Tarehe 22 Agosti 2019 kwa mara ya kwanza Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Kuwakumbuka Wahanga wa Vita na Kinzani zenye mlengo wa kidini na kiimani. Tarehe 22 Agosti 2019 kwa mara ya kwanza Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Kuwakumbuka Wahanga wa Vita na Kinzani zenye mlengo wa kidini na kiimani. 

UN: Kumbukumbu ya wahanga wa vita na kinzani za kidini & kiimani

Tarehe 22 Agosti 2019 Umoja wa mataifa unaadhimisha Siku ya Kuwakumbuka wahanga wa vita na kinzani zenye mlengo wa kidini na kiimani. Siku hii, ilianzishwa mwaka 2018 na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Lengo ni kulaani kwa macho makavu bila hata kupepesa macho dhidi ya vita, ghasia, kinzani na vitendo vya kigaidi vinavyofanywa kwa malengo ya kidini au kiimani duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kwa mara ya kwanza katika historia, Jumuiya ya Kimataifa tarehe 22 Agosti 2019 imeadhimisha Siku ya Kuwakumbuka Wahanga wa Vita na Kinzani zenye mlengo wa kidini na kiimani. Siku hii, ilianzishwa mwezi Mei, 2018 na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Lengo ni kulaani kwa macho makavu bila hata kupepesa macho dhidi ya vita, ghasia, kinzani na vitendo vya kigaidi vinavyofanywa kwa malengo ya kidini au kiimani dhidi ya dini kama taasisi au waamini wake. Kwa namna ya pekee, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antònio Guterres, katika ujumbe wake kwenye maadhimisho haya anapenda kuwahakikishia wahanga wa vita, kinzani na vitendo vya kigaidi kwamba, Umoja wa Mataifa utaendelea kujifunga kibwebwe ili kukomesha vitendo vyote hivi vinavyokiuka utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Jumuiya ya Kimataifa itaendelea kulaani mbinu, vitendo na njia zote zinazotumika kwa ajili ya kuendeleza mashambulizi ya kigaidi pamoja na kupandikiza mbegu ya chuki na uhasama kwa njia ya misimamo mikali ya kidini na kiimani. Vitendo vya kigaidi na misimamo mikali ya kidini ni mambo ambayo kamwe hayapaswi kufungamanishwa na dini, taifa, kabila au tamaduni za aina yoyote ile. Lengo ni kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni; kwa kuheshimiana na kuthaminiana hata katika tofauti msingi zinazoendelea kujitokeza kati ya watu wa Mataifa. Majadiliano haya hayana budi kuanzia katika ngazi ya kifamilia hadi ngazi ya kimataifa. Majadiliano katika ukweli na uwazi, yaendelee kuchangia mwelekeo chanya kuhusu mchango wa dini na imani katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusimama kidete ili kupambana na vitendo vya kigaidi, vita na misimamo mikali ya kidini inayohatarisha uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini. Ikumbukwe kwamba, uhuru wa kidini unafumbatwa katika mambo makuu matatu: Mosi ni umuhimu wa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali; Pili, ni kulinda na kudumisha amani na utulivu kama chachu muhimu ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Tatu, ni majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi ni mbinu mkakati inayoweza kuleta suluhu ya migogoro mingi. Uhuru wa kuabudu na kidini ni nguzo ya haki msingi za binadamu na ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu. Uhuru wa kuabudu na kidini unaweza kusaidia kukuza na kudumisha umoja, mshikamano na udugu wa kibinadamu.

Hii ni chachu ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa na kwamba, ukweli na uwazi ni kanuni msingi katika majadiliano ya kidini na kiekumene. Kumbe, hapa kuna haja ya kusimama kidete, kulinda, kutetea na kudumisha uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini umechambuliwa na kufafanuliwa vyema katika Tamko la Haki Msingi za Binadamu. Kwa kuheshimu, kuthamini na kutekeleza haki hizi msingi, Jumuiya ya Kimataifa itaweza kujizatiti zaidi katika mapambano dhidi ya ubaguzi unaoweza kufanywa kwa misingi ya kidini au imani ya mtu. Watu wanapaswa kukuza na kudumisha uhuru wa kujieleza kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi. Vyombo vya mawasiliano ya jamii vinaweza kusaidia kuchangia mchakato wa kuimarisha demokrasia shirikishi sanjari na mapambano dhidi ya mipasuko ya kidini na kiimani.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinabainisha kwamba, kumekuwepo na ongezeko kubwa la vitendo vya ukosefu wa uvumilivu wa kidini na kiimani, sehemu mbali mbali za dunia. Kwa bahati mbaya matukio kama haya yamepenyeza mizizi yake na kujikita hata katika vitendo vya uhalifu kitaifa, kikanda na kimataifa. Katika makundi yote, Wakristo ni kundi la kwanza katika orodha linalonyanyaswa na kudhulumiwa. Inakadiriwa kwamba, asilimia 61% ya idadi ya watu wote duniani, wanaishi katika nchi ambamo uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu hauheshimiwi wala kuthaminiwa. Katika kipindi cha mwaka 2018 kumekuwepo na matukio mengi ya uvunjwaji wa uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu sehemu mbali mbali za dunia, ikilinganishwa na miaka iliyopita.

Wahanga wa Vita
23 August 2019, 10:47