Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa katika mkutano wa TICAD7 amesema amani na utulivu ni kikolezo kikuu cha maendeleo fungamani ya binadamu. Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa katika mkutano wa TICAD7 amesema amani na utulivu ni kikolezo kikuu cha maendeleo fungamani ya binadamu. 

Amani na utulivu ni kikolezo cha maendeleo fungamani ya binadamu duniani!

Waziri Mkuu Majaliwa amesema bila amani ya kudumu Bara la Afrika litashindwa kutimiza mkakati wake wa kujenga uchumi imara. “Tanzania inafanya vizuri kiuchumi miongoni mwa nchi za Afrika sababu kubwa ni amani na utulivu uliopo tangu ipate Uhuru.” Uwepo wa wakimbizi wengi nchini Tanzania unachochewa na amani na utulivu uliopopo sambamba na utatuzi wa changamoto hii.

Na Ofisi ya Waziri Mkuu- Tokyo, Japan.

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema bila kuwa na amani ya kudumu Bara la Afrika litashindwa kutimiza mkakati wake wa kujenga uchumi imara kwa kuwa maendeleo ya bara hilo yanategemea kwa kiwango kikubwa amani na utulivu. Ametoa kauli hiyo Agosti 30, 2019) wakati akichangia mada kuhusu kuimarisha amani na utulivu katika Bara la Afrika kabla ya kuhitimishwa kwa Mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (Tokyo International Conference on African Development – TICAD 7), nchini Japan. Waziri Mkuu ambaye amemwakilisha Rais Dkt. John Magufuli katika mkutano huo, amesema bila amani ya kudumu Bara la Afrika litashindwa kutimiza mkakati wake wa kujenga uchumi imara. “Tanzania inafanya vizuri kiuchumi miongoni mwa nchi za Afrika sababu kubwa ni amani na utulivu uliopo tangu ipate Uhuru.” Ameongeza kuwa uwepo wa wakimbizi wengi nchini Tanzania unachochewa na amani na utulivu uliopopo sambamba na kuwa mstari wa mbele katika kutatua migogoro inayozikumba baadhi ya nchi Barani Afrika. 

Amesema hadi kufikia tarehe 1 Agosti 2019, Tanzania inahifadhi wakimbizi wapatao 305,983 kutoka nchi jirani ambao mara kwa mara wamekuwa wakizikimbia nchi zao kutokana na machafuko yanayosababishwa na vikundi mbalimbali vya uasi vilivyoibuka katika nchi hizo. Hata hivyo, Waziri Mkuu amesisitiza kwamba ni vyema Jumuiya ya Kimataifa ikashirikiana kikamilifu na nchi za Bara la Afrika kuhakikisha kwamba kunakuwepo na amani na utulivu Barani Afrika. Akihitimisha mkutano huo, Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe ameahidi kuwa atahakikisha Azimio la Yokohama (Yokohama Declaration) pamoja na Mpango Kazi wa Yokohama (Yokohama Action Plan) ambao utachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo katika Bara la Afrika unatekelezwa. Mpango huo utaiwezesha Tanzania kunufaika katika miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miradi katika sekta ya nishati, ujenzi, afya na kilimo kutokana na fedha zilizotengwa na Serikali ya Japan kwa ajili ya Bara la Afrika.  Jumla ya Dola za Marekani bilioni 20 zimetengwa na Serikali ya Japan ili zisaidie kugharimia miradi mbalimbali inayolenga kujenga uchumi wa Bara la Afrika.

 



31 August 2019, 15:20