Tafuta

Vatican News
Jumuiya ya Kimataifa kuanzia tarehe 25-30 Agosti 2019 inaadhimisha Juma la Maji Duniani: Kauli mbiu "Hakuna atakayeachwa: Kuongeza kasi ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na usafi. Jumuiya ya Kimataifa kuanzia tarehe 25-30 Agosti 2019 inaadhimisha Juma la Maji Duniani: Kauli mbiu "Hakuna atakayeachwa: Kuongeza kasi ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na usafi.  (ANSA)

Maadhimisho ya Juma la Maji Duniani 25-30 Agosti 2019!

Jumuiya ya Kimataifa kuanzia tarehe 25-30 Agosti 2019 inaadhimisha Juma la Maji Duniani kwa kuongozwa na kauli mbiu “Hakuna atakayeachwa: Kuongeza kasi ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na usafi wa mazingira kwa wote katika dunia inayobadilika kitabianchi”. Hii ni fursa muafaka kwa Jumuiya ya Kimataifa kukabiliana na matatizo, changamoto na fursa za maji duniani kote! UHAI!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maji ni sehemu ya haki msingi za binadamu na inaendelea kuwa ni changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa. Ikiwa kama suala zima la maji halitashughulikiwa kikamilifu, kwa siku za usoni, linaweza kuwa ni chanzo kikuu cha kinzani na migogoro ya kimataifa. Maji safi na salama ni muhimu sana katika mchakato mzima wa maboresho ya afya ya binadamu, ustawi na maendeleo yake. Maji yanaendelea kuwa ni sehemu muhimu ya agenda za Jumuiya ya Kimataifa hasa katika masuala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Lakini, maji yanapaswa kutambulika kwanza kabisa kuwa ni sehemu ya haki msingi za binadamu na kamwe isigeuzwe kuwa biashara inayoweza kumilikiwa na kuendeshwa na makampuni binafsi. Sera na kilimo endelevu zisaidie hifadhi ya ardhi, kwani uharibifu wa mazingira ni chanzo kikuu cha maafa, umaskini na magonjwa. Kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, baadhi ya nchi duniani zimekumbwa na ukame wa kutisha, joto kali na mafuriko ambayo yanaendelea kutishia amani na usalama wa watu na mali zao. Watu wawe makini kutunza mazingira na vyanzo vya maji.

Ikumbukwe kwamba, dhana ya maji kuwa ni sehemu ya haki msingi za binadamu ni agenda iliyoibuliwa hivi karibuni, lakini inaendelea kushika kasi kubwa sana katika Jumuiya ya Kimataifa kutokana na unyeti wake! Ndiyo maana kuna haja ya kuwa na miundo mbinu ya kisheria, kiufundi, kijamii na kisiasa ili kuanzisha mchakato wa ujenzi wa “utamaduni wa utunzaji bora wa maji”. Kwa njia hii, amani duniani inaweza kuimarishwa kwa kuzuia vita, kinzani na migogoro inayoweza kufumbatwa katika mafao ya kisiasa na kiuchumi kwa kubeza utu na maisha ya binadamu! Jumuiya ya Kimataifa kuanzia tarehe 25-30 Agosti 2019 inaadhimisha Juma la Maji Duniani kwa kuongozwa na kauli mbiu “Hakuna atakayeachwa: Kuongeza kasi ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na usafi wa mazingira kwa wote katika dunia inayobadilika kitabianchi”. Hii ni fursa muafaka kwa Jumuiya ya Kimataifa kukabiliana na matatizo, changamoto na fursa zilizopo sehemu mbali mbali za dunia.

Maji kimsingi, ni kichocheo muhimu sana cha maendeleo fungamani ya binadamu hasa katika: kilimo, biashara, utalii, viwanda; ustawi na maendeleo ya wengi. Maadhimisho ya Juma la Maji Duniani ni muda wa kutathmini kuhusu: Utekelezaji, mafanikio, changamoto na hivyo kuainisha utoaji wa huduma ya maji safi na salama; kwa kuendelea kutunza usafi wa mazingira; na kusimamia kikamilifu rasilimali za maji duniani. Shirika la Afya Duniani, WHO na kitengo cha Umoja wa Mataifa kinachoratibu masuala ya maji, UN-Water wameitaka Jumuiya ya Kimataifa kuchukua hatua za dharura zaidi kwa kuwekeza kwenye mchakato wa huduma za maji safi na salama pamoja na mifumo ya huduma za kujisafi. Kukosekana kwa huduma ya maji safi na salama kunaunda mazingira hatari ya maambukizi ya magonjwa sanjari na huduma ya maendeleo katika sekta ya afya ya umma anasema, Dr. Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani.

Kitengo cha Umoja wa Mataifa kinachoratibu masuala ya maji, UN-Water katika taarifa yake kinasema, kimebaini uwepo utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs hususan namba 6, jambo ambalo limesaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha huduma za maji safi na kujisafi. Takribani asilimia 50% ya nchi zilizofanyiwa utafiti kwa sasa zimeweka malengo ya maji safi na salama yanayopania kufikia viwango vya juu ifikapo mwaka 2030, kwa mfano kutatua suala la usalama na ubora wa maji na kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama kwenye makazi ya watu. Kwa upande wake, Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF, takwimu zinaonesha kwamba, kuna watoto zaidi milioni 800 wanaoishi katika mazingira hafifu ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa ajili ya matumizi ya binadamu.

Takwimu zinaonesha kwamba, zaidi ya watoto milioni 220 wanaishi katika mazingira mabaya zaidi ya ukosefu wa maji safi na salama. Ikiwa kama mwenendo huu hauta rekebishwa kuna hatari kwamba, ifikapo mwaka 2030 zaidi ya asilimia 80% ya watu maskini watakuwa wanaishi katika mazingira mabaya sana ya upatikanaji wa maji safi na salama. UNICEF inasema, kuna haja ya kusimama kidete, ili kuhakikisha kwamba, hakuna hata mtu mmoja anayeachwa nyuma ya mchakato wa maendeleo ya maji safi na salama. Ili kufanikisha azma hii, kuna haka ya kuzuia pamoja na kumaliza vita, kinzani na migogoro mbali mbali inayohatarisha usalama na maisha ya watu sehemu mbali mbali za dunia.

Juma la Maji Duniani
29 August 2019, 12:04