Tafuta

Rais Filipe Jacinto Nyusi analishukuru Kanisa kwa kuchangia ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Msumbiji hasa katika elimu, afya, ustawi na maendeleo fungamani. Rais Filipe Jacinto Nyusi analishukuru Kanisa kwa kuchangia ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Msumbiji hasa katika elimu, afya, ustawi na maendeleo fungamani. 

Hija ya Papa Francisko Msumbiji: Hotuba ya Rais Nyusi: Mshikamano

Rais Filipe Jacinto Nyusi amelishukuru na kulipongeza Kanisa Katoliki kwa mchango wake mkubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Msumbiji hasa katika sekta ya elimu, afya, ustawi wa jamii na maendeleo fungamani ya binadamu. Uwepo wa wamisionari nchini Msumbiji umewajalia wananchi wengi kupata fursa ya elimu. huduma na fursa za ajira.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa viongozi wa Serikali, wanadiplomasia pamoja na wawakilishi wa vyama vya kiraia nchini Msumbiji, Alhamisi tarehe 5 Septemba 2019, ameonesha uwepo wake wa karibu, upendo na mshikamano na familia ya Mungu nchini Msumbiji kutokana na majanga asilia. Amekazia umuhimu wa kujenga amani na upatanisho wa kidugu; mchakato wa maendeleo endelevu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Baba Mtakatifu amewashukuru watu wa Mungu nchini Msumbiji kwa mapokezi na ukarimu waliomwonesha wakati wa hija yake nchini Msumbiji. Amewapongeza kwa utajiri wa tamaduni, uoto wa asili, furaha na matumaini ya watu wa Mungu nchini Msumbiji. Amewashukuru wadau wote waliojisadaka ili kupyaisha tena mchakato wa amani na upatanisho nchini Msumbiji.

Kwa upande wake, Rais Filipe Jacinto Nyusi wa Msumbiji katika hotuba yake, amelishukuru na kulipongeza Kanisa Katoliki kwa mchango wake mkubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Msumbiji hasa katika sekta ya elimu, afya, ustawi wa jamii na maendeleo fungamani ya binadamu. Uwepo wa wamisionari nchini Msumbiji umewajalia wananchi wengi kupata fursa ya elimu iliyowawezesha kupata ajira na hivyo kukoleza mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Mtakatifu Paulo VI alikuwa ni kiongozi aliyeitakia Msumbiji amani na ustawi kwa kukazia umuhimu wa mshikamano na uhuru wa kweli kwa wananchi wa Msumbiji waliokuwa bado wanaelemewa na kongwa la ukoloni na miaka mitano baadaye,  yaani mwaka 1975 Msumbiji ikajipatia uhuru wake wa bendera.

Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1988 alitembelea Msumbiji ambayo ilikuwa bado imezama katika vita ya wenyewe kwa wenyewe. Hili ni janga ambalo limepelekea maelfu ya wananchi kupoteza maisha; kukimbilia uhamishoni na wengine kupata vilema vya kudumu. Vita ilivuruga umoja, mshikamano na mafungamano ya jamii kitaifa; familia zikasambaratika, uchumi ukachechemea na vijana wengi wakajikuta hawana tena fursa ya ajira. Hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Msumbiji imeongozwa na kauli mbiu “Matumaini, amani na upatanisho”. Baba Mtakatifu ametembelea Msumbiji baada ya kuathiriwa sana na Kimbunga cha Idai kilichopiga nchini Msumbiji mwezi Machi, 2019 na Kenneth kilichosababisha maafa makubwa mwezi Aprili. Katika muktadha huu, familia ya Mungu nchini Msumbiji katika unyonge wake, ikaonja ukarimu, upendo na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa, iliyofufua tena matumaini kwa wananchi wa Msumbiji.

Kwa hakika, kila mtu nchini Msumbiji alijisikia kutoka katika undani wa maisha yake kuguswa na kutikiswa sana na maafa yaliyowakumba ndugu zao. Msumbiji kwa sasa inataka kujielekeza katika mchakato wa matumaini, amani na upatanisho wa kidugu! Mkutano huu umehudhuriwa pia Bwana Ossufo Momade, Kiongozi mkuu wa Chama cha upinzani cha RENAMO. Lengo la Mkataba wa Amani wa mwaka 2019 nchini Msumbiji ni kusitisha vita na mashambulizi dhidi ya watu wasiokuwa na hatia; pamoja na kuhakikisha kwamba, ulinzi na usalama wa Msumbiji unaendelea kuimarishwa. Mkataba huu, unaweka matumaini makubwa katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na upatanisho wa kitaifa.

Rais Nyusi
06 September 2019, 15:27