Tafuta

Vatican News
Kuna haja ya chanzo ya kuzuia Surua na magonjwa mengine ya watoto barani Afrika Kuna haja ya chanzo ya kuzuia Surua na magonjwa mengine ya watoto barani Afrika 

Kuna idadi ya vifo 4,000 kutokana na Surua nchini Congo DRC!

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto,UNICEF kupitia taarifa yake iliyotolewa tarehe 9 Oktoba 2019 katika miji ya New York,Marekani na Kinshasa, DRC inasema idadi ya vifo 4,000 vya ugonjwa wa Surua nchini DRC.Na ni tangu mwezi Januari mwaka huu kati ya wagonjwa 203,179 walioripotiwa kwenye majimbo yote 26 ya taifa hilo.

Mlipuko wa ugonjwa wa Surua nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC umeendelea kuwa tishio wakati huu ambapo idadi ya vifo imefikia 4,000 na hivyo kulazimu mashirika ya Umoja wa Mataifa kuendelea kuwapatia chanjo watoto zaidi na kupeleka dawa za kuokoa maisha. Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF kupitia taarifa yake iliyotolewa tarehe 9 Oktoba 2019 katika miji ya New York, Marekani na Kinshasa, DRC inasema idadi hiyo ya vifo ni tangu mwezi Januari mwaka huu kati ya wagonjwa 203,179 walioripotiwa kwenye majimbo yote 26 ya taifa hilo.

Cha kusikitisha zaidi, asilimia 74 ya wagonjwa hao wa surua ni watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano na mbaya zaidi takribani asilimia 90ya vifo ni watoto wa umri huo. Mwakilishi wa UNICEF nchini DRC, Edouard Beigbeder amesema idadi  ya wagonjwa wa surua nchini humo mwaka huu ni mara tatu zaidi ya wagonjwa walio ripotiwa mwaka 2018 huku akisema kuwa surua umekuwa ugonjwa hatari zaidi kuliko Ebola ambayo tangu mwezi Agosti mwaka jana hadi leo hii umesababisha vifo vya watu 2,143. Bwana Beigbeder amesema, “tunakabili mlipuko wa Surua kwa njia mbili, kwa kuzuia maambukizi na kuzuia vifo. Kwa ushirikiano na serikali na wadau wetu wakuu, tunaongeza kasi ya utoaji wa chanjo kwa watoto na wakati huo huo tunazipatia kliniki dawa kutibu dalili za ugonjwa na kuongeza fursa ya walioambukizwa kuweza kuishi.”

Tayari wiki hii pekee, vikasha 1,111 zaidi vya tiba vimesambazwa kwenye vituo vya afya katika maeneo hatari zaidi kukumbwa na surua ambapo vikasha hivyo vina dawa aina za viuavijasumu, maji yenye chumvi, Vitamin A, dawa za kuzuia maumivu na vifaa vingine kwa ajili ya zaidi ya watu 111,000 walioambukizwa ugonjwa huo hatari. Katika mwaka mmoja uliopita, UNICEF imesambaza zaidi ya dozi milioni 8.6 za chanjo dhidi ya surua ambapo shirika hilo liliongoza kampeni ya chanjo kwenye majimbo manane yaliyokumbwa zaidi na surua na kupatia chanjo watoto zaidi ya milioni 1.4. Kampeni ya hivi karibuni zaidi ni ya kwenye jimbo la Kasai ya Kati ambako zaidi ya watoto 210,000 walipatiwa chanjo.

Hata hivyo mwakilishi huyo wa UNICEF nchini Congo DRC amesema, “tunakabiliwa na hali tete kwa sababu mamilioni ya watoto wa DRC wanakosa mzunguko wa chanjo na hawawezi kupata huduma za afya pindi wanapougua. Na zaidi ya hapo mfumo dhaibu wa chanjo, ukosefu wa usalama, tabia ya jamii kutoamiamin chanjo na watoa chanjo sambamba na changamoto za miundombinu vinasababisha watoto wengi wasio na chanjo kuwa hatarini kuambukizwa surua.” Kwa mujibu wa shirika la afya ulimwenguni, (WHO), kinacho pendekezwa ni dozi mbili za chanjo dhidi ya surua na takribani asilimia 95 ya wananchi w DRC wanapaswa kupatiwa chanjo ili kujenga kinga ya mwili na kuzuia milipuko.

Nchini Congo( DRC), kwa mwaka 2018, chanjo dhidi ya surua ilifikia asilimia 57 tu ya wananchi wote. “Iwapo tunataka kuepusha milipuko mibaya zaidi kama hii ya surua siku za usoni, lazima kunapaswa kuwepo uwekezaji wa hali ya juu katika kuimarisha mpango wa chanjo wa kitaifa, DRC na kushughulikia changamoto za ufikiaji eneo kubwa zaidi,” amesema Bwana Beigbeder. Tayari serikali ya DRC inajiandaa kuzindua awamu ya pili ya kampeni ya chanjo tarehe 22 Oktoba 2019,  ambayo ina lengo kupatia chanjo dhidi surua watoto wenye umri kuanzia miezi 6 hadi miaka mitano katika majimbo yote 26. Kampeni hii inaungwa mkono na wadau wengi ikiwemo UNICEF ambayo inatoa msaada wa kiufundi katika ngazi ya kitaifa, majimbo hadi vijijini kwa kusambaza chanjo na kusaidia kuendesha kampeni ya uhamasishaji.

10 October 2019, 14:35