Tafuta

Vatican News
Ujio na baraka za Baba Mtakatifu Francisko nchini Madagascar zitasaidia kuganga na kutakasa maisha ya wananchi wa Madagascar tayari kupyaisha historia ya maisha yao. Ujio na baraka za Baba Mtakatifu Francisko nchini Madagascar zitasaidia kuganga na kutakasa maisha ya wananchi wa Madagascar tayari kupyaisha historia ya maisha yao.  (ANSA)

Hija ya Papa Francisko nchini Madagascar: Amani, Upendo & Mshikamano

Ujio na baraka za Baba Mtakatifu Francisko zitasaidia kuganga na kutakasa maisha ya wananchi wa Madagascar, tayari kupyaisha historia na maisha yao. Upendo wa Mungu unawawajibisha na kuwaunganisha wananchi wote wa Madagascar, tayari kuchuchumilia na kuambata amani, upendo na mshikamano, ili kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 6-8 Septemba 2019 nchini Madagascar inaongozwa na kauli mbiu “Mpanzi wa amani na matumaini”. Rais Andry Rajoelina katika hotuba yake kwa niaba ya wananchi wa Madagascar, viongozi wa Serikali na kidini, wanadiplomasia pamoja na wawakilishi wa vyama vya kiraia nchini Madagascar walipokutana na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 7 Septemba 2019 amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa ujio na baraka zake za kitume nchini Madagascar, alama ya urafiki kama ule wa Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea nchini Madagascar tarehe 30 Aprili 1989.

Ujio ule uliacha alama ya kudumu katika imani na maisha ya wananchi wa Madagascar. Ujio huu unauwaunganisha watu katika imani, amani na matumaini, tayari kujizatiti zaidi katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Mwaka 2019 unafungua ukurasa mpya ulioshehenu matumaini kwa wananchi wa Madagascar wanaotaka kusimama kidete ili kuhakikisha kwamba, wanaongoza mchakato wa ustawi na maendeleo yao, wakiwa na imani na matumaini makubwa kama wale Waisraeli walipokuwa wanafanya hija kuelekea kwenye Nchi Takatifu. Wananchi wa Madagascar ni watu wenye imani thabiti, matumaini na mapendo sanjari na uzalendo kwa nchi yao. Wanatambua na kuthamini amana na utajiri waliokirimiwa na Mwenyezi Mungu. Hiki ni kipindi cha Injili ya matumaini kwa wananchi wa Madagascar.

Ujio na baraka za Baba Mtakatifu Francisko zitasaidia kuganga na kutakasa maisha ya wananchi wa Madagascar, tayari kupyaisha historia na maisha yao. Upendo wa Mungu unawawajibisha na kuwaunganisha wananchi wote wa Madagascar, tayari kuchuchumilia na kuambata amani, upendo na mshikamano, ili kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Wanaomba baraka ya Mwenyezi Mungu ili kweli kila mmoja aweze kupambana na hali yake, hatimaye, Madagascar iweze kujipambanua kuwa ni nchi ya amani, umoja na mshikamano wa kitaifa. Baba Mtakatifu Francisko katika utangulizi wa hotuba yake, amemsifia sana Rais Andry Rajoelina ambaye ametoa hotuba inayoshuhudia upendo mkubwa alio nao kwa wananchi wake na kwamba, huu ni ushuhuda wa uzalendo kwa nchi yake. Kwa hakika Baba Mtakatifu ameusifu mtazamo na mwelekeo huu wa Rais Andry Rajoelina.

Rais Madagascar
07 September 2019, 15:44