ajira ya vijana katika kilele cha Siku ya Walimu duniani Viongozi wakuu wanne wa Umoja wa Mataifa wamezitaka Serikali duniani kuchukua hatua za ualimu kama chaguo la kwanza kwa ajira ya vijana katika kilele cha Siku ya Walimu duniani 

Chaguo la ualimu liwe la kwanza kwa ajili ya fursa za vijana duniani!

Katika fursa ya maadhimisho ya Siku ya Walimu duniani viongozi wakuu wanne wa Umoja wa Mataifa wametaja hatua nyeti zichukuliwe ili kuvutia vijana kwenye tasnia ya ualimu. Nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara ndizo zenye uhaba zaidi wa walimu ikiwa ni asilimia 70 na kiwango kinafikia asilimia 90 kwenye ngazi ya sekondari.

Tarehe 5 Oktoba ya kila mwaka ni siku ya walimu Duniani, ambapo kwa mwaka 2019, viongozi wa mashirika  manne ya Umoja wa Mataifa na wadau wake wametaka hatua za makusudi zichukuliwe ili kuvutia vijana kwenye tasnia hiyo adhimu. Viongozi hao ni Audrey Azoulay wa UNESCO, Guy Rider wa ILO, Henrietta Fore wa UNICEF, Achim Steiner wa UNDP na David Edwards wa shirika la Elimu Kimataifa. Katika taarifa yao ya pamoja kwa siku hiyo inayoongozwa na mada, “Walimu vijana, mustakabali wa tasnia ya ualimu”, viongozi hao wamesema, “leo hii kufuatia kile tulichojifunza kutoka kwa mbobezi wa fizikia, Albert Einstein, tunasherehekea utaalam, nguvu na wito wa walimu, ambao ndio msingi wa mifumo ya elimu ijayo. Bila kizazi kipya cha walimu wenye motisha, mamilioni ya wanafunzi wataachwa nyuma, au wataendelea kuachwa nyuma kwenye haki yao ya kupata elimu.”

Albert Einstein alinukuliwa akisema kuwa, ni utaalam wa juu kabisa wa mwalimu wa kuamsha ari ya maelezo bunifu na ufahamu ambapo viongozi hao wamesema kwa sasa nukuu hiyo ina changamoto. Wamesema ingawa walimu wenyewe ndio kitovu cha kuendeleza tasnia hiyo, bado kuna changamoto kwa sababu ili waweze “wengi wao hawalipwi vizuri na hawathaminiwi jambo ambalo inafanya vigumu sana tasnia hiyo kuwavutia vijana.” Aidha viongozi hao wameongeza kuwa, tasnia hiyo inazidi kumomonyoka kwa kasi kubwa duniani kutokana na mazingira duni ya kazi na fursa finyu za kujiendeleza na zaidi ya yote, “kuna ukosefu wa rasilimali kwa watoto wenye mahitaji maalum ya elimu na wale wenye  ulemavu, wakimbizi na wale wanaofahamu zaidi  ya lugha moja.” Kwa mantiki hiyo wametaka hatua za dharura kwa kuwa takwimu za UNESCO zinatia wasiwasi mkubwa zikionesha kwamba, “dunia inahitaji walimu milioni 69 ili kufikia lengo la elimu la ajenda 2030. Iwapo walimu hao hawatopatikana, pengo la ukosefu wa usawa duniani litaongezeka.”

Nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara ndio zenye uhaba zaidi wa walimu ikiwa ni kwa asilimia 70 na kiwango kinafikia asilimia 90 kwenye ngazi ya sekondari. UNESCO inasema hali ni mbaya zaidi vijijini kwa sababu ya walimu kukimbilia mijini kutafuta maslahi. Ili kufanikisha lengo la kuwa na walimu bora, UNESCO inataka mbinu mpya zitumike katika kuajiri walimu, kuwafundisha, kuwapatia motisha na kupata walimu wenye ujuzi zaidi kwenye karne hii ya 21. Halikadhalika wakuu hao wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wanatoa wito kwa vyombo vya habari na mbinu nyingine mpya za mawasiliano vitumike kuinyanyua tasnia ya ualimu na kuonyesha umuhimu wake kwa haki za binadamu, haki, na mabadiliko ya tabianchi. “Serikali nazo lazima ziboreshe mazingira ya ajira na kazi kwa walimu. Hili ni jambo la dharura kwa kuzingatia uhaba wa walimu vijana wa kuziba pengo la walimu milioni 48.6 wanaotarajiwa kustaafu kwenye muongo ujao,” wamesema viongozi hao. Kwa kusisitiza zaidi ujumbe wao wanatoa wito kwa serikali zichukue hatua za makusudi ili kazi ya ualimu iwe chaguo la kwanza kwa vijana.

Je Malengo ya  Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni(UNESCO) litaweza kufikia kweli maslahi ya walimu sambamba na ajenda ya maendeleo endelevu ifikapo 2030(SDG's)? mfumo wa ajenda ya 2030 kuhusu elimu unaangazia umuhimu wa walimu katika utoaji wa elimu sawa na bora, na hivyo ili kufikia lengo hilo na chini ya mfumo wenye rasilimali za kutosha, ufanisi unaosimamiwa, ni lazima walimu hao wapate mafunzo ya kutosha, waajiriwe, wapewe motisha na wawezeshwe. 

05 October 2019, 11:21