Tafuta

Vatican News
Rais Sergio Mattarella wa Italia anamtakia heri na baraka Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake Barani Afrika kama mjumbe wa amani na upatanisho wa kidugu. Rais Sergio Mattarella wa Italia anamtakia heri na baraka Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake Barani Afrika kama mjumbe wa amani na upatanisho wa kidugu.  (Vatican Media)

Hija ya Papa Francisko Barani Afrika: Mt. Paulo VI Miaka 50 iliyopita!

Hija ya Kitume ya Papa Afrika ni kama sehemu ya kumbu kumbu endelevu ya Jubilei ya Miaka 50 tangu Mtakatifu Paulo VI alipotembelea Bara la Afrika. Anampongeza Baba Mtakatifu anayefanya hija hii kama hujaji wa amani, ushuhuda endelevu wa Kanisa kwa ajili ya kupyaisha mchakato wa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko akiwa njiani kuelekea nchini Msumbiji, Jumatano tarehe 4 Septemba 2019 ametuma salam na matashi mema kwa Marais na wakuu wa nchi mbali mbali ambamo amebahatika kupitia anga zao. Nchi hizi ni pamoja na Italia, Ugiriki, Misri, Sudan, Sudan ya Kusini, Uganda, Tanzania, Malawi pamoja na Zambia. Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia ujumbe Rais Sergio Mattarella wa Italia akimjuza kwamba ameanza hija yake ya kitume kuelekea Msumbiji, Madagascar na hatimaye Mauritius. Baba Mtakatifu anasema, ana kiu kubwa ya kukutana na ndugu zake wapendwa katika imani wanaoishi katika mataifa haya. Anapenda pia kumhakikishia sala zake kwa ajili ya ustawi wa watu wa Mungu nchini Italia.

Rais Sergio Mattarella wa Italia kwa upande wake, amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa ujumbe na matashi mema kwa watu wa Mungu nchini Italia, wakati huu wa hija yake ya kitume Barani Afrika, kama sehemu ya kumbu kumbu endelevu ya Jubilei ya Miaka 50 tangu Mtakatifu Paulo VI alipotembelea Bara la Afrika. Anampongeza Baba Mtakatifu anayefanya hija hii kama hujaji wa amani, ushuhuda endelevu wa Kanisa kwa ajili ya kupyaisha mchakato wa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu ataweza kuwaimarisha watu mbali mbali Barani Afrika ambao wanaendelea kujizatiti katika kutetea na kudumisha utu wa binadamu, upatanisho na maendeleo fungamani. Rais Sergio Mattarella wa Italia anapenda kumhakikishia Baba Mtakatifu sala za watu wa Mungu kutoka nchini Italia.

Rais Mattarella

 

04 September 2019, 15:10