Tafuta

Siku ya Chakula Duniani 2019: Kauli mbiu: "Lishe Bora kwa Ulimwengu Usio na Njaa". Hii ni dhamana ya watu wote, kuwa na uhakika wa usalama wa chakula ulimwenguni kote. Siku ya Chakula Duniani 2019: Kauli mbiu: "Lishe Bora kwa Ulimwengu Usio na Njaa". Hii ni dhamana ya watu wote, kuwa na uhakika wa usalama wa chakula ulimwenguni kote. 

Siku ya Chakula Duniani 2019: Ujumbe wa Katibu Mkuu UN

Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani ni wito kwa ajili ya kutokomeza baa la njaa kwa kujiwekea sera na mikakati ya kuwa na dunia ambamo chakula chenye lishe bora kinapatikana kwa bei nafuu na kwa watu wote. Kuna watu milioni 820 hawana chakula cha kutosheleza mahitaji yao msingi. Athari za mabadiliko ya tabianchi ni tishio kubwa kwa uhakika na usalama wa chakula duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kila mwaka ifikapo tarehe 16 Oktoba, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Chakula Duniani. Maadhimisho haya kwa Mwaka 2019 yanaongozwa na kauli mbiu “Lishe Bora kwa Ulimwengu Usio na Njaa”. Kauli mbiu hii inalenga kuhamasisha jamii na wadau wote wa sekta kilimo kuchangia kwa hali na mali katika kuhakikisha kwamba,  dunia inakuwa na chakula cha kutosha wakati wote na kwa watu wote. Taarifa za Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, zinaonesha kwamba, kila mwaka theluthi moja ya chakula kinachozaliwashwa kwa ajili ya matumizi ya binadamu kinapotea au kutupwa kama taka, wakati kuna watu milioni 820 sehemu mbali mbali za dunia, wanaoendelea kupekenywa kwa baa la njaa na utapiamlo wa kutisha. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres, anasema Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani ni wito kwa ajili ya kutokomeza baa la njaa pamoja na kujiwekea sera na mikakati ya kuwa na dunia ambamo chakula chenye lishe bora kinapatikana kwa bei nafuu na kwa watu wote na kila mahali.

Lakini hii leo, zaidi ya watu milioni 820 hawana chakula cha kutosheleza mahitaji yao msingi. Athari za mabadiliko ya tabianchi ni tishio kubwa kwa uhakika na usalama wa chakula duniani. Wakati huo huo, takwimu za Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, kuna watu bilioni mbili wenye uzito wa kupindukia, kiasi hata cha kuhatarisha afya yao. Watu wanapaswa kuzingatia lishe bora kwa ajili ya afya zao kwani ulaji mbovu ni hatari sana kwa afya na unaweza kuzua magonjwa na vifo. Kuna haja ya kujenga utamaduni wa matumizi bora ya chakula, kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Ni kutokana na muktadha huu kunako mwaka 2021, Jumuiya ya Kimataifa itaadhimisha Kongamano la Kimataifa kuhusu Mifumo ya Chakula kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Binadamu ifikapo mwaka 2030. Huu ni mchakato wa Jumuiya ya Kimataifa unaotaka kuhakikisha kwamba, inajizatiti katika kutokomeza umaskini, baa la njaa na magonjwa duniani.

Watu wanapaswa kupatiwa elimu bora, kwa kuhakikisha usawa wa kijinsia pamoja na uwezeshaji wa wanawake na wasichana wote. Jumuiya ya Kimataifa inataka kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na upatikanaji wa maji safi na salama; nishati mbadala kwa gharama nafuu pamoja na uwepo wa mipango bora ya miji na makazi ya watu, ili kudumisha usalama na upatikanaji wa maendeleo fungamani ya binadamu. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujifunga kibwebwe kulinda mazingira pamoja na kudumisha amani duniani! Kama familia ya binadamu, anasema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres,   dunia isiyo na njaa ni wajibu wa wote! Upotevu wa chakula kwa mujibu wa FAO hutokea kuanzia baada ya mavuno bila kujumisha mauzo, na upotevu huu unaweza kufanyika na wakulima, mchakato wa uandaaji na wale wanaofanya katika sekta ya usafirishaji kwa ajili ya uuzaji wa chakula.  Na utupwaji wa chakula kwa upande mwingine, hutokea katika ngazi ya soko baina ya muuzaji na mtumiaji.

Na tofauti baina ya upotevu na utupwaji wa chakula ni muhimu kwa sababu watu wana malengo tofauti. Bara la Asia linaongoza kwa kutupa chakula kingi duniani na inakadiriwa kuwa ni asilimia 21%, Marekani na Ulaya wanachangia utupwaji wa chakula kwa asilimia 16% FAO inafafanua kwamba,  kitu cha kwanza kabisa watu wanatakiwa kufahamu kuhusu upotevu na utupwaji wa chakula ili kusaidia kuchukua hatua madhubiti kama mtu mmoja mmoja, kama watunga sera sanjari na kuwekeza katika miundombinu inayohitajika.  Jamii inapaswa kupewa taarifa kuhusu hatua za kupunguza upotevu na utupwaji wa chakula na katika baadhi ya nchi kufanyia mabadiliko ruzuku ya chakula ambazo bila kukusudia zinaweza kuchangia upotevu na utupaji zaidi wa chakula.

Wakati huo huo, Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani, Kitaifa nchini Tanzania kwa Mwaka 2019 yamefanyika mkoani Singida. Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Rehema Nchimbi akizungumza na waandishi wa habari kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho hayo amesema kwamba, Takwimu zilizotolewa na Wizara ya Kilimo zinaonyesha hali yaupatikanaji wa chakula mwaka 2019/2020 ni nzuri, kwani Tanzania, ina chakula cha kutosha. Kiwango cha utoshelevu wa chakula ni asilimia 119%. Uzalishaji wa mazao ya chakula ulifikia tani 16,408,309 ukilinganisha na mahitaji ambayo ni tani 13,842,536. Kati ya hizo Tani 9,007, 909 ni mazao ya nafaka na tani 7,400,400 ni mazao yasiyo nafaka. Serikali ya awamu ya tano inawapongeza wadau wa kilimo nchini Tanzania kwa kutekeleza kauli mbiu hii kwa vitendo.

Siku ya Chakula 2019
16 October 2019, 13:28