Tafuta

Mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa umefunguliwa rasmi na Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, watu wanataka kuona vitendo, wamechoka na maneno matupu! Mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa umefunguliwa rasmi na Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, watu wanataka kuona vitendo, wamechoka na maneno matupu! 

Mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa: Mazingira

Mkutano huu hauna budi kutoa majibu muafaka ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Huu si wakati wa hotuba nzuri, bali utekelezaji wa ahadi. Jumuiya ya Kimataifa ikishikamana, inaweza kushinda kipeo cha athari za mabadiliko ya tabianchi. Ongezeko la nyusi joto Selsiyasi 3 ifikapo mwaka 2050 ni hatari kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Utunzaji wa Mazingira!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres, Jumatatu, tarehe 23 Septemba 2019 amefungua rasmi mkutano wa 74 wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa ambalo kwa sasa linajadili kuhusu  utekelezaji wa sera na mikakati ya kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi. Kwa namna ya pekee, Umoja wa Mataifa unawashukuru na kuwapongeza vijana ambao wameendelea kusimama kidete katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, huku wakiwataka wanasiasa kuwasikiliza wanasayansi na kutekeleza kwa vitendo ushauri unaotolewa ili kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi. Nchi 77 zenye viwanda vingi duniani, zimeamua kutozalisha kabisa hewa ya ukaa ifikapo mwaka 2050 kwa kuendelea kuwekeza katika teknolojia rafiki pamoja na kuendelea kuhamia katika uchumi wa kijani, unaojali na kuthamini utunzaji bora wa mazingira.

Kiasi cha dola za kimarekani Trilioni 2 zitawekezwa kwenye teknolojia rafiki na mazingira, ifikapo mwaka 2025, kwa kusaidia kuinua uchumi wa nchi 20 zinazochechemea kwa maendeleo sehemu mbali mbali za dunia. Benki 130 zimeahidi kuchangia katika mchakato wa Utekelezaji wa Makubaliano ya Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, COP21 uliotiwa sahihi kunako mwaka 2015, unazitaka nchi tajiri zaidi duniani kuonesha mshikamano wa dhati katika mchakato wa mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi, ili kujenga matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi kwa vizazi vijavyo! Ongezeko la hewa ya ukaa na joto duniani, kutasababisha pia kuongezeka kwa kina cha bahari sehemu mbali mbali za dunia, hali ambayo itapelekea maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Uchafuzi mkubwa wa mazingira unaendelea kuhatarisha upatikanaji wa maji safi na salama, sehemu ya haki msingi za binadamu na matokeo yake, ni watu wengi kuendelea kupoteza maisha kutokana na magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya maji machafu. Hali hii ina madhara makubwa katika mchakato mzima wa uchumi na maendeleo. Huu ni wakati kwa wadau mbali mbali kutekeleza dhamana na wajibu na ahadi zao, ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi. Ni wakati wa kuendelea kujikita katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kwa ajili ya kizazi hiki na kile kijacho.  Kwa kuwa kwa sasa kuna ongezeko kubwa la kiwango cha joto, kuenea kwa ukame wa kutisha pamoja na ongezeko la majanga asilia. Mkutano huu hauna budi kutoa majibu muafaka ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Huu si wakati wa hotuba nzuri, bali utekelezaji wa ahadi. Jumuiya ya Kimataifa ikishikamana, inaweza kushinda kipeo cha athari za mabadiliko ya tabianchi. Ongezeko la nyusi joto Selsiyasi 3 ifikapo mwaka 2050 ni hatari kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Wanaharakati vijana katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, wakiongozwa na Greta Thunberg kutoka Sweden wanawataka viongozi wa kisiasa kutekeleza ahadi zao, ili kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi.

Katibu Mkuu UN
24 September 2019, 14:55