Tafuta

Waziri mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, avitaka vyombo vya sheria kuwashughulikia mara moja wale wote wanaotuhumiwa "kumung'unya fedha ya maji mkoani Iringa", ili sheria ishike mkondo wake. Waziri mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, avitaka vyombo vya sheria kuwashughulikia mara moja wale wote wanaotuhumiwa "kumung'unya fedha ya maji mkoani Iringa", ili sheria ishike mkondo wake. 

Waliomung'unya fedha ya maji Iringa kukiona cha mtema kuni!

Waziri Mkuu alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela afuatilie suala hilo kwa kuwa kamati nyingi za watumiaji maji zimekuwa na tuhuma za matumizi mabaya ya fedha ya umma. Waziri Mkuu alitaka watuhumiwa wote wanaohusika na ubadhilifu huo wakamatwe mara moja na kufikishwa katika vyombo vya dola kwa ajili ya kwenda kujibu tuhuma zinazowakabili.

Na Ofisi ya Waziri Mkuu, - Iringa, Tanzania.

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ameagiza kukamatwa na kuwekwa ndani viongozi wa kamati ya watumiaji maji wa mradi wa maji wa Matunguru uliopo katika Kijiji cha Tungamalenga wilayani Iringa kwa tuhuma za ubadhilifu wa sh. milioni saba. Ametoa agizo hilo Jumamosi, Septemba 28, 2019 baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Idodi wilayani Iringa. Waziri Mkuu alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela afuatilie suala hilo kwa kuwa kamati nyingi za watumiaji maji zimekuwa na tuhuma za matumizi mabaya ya fedha zinazokusanywa kutoka kwa wananchi jambo ambalo si sahihi. Waziri Mkuu alitaka watuhumiwa wote wanaohusika na ubadhilifu huo wawe wameshakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya dola kwa ajili ya kwenda kujibu tuhuma zinazowakabili.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema kwamba Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Iringa hadi Ruaha yenye urefu wa kilomita 104 ili kuboresha huduma za usafiri kwa wakazi wa maeneo hayo na kuinua uchumi. Waziri Mkuu aliyasema hayo baada ya kupokea malalamiko ya ubovu wa barabara hiyo kutoka kwa mbunge wa jimbo la Ismani, William Lukuvu ambaye pia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Mbunge huyo alisema licha ya Serikali kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo ikiwemo ya maji, afya na umeme, lakini wanakabiliwa na tatizo la ubovu wa barabara ambapo aliomba Serikali iwasaidie. Baada ya Waziri Mkuu kusema kuwa Serikali itahakikisha barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami wananchi walifurahi na kuishukuru Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli kwa kuwajali wananchi wake.

Awali, Waziri Mkuu alikagua na kuzindua majengo matano ya kituo cha afya Idodi ambayo yamegharimu sh. milioni 400. Pia Serikali iliongeza sh. milioni 300 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba. Waziri Mkuu alisema ameridhishwa na ujenzi wa mradi huo. Kwa upande wao baadhi ya wagonjwa waliolazwa katika wodi ya Mama na Mtoto ambao walikuwa wajifungua kwa njia ya upasuaji waliishukuru Serikali kwa kuboresha na kusogeza huduma za afya karibu na makazi ya wananchi. Mmoja wa wagonjwa hao, Agusta Nyagawa alisema awali walikuwa wanalazimika kwenda hadi Iringa mjini kwa ajili ya kufuata huduma za afya lakini kwa sasa huduma hizo zikiwemo za kujifungua pamoja na vipimo wanazipata kituoni hapo. Naye, Chipe Ngugi alisema anaishukuru Serikali kwa kuwa huduma za afya zimeboreshwa katika hospitali yao ya kata, hivyo hawatalazimika tena kusafiri umbali mrefu hadi Iringa kwa ajili ya kufuata huduma za afya zikiwemo za upasuaji. Alisema yeye alijifungua kwa njia ya upasuaji na anawashuwashukuru madaktari na wauguzi kituoni hapo kwa huduma nzuri ambazo zimeokoa maisha yake na mtoto. Aliiomba Serikali iendelee kuboresha huduma kwa kuwa wapo mbali na mjini. 

 

30 September 2019, 13:21