UNICEF: Wanawake tekelezeni wajibu na dhamana ya kuwanyonyesha watoto wenu kadiri ya taratibu na kanuni za afya bora. UNICEF: Wanawake tekelezeni wajibu na dhamana ya kuwanyonyesha watoto wenu kadiri ya taratibu na kanuni za afya bora. 

Juma la Kimataifa la Kunyonyesha: Oktoba 2019: Faida & Hasara!

UNICEF inasema, kuna hatari inayoweza kuwakumba watoto sehemu mbali mbali za dunia kutokana na mama zao kushindwa kuwanyonyesha kadiri ya taratibu. Kuna wasi wasi kwamba asilimia 40% ya watoto wote duniani katika ya siku moja hadi miezi sita hawapati fursa ya kunyonya maziwa ya mama zao ambayo kimsingi yana virutubisho vingi kwa ajili ya kinga kwa mtoto mchanga.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, katika maadhimisho ya Juma la Kimataifa la Kunyonyesha, kuanzia tarehe 01 Oktoba hadi tarehe 07 Oktoba 2019 linasema, kuna hatari kubwa inayoweza kuwakumba watoto sehemu mbali mbali za dunia kutokana na mama zao kushindwa kuwanyonyesha kadiri ya taratibu za Jumuiya ya Kimataifa. Kuna wasi wasi kwamba asilimia 40% ya watoto wote duniani katika ya siku moja hadi miezi sita hawapati fursa ya kunyonya maziwa ya mama zao ambayo kimsingi yana virutubisho vingi, hali ambayo ingeweza kuchangia kukinga watoto hao dhidi ya magonjwa pamoja na kuokoa maisha yao. UNICEF inapenda kuwahamiza wanawake wanaonyonyesha watoto wao kuhakikisha kwamba, wanaifanya kazi hii kwa ufasaha zaidi, ili kuokoa maisha ya watoto wao.

Wataalam wa Lishe Kimataifa wanahimiza umuhimu wa akinamama kufuata taratibu za kitaalamu katika kunyonyesha watoto wao ili kuhakikisha kwamba, wanapata maziwa ya kutosha na kukua vizuri. Mtindo wa kutofuata taratibu na kanuni zinazotakiwa katika kunyonyesha kunapelekea watoto wengi kupata maradhi ya utapiamlo na kutokukua vizuri, hali inayohatarisha hata maisha yao kwa siku za mbeleni. Katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo mtoto hatakiwi kupewa chakula kingine chochote, hata maji, isipokuwa maziwa ya mama pekee kwani yana virutubisho vya kutosha kwa ajili ya kujenga afya yake. Baadhi ya taratibu za kitaalamu za kunyonyesha mtoto ni katika kipindi cha muda wa dakika 20 kila baada ya saa mbili kwa kipindi cha miaka miwili bila kumuachisha ziwa.

Kuna haja ya kujenga mazingira bora ndani ya familia ili kumwezesha mama anayenyonyesha kupunguziwa mzigo wa kazi na kupata nafasi ya kuweza kutekeleza dhamana hii nyeti katika malezi na makuzi ya mtoto! Zifuatazo ni faida za kuwanyonyesha watoto: Kunyonyesha ni moja ya njia sahihi ya kuhakikisha mtoto anakuwa mwenye afya na kuendelea kuishi. Kama viwango vya kunyonyesha vingekuwa vya hali ya juu duniani, takriban maisha 820, 000 ya watoto yangenusurika kila mwaka, linasema Shirika la Afya Duniani,WHO. Unyonyeshaji wa mtoto kwa miezi 6 kuna faida nyingi za kiafya kwa mama na mtoto. Kumnyonyesha mtoto mara anapozaliwa kwa kipindi cha saa moja, humkinga kwa maambukizi yanayowapata watoto wachanga na kupunguza vifo vya watoto wachanga. Maziwa ya mama pia ni chanzo muhimu cha nguvu na virutubisho kwa watoto wa kati ya miezi 6 hadi 23.

Wachunguzi wa malezi na makuzi ya watoto wadogo wanasema, maziwa ya mama yanaweza kuchangia nusu au zaidi ya nguvu za mtoto katika umri wa miaka 6 hadi 12. Watoto na vijana wadogo walionyonyeshwa wakiwa wachanga wana uwezekano mdogo wa kuwa na uzito wa mwili wa kupindukia. Unyonyeshaji wa mtoto humsaidia kuboresha uwezo wa utambuzi wa akili (IQ), mahudhurio ya shule, na pia huhusishwa na mapato ya juu katika maisha yake ya utu uzima. Kunyonyeshwa kwa muda mrefu pia huchangia afya na maisha bora ya mama kwani humpunguzia hatari ya kupata saratani ya mfuko wa mayai ya uzazi na matiti. Kunyonyesha hutengeneza vichocheo vya mwili (hormone) ambazo humtuliza mama na mtoto. Juma hili linaadhimishwa huku baadhi ya wanawake duniani wakishindwa kuwanyonyesha watoto wao ipasavyo kutokana na sababu mbali mbali.

Baadhi ya imani potofu kuhusu kunyonyesha: Maziwa ya kwanza ya mama si mazuri kwa mtoto yanapaswa kumwagwa. Kunyonyesha humfanya mama anenepe kupindukia. Maziwa ya mama pekee hayawezi kumridhisha mtoto wa umri wa miezi 0 hadi sita. Baadhi ya vyakula si vizuri kwa wanawake wanaonyonyesha. Ni lazima mtoto mchanga anywe maji mara baada ya kuzaliwa. Maziwa ya mama humfanya mtoto ajihisi mwenye kiu. Baadhi ya wanawake hudai wanaponyonyesha matiti yao husinyaa na kuanguka.

UNICEF
01 October 2019, 13:31