Tafuta

Bi Amina Mhammed ametoa sifa kwa viongozi wanawake wa Afrika miongoni mwao ni Rais wa zamani wa Liberia,Ellen J.Sirleaf,wa Malawi Joyce Banda,na wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Catherine Samba-Panza Bi Amina Mhammed ametoa sifa kwa viongozi wanawake wa Afrika miongoni mwao ni Rais wa zamani wa Liberia,Ellen J.Sirleaf,wa Malawi Joyce Banda,na wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Catherine Samba-Panza  

Bi Amina Mohammed awapongeza wanawake viongozi wa Afrika!

Umoja wa Mataifa umepongeza wanawake viongozi Afrika kwa kuweka mjadala wa vizazi tofauti.Hayo yametamkwa na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bi Amina J.Mohammed ambaye ameshiriki mkutano wa mtandao wa wanawake viongozi barani Afrika(AWLN),ulionza tarehe 16-18 Agosti 2019 jijini Nairobi Kenya.Amepongeza mtandao huo kwa kuchukua hatua za kuleta pamoja viongozi wanawake wastaafu,wale wa sasa na viongozi vijana!

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed ameshiriki mkutano wa mtandao wa wanawake viongozi barani Afrika, AWLN, akipongeza mtandao huo kwa kuchukua hatua za kuleta pamoja viongozi wanawake wastaafu, wale wa sasa na viongozi vijana. Bi. Mohammed amesema mtandao huo unaonesha njia ya kwamba, “tunaweza kuvuka tofauti za umri na kuunganisha wanawake, hususan wanawake wa Afrika na kwa pamoja kushughulikia changamoto za dunia zinazotuathiri sote, iwe ni ukosefu wa usawa wa jinsia, maendeleo endelevu, ghasia au haki kwenye tabianchi.”  Miongoni mwa wanawake viongozi walioshiriki ni Rais wa zamani wa Malawi Joyce Banda, Rais wa zamani wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf pamoja na Rais wa zamani wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Catherine Samba-Panza pamoja na viongozi vijana ambao nao walipata fursa ya kuzungumza katika mkutano huo wa siku tatu ulioanza jana tarehe 16 na kumalizika Jumapili tarehe 18 Agosti 2019 jijini Nairobi, Kenya.

Upo umuhimu wa kuleta pamoja wanawake wa vizazi viwili tofauti

Katika hotuba yake, Bi. Mohammed amezungumzia kuletwa pamoja kwa wanawake wa vizazi viwili tofauti na kusema kwamba, “kuna  umuhimu wa mazungumzo kati ya vizazi hivi, kama mkutano huu ili kusisitiza maadili yetu ya pamoja ikiwemo umuhimu wa kutomwacha yeyote nyuma, kuondoa utofauti, stahamala na jamii zisizo na mizozo.” Halikadhalika amesema mashauriano kama hayo yanasaidia kuchagiza urithi wa kiafrika na utambulisho wa kiafrika na pia kuthibitishwa kwamba, “natiwa moyo kuona vijana hawa kimkakati kabisa wakendeleza malengo hayo, ikiwemo kuhoji mifumo iliyopo, kupanga mambo mapya na kutumia vyema teknolojia. Na ninaamini kuwa tunaweza kujifunza sana kutoka kila mmoja wetu na kunufaika na uzoefu wetu wa uongozi.”

Mikutano ya ngazi ya juu mwezi Septemba New York

Naibu Katibu Mkuu aidha amekumbushia pia juu ya mikutano ya ngazi ya juu itakayofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mwezi ujao wa Septemba ambayo itaangazia juu ya mabadiliko ya tabianchi, huduma ya afya kwa wote, tathmini ya malengo ya maendeleo endelevu, ufadhili kwa maendeleo na ule wa nchi za visiwa vidogo.

Usawa wa jinsia:kuna athari hasi za ukosefu wa usawa wa jinisa Afrika

Bi. Mohammed amegusia hata juu ya athari hasi za ukosefu wa usawa wa jinsia barani Afrika na kwamba hugharimu takribani dola bilioni 95 nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara kila mwaka. “Afrika imeweka mwelekeo katika miaka ya hivi karibuni, lakini bado haijafanikisha malengo yake kwa mujibu wa ajenda yake ya 2063. Malengo hayo ni pamoja na asilimia 50 ya wanawake kwenye ofisi za kuchaguliwa katika ngazi ya serikali kuu, kanda na mitaa pamoja na asilimia 50 kwenye nafasi za uongozi. Halikadhalika amesema ukosefu wa usawa wa jinsia unagharimu amani endelevu barani Afrika. “Kuanzia kaskazini mwa Nigeria hadi Sudan, wanawake wakiwemo wasichana wanachukua dhima nzito za kuzuia mizozo na kuchagiza amani. Lakini pale mazungumzo yanapokuwa rasmi, au kipindi cha mpito kinapofika, wanaondolewa sauti zao na kuzimwa na michango yao inakandamizwa! Hata hivyo kwa kusisitiza zaidia amesema, “hii haipaswi kuachwa iendelee na labda tunaweza kuchukua Sudan kama mfano wa kwanza ambako wanawake walihoji mfumo uliopo na kuleta mabadiliko na wanawake ndio wapitisha maamuzi”.

Ushirikiano wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika (AU)

Na wakati wa mahojiano na Bi Mohammed kando ya mkutano huo kuhusu uwepo wa Naibu Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa kwenye mkutano huo kwamba ni kiashiria gani cha uhusiano kati ya Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika amejibu kwamba: “hakika na ni muhimu sana kwa kuwa kwa muda mrefu katika Muungano wa Afrika tulifanikiwa kuwa na usawa wa jinsia kwenye uongozi wa kamisheni zake na sasa tuna usawa wa jinsia kwenye uongozi wa juu na kile tunachotaka kusema kama wanawake ni kwamba tupo hapa kwa sababu tuna uwezo wa kutekeleza majukumu tunayopatiwa.”Aidha amesema kuwa, “kile tunanachotaka kufanya ni kuimarisha zaidi uhusiano na na kuona usawa wa jinsia na idadi usawa katika uongozi kama jambo endelevu si jambo la mara moja na kupita tu”.

Hata hivyo amesema ni kweli kwamba hii ndiyo sehemu ya kuimarisha ubia ambao mwenyekiti wa kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU), Mahammat Faki na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres wako makini kuona kwamba unafanya kazi.” Naibu Katibu Mkuu amesema pia kwamba  wamezindua mfuko wa wanawake ambao ni kwa ajili ya wale wanaosimamia mafungu ya fedha za uwekezaji, “kwa hiyo ni mwelekeo mwingine kabisa, na  si tu kwa ajili ya kujitolea bali kuwezesha watu wachukue jukumu la kusimamia fedha na kuweka usawa kwa wanawake wafanyabiashara.”

Bi AMINA MHAMMED
21 August 2019, 15:30