Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, SADC imetiliana sahihi itifaki na mikataba pamoja na marekebisho ya sheria za nchi zao kwa ajili ya utekelezaji wa maamuzi haya, 2019. Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, SADC imetiliana sahihi itifaki na mikataba pamoja na marekebisho ya sheria za nchi zao kwa ajili ya utekelezaji wa maamuzi haya, 2019. 

Mkutano mkuu wa 39 SADC: Itifaki na Mikataba mbali mbali

Nchi wanachama wa SADC wametiliana sahihi kuhusu: Itifaki ya viwanda yenye lengo la kuboresha mazingira ya kukuza viwanda viweze kuzalisha vya kutosha na katika ubora wa ushindani. Itifaki ya kubadilishana wafungwa miongoni mwa nchi wanachama pamoja na makubaliano ya kurekebisha sheria za nchi zao ili kuendana na Itifaki pamoja na makubaliano ya kupambana na uhalifu.

Na Mwandishi maalum – Dar Es Salaam, Tanzania

Wakuu wa nchi 16 zinazounda Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika SADC, Jumapili tarehe 18 Agosti 2019 wametia sahihi  Itifaki na makubaliano mbalimbali kwa ajili ya kuanza utekelezaji. Ambapo  Itifaki iliyosainiwa na wakuu hao ni: Itifaki ya viwanda yenye lengo la kuboresha mazingira ya kukuza viwanda viweze kuzalisha vya kutosha na katika ubora unaoweza kushindana  duniani. Wakuu hao pia wamesaini Itifaki ya kubadilishana wafungwa miongoni mwa nchi wanachama itakayowezesha wafungwa waliohukumiwa nje ya nchi zao kwenda kutumikia kifungo ndani ya nchi zao. Aidha walisaini pia makubaliano ya kurekebisha sheria za nchi zao ili kuendana na Itifaki zilizosainiwa pamoja na makubaliano ya kusaidiana katika mapambano dhidi ya uhalifu wa kimataifa.

Itifaki hizo zimesainiwa wakati wa kufunga mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Kiuchumi Kusini  mwa Afrika SADC uliofanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 17-18 Agosti 2019  ambapo pamoja na mambo mengine wakuu wa nchi 16 zinazounda jumuiya hiyo wamesaini itifaki na makubaliano mbalimbali kwa ajili ya kuanza utekelezaji. Akizungumza katika wakati akifunga mkutano huo Mwenyekiti  wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Rais John  Pombe Magufuli wa Tanzania ameisisitizia  Sekretarieti ya SADC kutumia fedha wanazopata vizuri badala ya kuishia kuzitumia katika warsha, semina na mikutano. Rais Magufuli amependekeza kwa Sekretarieti hiyo kuona umuhimu wa kuanza kutumia fedha hizo katika masuala ya maendeleo fungamani ya binadamu kama vile: elimu, afya, uanzishaji na uboreshaji wa miundombinu. “Bajeti ya Jumuiya yetu inafikia Dola milioni 74 lakini kituo cha afya kinagharimu Shilingi  milioni 400 hadi 500 sawa na dola 200,000 ambazo zipo ndani ya uwezo wa sekretarieti, ” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli pia amesema katika mkutano huo wamepitisha kauli mbiu itakayotumika mwaka mzima 2019-2020 ambayo inasisitiza ujenzi wa viwanda endelevu vitakavyoongeza ufanyaji biashara na kukuza fursa za ajira hasa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya. Kauli mbiu hiyo inasema, “Maendeleo endelevu ya viwanda kuongeza ufanyaji biashara na kukuza ajira,” Rais Magufuli amesema katika mambo waliyoazimia wamehimizana nchi wanachama kuahkikisha zinajenga miundombinu wezeshi ili kuweza kusaidia kukuza uchumi wa nchi hizo pamoja kuboresha sera za uchumi na fedha. Aidha amesema, mambo mengine waliojadili katika mkutano huo ni ombi la nchi ya Burundi kutaka kuingia SADC ambapo walijiridhisha kuwa bado kuna mambo ambayo hayajafanyiwa kazi na kuagiza Sekretarieti kuu kuwapa taarifa hiyo na baadae kwenda kuchunguza kama mambo hayo yamefanyiwa kazi.

Akizungumza kuhusu suala la vikwazo vya kiuchumi kwa nchi ya Zimbabwe, Rais Magufuli amesema wamekubaliana waendelee na mazungumzo na Jumuiya za kimataifa ili kuangalia namna ya kuondoa vikwazo hivyo kwani waathirika wakuu ni wananchi wa kawaida. Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Sekretaieti ya SADC, Dk Stergomena Tax, mkutano huo umekubaliana kuwa tarehe 25 Oktoba 2019, itakuwa ni siku ya kutoa wito kwa Jumuiya ya kimataifa kuondoa vikwazo dhidi ya Zimbabwe. Wajumbe wa SADC wameondoka nchini Tanzania wakiwa na sura mpya ya maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu. Wameridhishwa na ukarimu, umoja na upendo kutoka kwa watanzania. Wamefurahiswa na huduma ya Kiwanja cha Ndege wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere uliozinduliwa hivi karibuni na Rais John Pombe Magufuli. Mafanikio yote haya yataendelea kuiweka Tanzania katika ramani ya maendeleo ya dunia kama inavyostahili. Ukweli lazima usimamiwe na kuheshimiwa na wengi!

19 August 2019, 09:06