Tafuta

Vatican News
Martinho Mateus da Silva ametoa ushuhuda wa maisha yake akiwa mdogo wakati wa vita nchini Msumbiji Martinho Mateus da Silva ametoa ushuhuda wa maisha yake akiwa mdogo wakati wa vita nchini Msumbiji 

Msumbiji:Historia ya Martinho:majeraha ya vita yemepona kwa njia ya msamaha!

Kabla ya kuondoka na wengine kwenda Msumbiji kama wawakilishi wa Vatican News,katika ziara ya Papa nchini Msumbiji,Padre Paulo Samasumo amehojiana na Bwana Martinho Mateus da Silva mzaliwa wa Msumbiji ambaye anaishi nchini Italia.Ni mwanzilishi na rais mstaafu wa Chama cha wanamsumbiji wanaoishi Italia.Ametoa ushuhuda wa historia ya kusisimua kuhusu vita vya wenyewe kwa wenyewe na kupoteza kila kitu hata baba yake.

Na Sr. Angela Rwezaula -Vatican

Ziara ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika kwa namna ya pekee mwezi huu katika nchi tatu, Msumbiji, Madagascar na Mauritus, ni moja ya historia ambayo inajirudia kila wakati anapopata fursa ya kutembelea nchi kadhaa. Ni njia mwafaka ya kuchimba chimba habari zaidi zinazohusu nchi ambayo kwa kawaida Baba Mtakatifu anakwenda kutembelea. Kutokana na hilo mwakilishi wetu Padre Paulo Samasumo na wengine wa Vatican News, kwa sasa wapo nchini Msumbiji katika fursa ya Ziara ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko, nchini Msumbiji na nchi nyingine, Madagascar na Mariutius. Kabla ya kuondoka kwenda nchini Msumbiji tayari kutuhabarisha kinachojiri na kitakachojiri huko kwenye ziara ya kitume, amekutana na kufanya mahojiano na Martihno Mateus da Silva. Bwana Da Silva kwa sasa anaishi nchini Italia pia ni mwanzilishi na rais mstaafu wa Chama cha wanamsumbiji wanaoishi Italia. Hii ni historia ya kusisimua ya maisha yake, hasa kwa kuzingatia mantiki au mada ya matumaini, amani na upatanisho ambayo ni kauli mbiu ya ziara ya Baba Mtakatifu nchini Msumbiji. Padre Samasumo anasema kuwa, amekutana na Bwana Martinho wakati anatafuta baadhi ya shuhuda fupi kutoka kwa kiongozi wa Jumuiya ya wanamsumbiji nchini Italia. Lengo lake lilikuwa ni kutaka kujua mtazamo wake kwa ujumla kuhusiana na ziara ya Baba Mtakatifu Francisko katika ardhi yake ya asili.

Ni furaha kwa hakika ziara hii ya Papa kugusa wanamsumbiji

Ni mara moja tu alipoanza kuzungumza naye, alitambua ni kwa jinsi gani, hakika ziara ya Baba Mtakatifu Francisko inamgusa kwa karibu  sana na kwa watu walio wengi wa Msumbiji. Ni furaha kubwa kwa hakika anathibitisha kwamba, Baba Mtakatifu amechagua kupaza sauti ya uchungu na mapambano yao nchini humo, kwa maana hiyo ziara hii kwa  upande wa rais ina maana kubwa, anasema Padre Samasumo. Akianza kuelezea historia  yake Bwana Da Silva anasema kwamba, baba yake alikufa wakati wa vita. Yeye aliunguzwa  ndani ya gari hadi majivu, kwa maana hiyo wao hawakuona mwili wake. Bwana Martinho ameeleza historia  hii mbaya inayozungukia wapendwa wake. Alipoteza hata baba zake wadogo na ndugu wa karibu wakati wa vita. Watu wengi nchini Msumbiji waliacha nchi yao na wakaishia kuwa wakimbizi katika nchi za jirani kama vile Zimbabwe, Zambia, Malawi na Tanzania. Aidha anasema familia yake  haikuondoka nchini humo kwenda katika kambi ya wakimbizi, bali wao walibaki nyumbani, lakini maisha yake akiwa mdogo yalipitia  kukimbia huko na kule katika eneo dogo la InhaIania- Barue wilayani Manica katika msituni mahali ambamo walikuwa wanajificha na hofu ya mapigano au kuhofia kukamatwa mafichoni.

Akiendelea na historia ya vita vya msumbiji anasema kuwa aliweza kuponea chupu, lakini shukrani kwa  Mungu na mama yao

Mtazamo wa kwanza kwa kawaida Padre Samasumo anasema, unadanganya kwa maana ya kwamba tendo la kukutana na Martinho,  huwezi kufikiria kama ni mtu rafiki, mchangamfu, mkarimu na aliye tulia. Anazungumza lugha nne za Ulaya. Yeye anafanya kazi mjini Vatican na amekwisha kaa nchini Italia kwa miaka 15 sasa. Martinho ameoa mwanamke mwenye asili ya Kenya, ambapo ana familia ya watoto watatu, lakini licha ya hayo yote mwoyoni kwake bado kovu ni hai, hasa kwa kufikiria vita vilivyotokea nchini humo na ambapo alipata uzoefu huo akiwa mdogo na kumnyima furaha ya udogo. Katika historia yake anasimulia pia ni kwa jinsi gani hakupata bahati ya kucheza na watoto wengine wadogo. Wengi wa ndugu zao wa karibu walikufa wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe, kwa maana hiyo macho yake yanaonesha wazi uchungu huo.

Sikuwa na lolote kwa maana nilipoteza kila kitu kwa sababu ya vita

Akijibu ni kwa njia gani aliweza kuokoa na kufika mahali alipo, anajibu ni kwa neema ya Mungu na mama yake. Familia yake imeweza kutunzwa anathibitisha ni kutokana na mama yake ambaye hakuchoka kusisitiza kwenda shuleni pamoja na mambo mengi. Martinho anaeleza kipindi kigumu cha maisha yake kwani hawakuwa na kitu chochcote wakati wa vita. Mama yake alikuwa akienda kutafuta chakula cha kuwawezesha waende mbele. Na ndiyo kwa namna hiyo waliweza kula. Hadi leo hii amesema hajuhi ni kwa namna gani aliweza kusaidia familia yake hasa kwa kile kidogo alicho wawezesha kuweka katika  mdogo wao na kutafuna kitu katika changamoto za vita na hata ukame ambao ulikuwa unaikumba Afrika ya kusini kipindi cha miaka ya 90. Hata hivyo siyo kwamba mambo yote daima yalikwenda vizuri. Wakati mwingine walikosa chakula na mara nyingi walikula mlo mmoja kwa siku. Maduka ya karibu zaidi ambayo ungeweza kununua chochote kile yalipatikana katika nchi ya jirani  Zimbabwe lakini ilitakiwa uthubutu wa kujihatarisha au kukamatwa njiani au hapana. Na daima kulikuwa na hatari za mabomu yaliyotegwa ardhini.

Mkataba mpya wa amani nchini Msumbiji

Nchi ya Msumbiji ilipata uhuru wake kunako mwaka 1975 kutoka mikononi mwa ukoloni wa kireno. Lakini hali halisi ya uhuru kamili uliingiliwa na kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya nguvu tawala za Frelimo na chama cha Upinzani-Renamo. Kutokana na hiyo vita mbaya sana ilidumu kwa muda mrefu. Inasadikika kuwa watu milioni moja wamekufa kwa kipindi cha miaka kumi na sita wakati wa mapigano, na maelfu ya watu kukumbwa baa la njaa na majeruhi au ulemavu wa viungo kufuatia na mabomu ya kutegwa ardhini. Milioni tano ya watu walilazimika kukimbia na kuacha nyumba zao. Hata hivyo kwa sasa, vyombo vya habari  ndani ya nchi vinasema makubaliano mapya ya amani yaliyosainiwa mnamo Agosti 2019 yanatoa ahadi kwa sababu ni mpango wa ndani ya nchi. Wapatanishi wa kimataifa ni kutoka Jumuiya ya Mtakatifu Egidio Roma, Rais mstaafu  Bwana Jakaya Kikwete wa Tanzania, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), balozi wa Uswizi nchini Msumbiji, Mirko Manzoni, wapatanishi Neha Sanghrajka na Jonathan Powell wamechangia. Lakini  mwisho wa yote  hayo ni kusema kuwa imetokana na  makubaliano ya amani ya kitaifa ndani ya nchi! Na ni Rais Filipe Nyusi na kiongozi wa zamani marehemu wa Renamo, Alfonso Dhlakama walioongoza. Na baadaye yakafuatia mazungumzo kati ya Rais Nyusi na kiongozi mpya wa Renamo, Ossufo Momade.

Mshangao wa Papa kwa furaha nchini Msumbiji

Bwana Martinho akifafanua ni hisia gani aliyo nayo kufuatia na ziara ya Papa nchini Msumbiji, amejibu kuwa, Baba Mtakatifu atashangazwa na furaha hasa wakati wa Misa katika uwanja wa Zimpeto. Ni furaha kubwa hasa kwa sababu Papa anakwenda Msumbiji kuwatia moyo watu na kwa ajili ya kupeleka amani na matumaini na hasa zaidi matumaini! Watu wa Msumbiji wanahitaji matumaini katika kipindi hiki. Hawakuwahi kuwa na amani ya kweli tangu enzi za ukoloni kunako mwaka 1964 ambapo vilianza vita vya kuwania uhuru amethibitisha Bwana Martinho. Hatimaye akizungumza juu ya msamaha kwa ajili ya Msumbiji na wakati endelevu anasema, kwa ajili ya watu wa Msumbiji na kizazi cha nyakati zake na kwa wale walio wazee, baadhi bado wana hasira kwa sababu ya vita na misiba iliyowapata. Lakini kwa ujumla watu wa Msumbiji wanawajibu mbele ya kizazi kijacho. Lazima kusamehe na kuanza upya, kwa maana majeraha yanapona kwa njia ya msamaha. Amethibitisha hayo kwa uhakika.

04 September 2019, 09:53