Tafuta

Vatican News
Kimbunga Dorian kimeleta madhara makubwa kisiwani bahamas,kwa maana hiyo Shirika la Kuhudumia watoto,Unicef,linahitaji msaada wa dola milioni 4 kwa ajili ya dharura ya watoto na familia zao Kimbunga Dorian kimeleta madhara makubwa kisiwani bahamas,kwa maana hiyo Shirika la Kuhudumia watoto,Unicef,linahitaji msaada wa dola milioni 4 kwa ajili ya dharura ya watoto na familia zao  (ANSA)

UNICEF:Shirika la Kuhudumia Watoto linaomba msaada wa kuwasaidia na familia zao huko Bahama!

Katika harakati za dharura ya kusaidia waathirika wa Kimbunga Dorian visiwani Bahama,Shirika la kuhudumia watoto UNICEF linahitaji dola milioni 4 ili kusaidia mahitaji ya haraka ya watoto na familia zao.Inasadikika takribani ya watoto 18,000 kwenye kisiwa cha Abaco na kisiwa cha Bahama Kuu wameathiriwa na kimbunga Dorian ambapo wengi wao wanahitaji misaada ya kibinadamu.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema linatahija dola milioni 4 za dharura ili kusaidia mahitaji ya haraka ya watoto na familia zao huko visiwani Bahama baada ya kimbunga Dorian kupiga eneo hilo na kusababisha madhara makubwa. Kwa mujibu wa UNICEF, dola milioni 4 zinalenga kufanikisha upatikanaji wa maji safi na salama, huduma mbalimbali kama vile lishe, misaada ya kisaikolojia na elimu.

Ombi la UNICEF linakuja wakati huu ambapo ndege iliyosheheni tani 1.5 ya misaada ya dharura ya kuokoa maisha iliwasili mapema wiki hii kwenye mji mkuu wa visiwa vya Bahama, Nassau. Vifaa hivyo ikiwa ni pamoja na vidonge 400,000 vya kutakatisha maji, matenki kadhaa ya ujazo wa lita 5,000 za maji na madumu 1,000 ya kutekea maji, vinalenga kusaidia zaidi ya watoto 9,500 na familia zao kupata maji safi na salama kufuatia kimbunga Dorian kilichosambaratisha miundombinu ya maji nchini humo. Taarifa ya UNICEF iliyotolewa tarehe 9 Septemba 2020 huko New  York, Marekani, kuwa shehena hiyo ni ya kwanza kupelekwa na shirika hilo na ilisafirishwa na ndege ya shirikisho la msalaba mwekundu na hilal nyekundu, IFRC na vinatarajiwa kuanza kusambazwa kwa jamii siku chache zijazo.

Inasadikika kuwa takribani watoto 18,000 kwenye kisiwa cha Abaco na kisiwa cha Bahama Kuu wameathiriwa na kimbunga Dorian ambapo wengi wao wanahitaji misaada ya kibinadamu, ambapo makadirio hayo ni kwa mujibu wa mamlaka ya dharura za majanga ya Karibea, CEDMA. Mapema Ijumaa tarehe 6 Septemba 2019  UNICEF iliweza kufika eneo la Abaco, eneo ambalo limeathiriwa zaidi na kimbunga Dorian kilichopiga visiwa vya Bahama mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo maafisa wa shirika hilo walishuhudia uharibifu mkubwa, ikiweme shule kusambaratishwa, halikadhalika hospitali, nyumba, barabara huku magari na mashua vikiwa vinang’inia kwenye miti!

Naye Youssouf Abdel-Jelil, Naibu Mkurugenzi wa UNICEF kanda ya Amerika ya Kusini na Caribean amesema, “Watoto na familia zao ambao wamenusurika kwenye kimbunga hiki wamepoteza nyumba zao, mbinu zao za kuishi, ndugu na jamaa na wamesalia na kiwango kidogo cha maji na chakula,” Aidha Bwana Abdel-Jelil amesema, muda unakwenda kwa wao kupata misaada na  kuwa siku tano tangu kimbunga hicho kipige eneo hilo, maji safi na salama ni vitu vinavyohitajika zaidi sambamba na vifaa vya dharura kwa ajili ya akina mama na watoto.

10 September 2019, 15:04