Tafuta

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anawahimiza watanzania kuchangamkia fursa za maonesho ya SADC yaliyofunguliwa rasmi Jijini Dar Es Salaam na Rais Magufulu kutangaza bidhaa zao! Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anawahimiza watanzania kuchangamkia fursa za maonesho ya SADC yaliyofunguliwa rasmi Jijini Dar Es Salaam na Rais Magufulu kutangaza bidhaa zao! 

Watanzania changamkieni Maonesho ya SADC, Dar es Salaam! Kumenoga!

Maonesho ya SADC yaliyofunguliwa na Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania ni fursa kwa Tanzania kutangaza bidhaa na huduma zake na pia ni fursa kwa nchi wanachama wa SADC kutangaza bidhaa na huduma zinazotolewa na nchi hizo, ili watanzania waweze kujionea na hatimaye, kujifunza teknolojia mpya katika uzalishaji pamoja na kukaribisha wawekezaji wa ndani na nje!

Na Mwandishi Maalum, Ofisi ya Waziri Mkuu – Dar es Salaam.

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema wiki ya maonesho ya nne ya viwanda ya nchi za SADC ni fursa pekee ya kutangaza bidhaa zinazozalishwa hapa nchini. Ametoa kauli hiyo Jumanne, Agosti 6, 2019 wakati akizungumza na waandishi wa habari mara ya kukagua mabanda kwenye maonesho hayo yanayoendelea kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam. Maonesho hayo ambayo yalifunguliwa Jumatatu, tarehe 5 Agosti 2019 na Rais John Pombe Magufuli, yanafanyika katika maeneo matatu ambayo ni ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Nyerere, viwanja wa Gymkhana na viwanja vya Karimjee.

“Nimekuja kufanya ufuatiliaji wa maandalizi ya mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi za SADC, nimekuta yanaendelea vizuri. Nimekuja kuangalia mwitikio wa wajasiriamali wa pande zote mbili za Muungano pamoja na wajasiriamali kutoka nchi wanachama wa SADC, na pia mwitikio wa wananchi wetu ukoje,” amesema. Waziri Mkuu amesema fursa hiyo ni muhimu kwa Watanzania kuonesha bidhaa za ndani ili wageni wanaokuja wajue kuna bidhaa zipi zinazozalishwa nchini. “Tumetoa fursa kwa nchi za SADC zote nao pia waoneshe bidhaa zao. Maonesho haya ni ya wazi, Watanzania wanayo nafasi ya kuja kuona na kujifunza,” amesema.

Amesema mbali ya fursa ya masoko, Tanzania inayo pia fursa ya kupata teknolojia mpya na za Kisasa ikiwa ni pamoja na wawekezaji wa viwanda vya usindikaji bidhaa mbalimbali. “Tumeona utaalamu unaotumika kutengeneza bidhaa mbalimbali, hii maana yake ni kwamba tunajifunza na teknolojia zinazotumika,” amesema. “Tunayo fursa ya kukaribisha viwanda kutoka nje ya nchi, wote hapa wameleta bidhaa zao. Pia tunawakaribisha waje waanzishe viwanda kwa ubia na Watanzania. Sisi tunayo ardhi, tunazalisha mazao mengi tu, kwa hiyo mbia wa nje anaweza kuunganisha mtaji na Mtanzania na wakajenga kiwanda hapa nchini,” amesema.

Mbali ya fursa za kiuchumi kwao binafsi, Waziri Mkuu amewataka washiriki wa maonesho hayo, watangaze vivutio vya utalii vilivyopo nchini ambavyo vitasaidia kuwafanya wageni wanaoshiriki mkutano huo watamani kubaki nchini na kuvitembelea. “Watanzania tutumie nafasi hii kutangaza vivutio vingine tulivyonavyo. Mbuga za wanyama tunazo nyingi, tunao Mlima Kilimanjaro ambao ni mrefu kuliko yote barani Afrika na huwezi kuupanda kutokea popote. Ili uupande, ni lazima uje Tanzania,” amesema. “Pia tuna eneo maarufu la Olduvai Gorge ambalo ni chimbuko la binadamu wa kwanza duniani, na hili liko eneo liko Ngorongoro. Tuna fukwe nzuri, zenye mchanga mzuri ambazo ukikaa wala huwezi kuchafuka, zina urefu wa zaidi ya km. 1,400 kutokea Tanga hadi Mtwara,” ameongeza.

Mapema, Waziri Mkuu alifanya kikao na Mawaziri wa Mambo ya Nje, Utumishi na Utawala Bora, Viwanda na Biashara wa SMT, Viwanda, Biashara, Wazee na wa Zanzibar (SMZ), Naibu Mawaziri wa TAMISEMI, Mambo ya Nje na Mifugo na Uvuvi na kuwapa maelekezo ya kuboresha maandalizi hayo. Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Makatibu Wakuu wa wizara hizo.

06 August 2019, 16:16