Tafuta

Mkutano wa 39 wa SADC: Vipaumbele: Ulinzi na Usalama; Maendeleo ya viwanda na biashara; Utengenezaji wa fursa za ajira pamoja na kukuza lugha ya Kiswahili. Mkutano wa 39 wa SADC: Vipaumbele: Ulinzi na Usalama; Maendeleo ya viwanda na biashara; Utengenezaji wa fursa za ajira pamoja na kukuza lugha ya Kiswahili. 

Rais Magufuli: Mkutano wa 39 wa SADC: Fursa, Vipaumbele na changamoto kwa nchi wanachama

SADC, kipaumbele cha kwanza ni: usalama, amani na utulivu, maendeleo na ukuaji wa viwanda, biashara pamoja utengenezaji wa fursa za ajira. Amependekeza kwamba, lugha ya Kiswahili iwe ni lugha ya nne itakayotumiwa na SADC, kwani Kiswahili ni kati ya lugha 10 duniani inayozungumzwa na nchi 10 duniani na katika Ukanda wa SADC, Kiswahili kinazungumzwa na nchi wanachama 6.

Na Mwandishi Maalum Dar es Salaam & Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa SADC, amewataka Wakuu Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuendelea kuimarisha Umoja na Mshikamano na kuwa na sauti moja katika kusimamia maslahi mapana ya Jumuiya hiyo katika kuleta maendeleo fungamani kwa wananchi wake. Akifunga Mkutano wa 39 wa Wakuu wa nchi za Jumuiya hiyo, Jumapili tarehe 18 Agosti 2019, Jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli amesema Tanzania ipo tayari kutoa ushirikiano unaohitajika ili kuharakisha jitihada za kuleta maendeleo fungamani kwa nchi wanachama wa SADC. Rais Magufuli katika hotuba yake ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 39 wa SADC, Jumamosi, tarehe 17 Agosti 2019, amezipongeza nchi wanachama wa SADC kwa kuendeleza amani na utulivu, demokrasia na utawala wa sheria. Katika uongozi wa Rais Edgar Chagwa Lungu wa Zambia kama Mwenyekiti wa SADC, Visiwa vya Comoro, DRC, Eswatini, Madagascar, Malawi na Afrika ya Kusini zilifanya chaguzi zake kwa amani na utulivu.

Nchi za SADC zimeendelea kuwa ni kitovu cha amani Barani Afrika sanjari na kuendeleza mapambano dhidi ya sera za ubaguzi wa rangi na ukoloni mamboleo. SADC imeendelea kujikita katika mchakato wa kujenga na kudumisha ulinzi na usalama, chachu muhimu sana katika masuala ya uchumi, siasa na maendeleo fungamani ya binadamu.Kumekuwepo na ukuaji wa Pato Ghafi la Taifa katika nchi za SADC kwa asilimia 22% katika kipindi cha mwaka 2018 na kwamba, utamaduni wa amani unaanza kushika kasi katika eneo hili. Rais John Pombe Magufuli amebainisha changamoto changamani zinazoikabili SADC kwa wakati huu ni pamoja: vitendo vya ugaidi kimataifa, uhalifu wa kimataifa, athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo zimepelekea nchi kadhaa za SADC kukumbwa na mafuriko pamoja na ukame wa kutisha kiasi cha kuathiri utu, ustawi na maendeleo ya wengi katika nchi hizo. SADC inapaswa kushirikiana na kushikamana ili kupambana na changamoto hizi, ili hatimaye, SADC iweze kuwa ni kisiwa na amani, upendo na mshikamano wa dhati.

SADC isimame kidete kutafuta, kulinda na kudumisha amani. Katika uongozi wake kama Mwenyekiti wa SADC, kipaumbele cha kwanza ni: usalama, amani na utulivu, maendeleo na ukuaji wa viwanda, biashara pamoja utengenezaji wa fursa za ajira. Amependekeza kwamba, lugha ya Kiswahili iwe ni lugha ya nne itakayotumiwa na SADC, kwani Kiswahili ni kati ya lugha 10 duniani inayozungumzwa na nchi 10 duniani na katika Ukanda wa SADC, Kiswahili kinazungumzwa na nchi wanachama 6. Rais John Pombe Magufuli  katika hotuba yake ya kufunga mkutano wa 29 wa SADC, Jumapili, tarehe 18 Agosti 2019, amekazia umoja na mshikamano kama kiungo muhimu cha maendeleo fungamani katika ushirikiano wa Jumuiya yoyote, hivyo ili kuleta kasi ya mabadiliko ndani ya Jumuiya hiyo ni wajibu wa nchi wanachama kuhakikisha inatumia vyema rasilimali zake pamoja na kuweka mkazo wa maazimio na agenda za Mkutano wa 39 kwa kutafakari masuala muhimu ya maendeleo.

Rais Magufuli amesema chini ya Uongozi wake, jumuiya hiyo itaendelea kusimama imara na kuwa na nguvu ya pamoja katika kutetea maslahi ya nchi wanachama ikiwemo vikwazo ilivyowekewa  Zimbabwe na kusema Viongozi wa Jumuiya hiyo kwa kauli moja wameungana katika kuitaka Jumuiya ya kimataifa kuondoa vikwazo dhidi ya nchi ya Zimbabwe kwani waathirika ni wananchi wa kawaida. “Tutahakikisha kuwa jumuiya yetu inaondoa changamoto mbalimbali zinazozuia ukuaji wa uchumi ukiwemo vitendo vya rushwa, ufisadi na ukiritimba vinavyokwamisha sekta ya sekta ya biashara baina ya nchi zetu” amesema Rais Magufuli. Akifafanua zaidi, Rais Magufuli amesema katika mkutano huo wa 39, Wakuu wa Jumuiya hiyo kwa pamoja wameweza kuwa na mjadala wa pamoja uliowawezesha Viongozi hao kutoa maoni, ushauri na michango yao na pamoja kusaini itifaki mbalimbali zilizoridhia agenda na mikakati mbalimbali kwa ajili ya kuharakisha maendeleo fungamani ya nchi wanachama wa SADC.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli amesema kutokana na kasi ndogo ya ukuaji uchumi iliyopo kwa sasa ndani ya SADC, amewataka viongozi hao kuhakikisha wanaweka mkazo katika kukuza na kuimarisha sekta ya miundombinu pamoja na kuboresha sera za kifedha na kiuchumi ili kukuza kiwango cha ukuaji wa Pato la Taifa, (GNP) kwa kila nchi mwanachama. Rais Magufuli pia aliitaka Sekretarieti ya SADC  kutumia fedha kwa malengo yaliyokusudiwa badala ya fedha hizo kutumika katika kuandaa makongamano, warsha na semina mbalimbali na sasa zielekezwe katika utekelezaji wa miradi inayoweza kuleta manufaa kwa nchi wanachama ndani ya jumuiya hiyo. “Katika Bajeti yetu ya mwaka 2019/2020 tumepanga kutumia Dola Milioni 74, mchango wa Dola Milioni 43 zinazotolewa na nchi wahisani tunaweza kujenga vituo 17, nitafurahi kuona siku moja Sekretarieti ya Jumuiya yetu ikiwaalika wanachama katika uzinduzi wa vituo hivyo” alisema Rais Magufuli.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amewakaribisha wawekazaji waliopo ndani ya SADC kuja kuwekeza katika miradi ya sekta mbalimbali iliyopo nchini Tanzania ikiwemo nishati, madini, utalii, mifugo, kilimo pamoja na utalii kwani Tanzania imeweka mazingira bora na wezeshi kwa kwa ajili ya wawekezaji na wafanyabiashara.  Akizungumzia kuhusu maombi ya nchi ya Burundi kujiunga na Jumuiya hiyo, Rais Magufulli amesema Sekretarieti ya SADC imepanga kutuma timu ya uchunguzi katika nchini Burundi kwa ajili ya kujiridhisha na masuala muhimu na ya kimsingi yanayopaswa kuzingatiwa kabla ya kukubaliwa kwake kujiunga na SADC. Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Jumuiya hiyo, Dr. Stegomena Tax amesema Mkutano wa 39 wa SADC umekuwa wa mafanikio makubwa kutokana na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa nchi wanachama ambapo wameweza kuweka mikakati ya pamoja itakayosaidia kuongeza kasi ya ukuaji uchumi, biashara na maendeleo fungamani ya Nchi hizo.

Dk. Tax amesema kuwa katika mkutano huo pia, Viongozi wa Jumuiya hiyo waliweza kufanya maamuzi ya kuchagua viongozi wa ndani katika Jumuiya hiyo ikiwemo Nafasi ya Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa, Ulinzi na Usalama ndani ya Jumuiya hiyo (TROIKA) aliyokwenda kwa Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa. Dr. Stegomena Tax wakati wa hotuba yake ya ufunguzi wa Mkutano wa 39 wa SADC, Jumamosi tarehe 17 Agosti 2019 ameipongeza Tanzania kwa kufikia kiwango cha asilimia 7% cha ukuaji wa uchumi, ingawa katika ukuaji wa uchumi mpana wa SADC nchi nyingi zinaendelea kufanya vizuri. Tanzania inapongezwa katika eneo la nishati ya umeme kwa kuhakikisha kwamba, inakuwa na umeme wa uhakika na unaojitosheleza. SADC inaipongeza Tanzania kwa kuamua kuanzisha mradi mkubwa wa umeme katika maporomoko ya Mto Rufiji ambao umezinduliwa hivi karibuni na Rais Magufuli na maendeleo yake ni moto wa kuotea mbali. Huu ni umeme utakaotumika pia na nchi wanachama wa SADC utakapokamilika.

19 August 2019, 09:30