Tafuta

Vatican News
Dr. Jacques Diouf aliyekuwa Mkurugenzi mkuu wa FAO kati ya Mwaka 1994 hadi mwaka 2011 amefariki dunia huko Paris, tarehe 17 Agosti 2019 akiwa na umri wa miaka 81. Dr. Jacques Diouf aliyekuwa Mkurugenzi mkuu wa FAO kati ya Mwaka 1994 hadi mwaka 2011 amefariki dunia huko Paris, tarehe 17 Agosti 2019 akiwa na umri wa miaka 81. 

Dr. Jacques Diouf, Mkurugenzi wa zamani wa FAO amefariki dunia!

Dr. Jacques Diouf, aliyekuwa Mkurugenzi mkuu wa FAO kuanzia mwaka 1994 - 2011, amefariki dunia tarehe 17 Agosti 2019. Katika salam zake za rambi rambi, Mkurugenzi mkuu mpya wa FAO, Bwana Qu Dongyu amemwelezea Hayati Dr. Diouf kuwa ni kiongozi mchakakazi, aliyejisadaka bila ya kujibakiza katika mchakato wa mapambano dhidi ya umaskini, baa la njaa na utapiamlo wa kutisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, linasikitika kutangaza kifo cha Dr. Jacques Diouf, aliyekuwa Mkurugenzi mkuu wa FAO kuanzia mwaka 1994 hadi mwaka 2011. Amefariki dunia tarehe 17 Agosti 2019 akiwa na umri wa miaka 81 tangu alipozaliwa. Katika salam zake za rambi rambi, Mkurugenzi mkuu mpya wa FAO, Bwana Qu Dongyu amemwelezea Hayati Dr. Jacque Diouf kuwa ni kiongozi mchakakazi, aliyejisadaka bila ya kujibakiza katika mchakato wa mapambano dhidi ya umaskini, baa la njaa na utapiamlo wa kutisha.

Ni kiongozi ambaye alitumia karama na mapaji yake ili kupambana na baa la njaa duniani, kwa kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inakuwa na uhakika wa usalama wa chakula pamoja na sera za kilimo fungamani. Jumuiya ya Kimataifa itaendelea kumkumbuka Dr. Jacques Diouf kwa njia ya Tuzo ya Jacques Diouf inayotolewa na FAO kila baada ya miaka miwili, kwa watu wanaojipambanua katika mapambano dhidi ya baa la njaa na utapiamlo wa kutisha katika ngazi ya kimataifa. Kuanzia mwaka 2014 Dr. Jacques Diouf aliteuliwa kuwa Mwakilishi maalum wa FAO kwenye Ukanda wa Sahel na Pwani ya Pembe ya Afrika.

FAO: Diouf
19 August 2019, 13:45