Tafuta

Vatican News
Serikali ya Msumbiji chini ya Chama cha FRELIMO pamoja na Chama cha Upinzani cha RENAMO wametiliana sahihi mkataba wa amani, mwanzo wa ujenzi mpya wa Msumbiji! Serikali ya Msumbiji chini ya Chama cha FRELIMO pamoja na Chama cha Upinzani cha RENAMO wametiliana sahihi mkataba wa amani, mwanzo wa ujenzi mpya wa Msumbiji!  (ANSA)

Makubaliano ya Amani Msumbiji: FRELIMO & RENAMO: Matumaini mapya kwa Msumbiji!

Chama cha FRELIMO kimewekeana tena sahihi Mkataba wa Amani na RENAMO chini ya uongozi wa Bwana Ossufo Momade. Lengo ni kusitisha vita na mashambulizi dhidi ya watu wasiokuwa na hatia; pamoja na kudumisha ulinzi na usalama wa Msumbiji. Hakuna tena sababu msingi za vikosi vya ulinzi na usalama vya Serikali ya Msumbiji kushambuliana na majeshi ya RENAMO. AMANI!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji, anasema kwa hakika, Jumuiya ya Mtakatifu Egidio yenye Makao yake makuu mjini Roma, imekuwa ni nyumba ya amani kwa familia ya Mungu kutoka Msumbiji, iliyosaidia FRELIMO na RENAMO kuwekeana sahihi Mkataba wa Amani kunako mwaka 1992 na huo ukawa ni mwanzo wa hija ya amani nchini Msumbiji. Bado kuna changamoto ya kuhakikisha kwamba, amani ambalo ni jina jipya la maendeleo fungamani ya binadamu inadumishwa nchini Msumbiji, lakini hatua kubwa imekwisha kutekelezwa hadi sasa! Mkataba huu ulikuwa ni juhudi za Umoja wa Mataifa, Kanisa Katoliki, Jumuiya ya Mtakatifu Egidio pamoja na Serikali ya Italia. Hayati Askofu Jaime Pedro Gonzalves anakumbukwa sana kwa mchango wake katika mchakato wa haki, amani na maridhiano nchini Msumbiji.

Rais Nyusi amedhamiria na anataka kuhakikisha kwamba, Msumbiji inajenga na kudumisha misingi ya haki, amani na umoja wa kitaifa, ndiyo maana hivi karibuni, Chama cha FRELIMO kimewekeana tena sahihi Mkataba wa Amani na Chama cha RENAMO ambacho kwa sasa kinaongozwa na Bwana Ossufo Momade. Lengo ni kusitisha vita na mashambulizi dhidi ya watu wasiokuwa na hatia; pamoja na kuhakikisha kwamba, ulinzi na usalama wa Msumbiji unaendelea kuimarishwa. Hakuna tena sababu msingi za vikosi vya ulinzi na usalama vya Serikali ya Msumbiji kushambuliana na majeshi ya RENAMO. Mkataba huu, unaweka matumaini makubwa katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na upatanisho wa kitaifa. Wachunguzi wa mambo ya kisiasa wanasema, Mkataba wa Amani umetiwa sahihi kwenye msitu wa Gorongosa, ulioko kwenye Jimbo la Sofala nchini Msumbiji.

Mji huu ni ngome ya Chama cha RENAMO. Rais Nyusi anasema, tayari Serikali ya Msumbiji imeanza mchakato wa kuwanyang’anya silaha wanajeshi wa vikosi vya uasi nchini Msumbiji, ili kuwashirikisha katika vikosi vya ulinzi na usalama vya Msumbiji. Rais Nyusi amekwisha pokea orodha ya wanajeshi waliokuwa msituni ambao wataenda Maputo, tayari kusajiliwa kwenye Jeshi la Polisi nchini Msumbiji. Hivi ndivyo Rais Nyusi na Bwana Ossufo Momade wa RENAMO walivyoamua kuanza kuandika ukurasa mpya wa historia ya Msumbiji, ili kukamilisha mchakato wa majadiliano ya upatanisho na ujenzi wa umoja wa kitaifa yaliyoanza na Hayati Afonso Dhlakama, aliyefariki dunia mwezi Mei, 2018. Vita ya wenyewe kwa wenyewe ilianza kutimua vumbi nchini Msumbiji mara tu baada ya kujipatia uhuru kutoka kwa Wareno mwaka 1975.

Katika kipindi cha miaka kumi na mitano, inakadiriwa kwamba, watu zaidi ya milioni moja walipoteza maisha pamoja na vita kuacha madonda makubwa katika maisha ya wananchi wengi wa Msumbiji ambao walilazimika kuikimbia nchi yao ili kutafuta: usalama na hifadhi kutoka katika nchi jirani. Kunako mwaka 1992, RENAMO kikasajiliwa kuwa ni Chama cha Upinzani, lakini, kikaendelea kuwa na vikosi vyake vya kijeshi. Kati ya mwaka 2013 hadi mwaka 2016 Mkataba wa Amani uliokuwa umetiwa sahihi kunako mwaka 1992 uliingia “mchanga” mashambulizi ya kushtukiza na mauaji ya kinyama yakaanza tena kupandikiza hofu na wasi wasi nchini Msumbiji kutokana na RENAMO kushindwa kuridhia matokeo ya Uchaguzi mkuu uliofanyika kunako mwaka 2014 na FRELIMO kuibuka kidedea! Uchaguzi mkuu nchini Msumbiji unatarajiwa kufanyika tarehe 15 Oktoba 2019.

Wakati huo huo, Familia ya Mungu nchini Msumbiji inaendelea kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya kumpokea na kumkaribisha Papa Francisko; hujaji wa matumaini, amani na upatanisho atakapofanya hija ya kitume nchini Msumbiji, mwezi Septemba, 2019. Bara la Afrika kwa sasa lina kiu kubwa ya: haki, amani, upatanisho na matumaini ya kuweza kuanza upya na kusonga mbele kwa imani na matumaini thabiti pasi na kukata tamaa hasa baada ya matukio ya vita, ghasia na kinzani.

Amani Msumbiji

 

06 August 2019, 10:46