Serikali ya Tanzania imejipanga kuimarisha biashara ya mazao ya kilimo na Nchi wanachama wa SADC. Serikali ya Tanzania imejipanga kuimarisha biashara ya mazao ya kilimo na Nchi wanachama wa SADC. 

Tanzania imejipanga kuimarisha biashara ya mazao kwa nchi za SADC & Afrika Mashariki

Waziri Hasunga amesema huu ni wakati wa nchi za Afrika Mashariki na SADC kuanza kutumia masoko ya ndani ya nchi katika mazao ya kilimo kuliko kutegemea kuagiza kutoka nje ya Afrika. Lengo ni kuimarisha masoko ya mazao mbali mbali nchini Tanzania na hivyo kuwaimarisha wakulima katika kilimo, kuwa na kipato kikubwa kinachokidhi mahitaji yao na kuchangia ukuaji wa uchumi.

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo - Dar es Salaam.

Serikali ya Tanzania imejipanga kuimarisha biashara ya mazao ya kilimo na mengineyo kwa nchi wanachama wa SADC ili kuwanufaisha wakulima katika nchi hizo. Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo tarehe 15 Agosti 2019 wakati akizungumza Mubashara (Live) kwenye kipindi cha Clouds 360 kilichorushwa na Clouds TV wakati wa mkutano wa 39 wa wakuu wa nchi 16 wanachama wa SADC katika ukumbi wa Julius Nyerere International Convention Center. Amesema kuwa zaidi ya watanzania Milioni 50 nchini wanategemea chakula hivyo lazima kubadili mbinu za uzalishaji katika mazao ya kilimo kwa kuongeza tija kupitia teknolojia mpya ili kuwa na uzalishaji mkubwa na wenye tija.

Waziri Hasunga alisema kuwa malighafi zinazohitajika zaidi ya Asilimia 66 zinatokana na mazao ya Kilimo hivyo ukamilisho wa serikali ya viwanda unaungwanishwa kwa ukaribu na sekta ya kilimo. Mkutano wa SADC ni fursa kwa wakulima wa Tanzania kwa kuwa wageni wote waliowasili na watakaoendelea kuwasili watahitaji kula vizuri hivyo mkutano huo ni sehemu ya kuimarisha na kutangaza masoko ya mazao mbalimbali hususani vyakula vya asili. Aidha, utoshelevu wa chakula nchini Tanzania ni asilimia 119% ukilinganisha na mwaka 2018 ambapo ilikuwa asilimia 124% hivyo serikali imefungua mipaka ya kuuza mazao nje ya nchi lakini pia ni lazima kuwa na kumbukumbu muhimu za taarifa zote za usafirishaji wa mazao.

Waziri Hasunga alisema kuwa ni wakati wa nchi za Afrika Mashariki na nchi zote za SADC kuanza kutumia masoko ya ndani ya nchi katika mazao ya Kilimo na mengineyo kuliko kutegemea kuagiza katika nchi zingine nje ya Afrika. Alisema kuwa kufanya hivyo kutaimarisha masoko ya mazao mbalimbali nchini hivyo kuwaimarisha wakulima katika Kilimo chao na kuwa na kipato kikubwa kinachokidhi mahitaji ya kila mkulima ikiwa ni pamoja na uimara wa uchumi wa nchi.

17 August 2019, 11:51